Serikali ipo kwenye mpango wa
kuunda Mamlaka ya Mapato Kuu ya Taifa nje ya Mamlaka ya Mapato ya
Tanzania (TRA) iliyopo kwa sasa ili kuondokana na malalamiko ya kero za
kodi kwa wananchi wenye kipato cha chini.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Alphayo Kidata
alipokuwa akifafanua kuhusu juhudi za Serikali katika kuwasaidia
wananchi wa kipato cha chini kuweza kumudu kulipa kiwango cha kodi
kinachowekwa na na Mamlaka hiyo.
“ Napenda kuwambia umma wa
watanzania kwamba Serikali ya Awamu ya tano inawajali watu wake na ndio
maana imeona kuwa kuna haja ya kuunda Mamlaka moja ya utozaji wa kodi
itakayojumuisha taasisi zote zinazohusika na kukusanya mapato nje ya
kodi na ushuru ili kuondokana na malalamiko mengi ya wananchi juu ya
utozaji wa kodi hasa katika Halmashauri zetu”Alisema Kidata.
Kamishna Kidata amesema kuwa
katika dunia hii hakuna Serikali ambayo imechaguliwa na wananchi ikaamua
tu kuwakandamiza wananchi wake katika jambo lolote lile hivyo basi kwa
sasaserikali ipo katika mchakato wa kuunda Mamlaka hiyo ambayo
itasaidia kuweka viwango vya kodi ambavyo wananchi wa hali ya chini
watamudu kulipa kutokana na biashara au kazi wanazozifanya.
Kamishna huyo ameongeza kuwa
Mamlaka yake kwa kushirikiana na mamlaka nyingine zinazokusanya kodi
katika Halmashauri nchini watahakikisha wanalipatia ufumbuzi suala la
kero ya kodi kwa wananchi wa hali ya chini kwa kupata muafaka ambao
utasaidia pande zote mbili bila kukandamiza upande wowote iwe Serikali
ama mwananchi wa kawaida.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
imekuwa na rekodi nzuri ya ukusanyaji wa kodi ila kumekuwa na malalamiko
mengi kutoka kwa wananchi kuhusu kodi ambazo zimekuwa kero na hazina
tija. Hivyo Serikali imejipanga kuiongezea nguvu Mamlaka hiyo kwa kuipa
uwezo wa kukusanya na mapato ambayo hayatokani na kodi toka katika
wizara, mashirika,tasisi za serikalina Halmashauri zote nchini.
No comments:
Post a Comment