Tuesday, November 18, 2014

Hamad:Ukawa utasimamisha mgombea mmoja Urais

Katibu Mkuu Wa Chama cha Wananchi CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad
Katibu Mkuu Wa Chama cha Wananchi CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema umoja wa katiba yawananchi Ukawa wakati utakapofika utahakikisha unaweka mgombea mmoja wa Urais aliye madhubuti mwenye uwezo wa kusimamia mabadiliko na kutatua shida zinazowakabili Watanzania.

Maalim Seif amesema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Manzese kwa Bakhresa mara baada ya kumaliza ziara ya kukagua uhai wa chama, kuzindua ofisi mpya za mitaa na Kata katika Wilaya za Temeke, Kinondoni na Ilala Dar es Salaam.

Maalim Seif amesema lengo la ushirikiano wa vyama hivyo ni kuwaongoza wananchi kukikataa CCM kwa vile kwa muda wa miaka 53 kimeshindwa kuweka sera nzuri zitakazowaletea maisha bora Watanzania.

Ameeleza kuwa chini ya Serikali itakayoongozwa na Ukawa kila mtu atakuwa na haki ya kujiamulia ni namna gani anataka kuishi kwa sababu kipaumbe kitakuwa ni kuwapatia wananchi uwezo ukiwemo wa kitaaluma kumuwezesha kila mtu kutumia kipaji chake kuishi maisha bora.

Maalim Seif alisema hayo yanawezekana na zipo nchi kama Korea ya Kusini ambazo zilipata uhuru wake sawa na Tanganyika, lakini nchi hizo zimeweza kupiga hatua kubwa kimaendeleo na kuzikaribia nchi zinazoitwa zimeendelea.

Amesema chini ya utawala wa CCM hali ni tafauti kwa sababu elimu inapatikana kwa matabaka kwa kuzingatia wenye uwezo ambao wanamudu elimu bora na wasiokuwa na uwezo ambao wamekuwa wakiishia katika shule za Kata zenye mazingira duni .

“Huu wetu ni umasikini wa kujitakia, nchi yetu ina utajiri mkubwa kuna kila aina ya madini, lakini wanaonufaika ni wageni na viongozi mafisadi, tushirikiane kuiondoa CCM tujenga Tanzaia mpya yenye matumaini”, alihimzia Maalim Seif. 

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Magdalena Sakaya akizungumza katika mkutano huo alisema kutokana na sera mbaya za CCM nchi imekosa viwanda ambavyo vina nafasi kubwa ya kuleta ajira na kupunguza umasikini miongozi mwa wananchi.

Alisema wakati Tanzania ni nchi inayotegemea zaidi shughuli za kilimo na ufugaji, hakuna viwanda vya kusindika nyama, maziwa wala mazao ya kilimo na kila kitu kinaagizwa kutoka nje ya nchi.

“Hii ni aibu CCM haina sera zenye mwelekeo wa kuwaletea maisha mazuri wananchi, leo hii ni miaka minane wafanyabiashara wadogo wameahidiwa kupatiwa eneo la Machinga Complex lakini hakuna kilichoendelea ni ahadi zisizotekelezwa”, alisema Sakaya.

Mbunge wa Viti Maalum Kulthum Mchuchuri alisema uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Disemba 14 mwaka huu utumiwe na wananchi kukikataa CCM ili iwe salamu tosha kwamba wananchi wameamua kukiweka pembeni.

No comments: