Tuesday, November 11, 2014

WAISLAM WA MADHEHEBU YA SHIA ITHNA ASHARIYYAH WAMEADHIMISHA MAOMBOLEZO YA IMAM HUSSEIN (A.S), TANDIKA BILAL , JIJINI DAR ES SALAAM.

Viongozi wa taasisi mbalimbali wakiwa katika Maandamano ya Maombolezo ya kifo cha mjukuu wa Mtume (s.a.w.w), yaliyofanyika leo katika Msikiti wa Bilal Tandika,jijini Dar es Salaam,Tanzania.
 
Imam Hussein AS akizungumza Makka alisema: "Ewe Allah! Unajua kile ambacho tunakifanya katika jamii si kwa sababu ya kupata mamlaka na utawala na wala si kwa ajili ya kupata utajiri. Sisi tunataka kuonyesha njia ya dini yako, tufanye marekebisho katika miji yako, waja wako waliodhulumiwa waishi katika utulivu na usalama na waweze kukutii Wewe pasina bughudha. Sisi tumeazimia kutekeleza yaliyofaradhishwa katika Uislamu, Suna ya Mtume SAW na sheria za Allah."

Imam Hussein AS alianzisha mapambano yake ili kutenganisha baina ya haki na batili. Alifahamu kuwa nguvu za utawala wa Yazid ulikuwa umejengeka katika misingi ya batili na iwapo ungeendelea hivyo, basi kungeshuhudiwa kuangamia kazi zote za mitume za kueneza uadilifu na ukweli. Kwa hivyo katika vikao vyake tafauti mtukufu huyo alifafanua na kuweka wazi haki na batili.

Maombolezo ya Kifo cha Imam Hussein (a.s), yamefanyika leo Tandika katika Msikiti wa Bilal, Maombolezo hayo yameudhuliwa na watu mbalimbali wakiwemo Wanawake kwa Waume.
Moja ya sababu nyingine za kudumu harakati adhimu ya Karbala ni uwazi wa mwamko huo. Imam Hussein AS wakati akianzisha mapambano yake makubwa, awali kabisa alibainisha utambulisho wa mapinduzi yake  kwa njia ya wazi kabisa. Aliwafahamisha watu kuwa mapamabano yake yalilenga kupinga dhulma na kuhuisha Uislamu sambamba na kuwaokoa watu kutoka katika shari ya utawala wa Yazid. Alibainisha hata mbinu za mapambano ambazo zilipaswa zitumike.

Kijana wa Hawza ya Bilal, akiongoza Masira kwa nyimbo za huzuni juu ya Imam Hussein (a.s).
Tokea kuumbwa Adam kulikuwepo mapambano baina ya haki na batili na vita vingi katika historia ya mwanaadamu vilijiri kwa ajili ya hayo mawili. Katika kipindi muhimu zaidi, Imam Hussein AS alijitokeza kama mbeba bendera ya haki alipokabiliana na Yazid ambaye alikuwa mbeba bendera ya batili. Ili kulinda haki na kuweka wazi njia yake hadi siku ya qiyama, Imam Hussein AS, familia yake pamoja na wafuasi wake watiifu; wote kwa pamoja walitoa maisha yao muhanga. Ashura ni kielelezo cha vita vya daima baina ya haki na batili na thamani bora dhidi ya upotofu.

Ashura ni tukio ambalo imepita miaka 1373 tokea kujiri kwake lakini si tu kuwa tukio hili la kihistoria linawavutia Waislamu bali pia wapenda uhuru kote duniani wamevutiwa na yaliyojiri katika jangwa la Karbala.
Katika kipindi chote cha historia, kumejiri matukio mengi ambayo akthari yamesahaulika. Lakini tukio la Karbala ni la aina yake kwani tokea kujiri kwake hadi sasa limekuwa likivutia hisia za wengi na kuleta nuru katika nyoyo zilizokuwa kizani.
Siku ya 10 ya mwezi Muharram mwaka 61 Hijria Qamariya, kilio cha Imam Hussein AS na wafuasi wake cha kutaka haki kimebakia na kudumu katika kurasa historia. Leo kilio cha Imam Hussein AS kimewafikia watu wenye kiu cha kusikia kilio cha haki. Tuko katika siku za kukumbuka kuuawa shahidi Mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS na wafuasi wake katika jangwa la Karbala.

No comments: