Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali
Khamenei amesema, wananchi wa Iran wameonesha kivitendo imani yao kwa
Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi
uliofanyika nchini hivi karibuni.
Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo katika mkutano wa mwisho na
Mkuu pamoja na wajumbe wa Baraza la nne la Wanazuoni Wataalamu
wanaomchagua Kiongozi Mkuu.
Amewasifu na kuwapongeza wananchi kwa
kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Februari 26 na kueleza kwamba:
Wananchi waling'ara vizuri katika uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya
Kiislamu na wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu kutokana na asilimia 62 ya
waliotimiza masharti kushiriki katika upigaji kura; na hicho ni kiwango
cha juu kulinganisha na nchi nyingi zinazojigamba kuwa za kidemokrasia.
Huku akibainisha kuwa wananchi wametimiza wajibu wao kwa kujitokeza
kupiga kura katika uchaguzi, Kiongozi Muadhamu amesema sasa ni zamu ya
viongozi kutekeleza majukumu yao.
Ayatullah Khamenei amesema jukumu la Baraza la Wanazuoni Wataalamu ni
"Kubakia katika hali ya Kimapinduzi, Kufikiri Kimapinduzi na Kufanya
Kazi Kimapinduzi", na akafafanua kwa kusema, kuzingatia sifa hizo tatu
maalumu katika namna ya kumchagua Kiongozi Mkuu wa baadaye wa nchi ni
miongoni mwa mas-ulia makuu liliyonayo baraza hilo, na kwamba katika
kumchagua Kiongozi wa baadaye ni lazima kuweka kando ucheleaji, muhali
na kufikiria mambo kimaslahi.
Katika hotuba yake hiyo mbele ya wajumbe wa Baraza la Wanazuoni
Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu, Ayatullah Khamenei ameashiria pia
majukumu ya viongozi wa serikali na kusema: Katika mazingira ya hivi
sasa viongozi wazingatie na kuvipa umuhimu vipaumbele vitatu ikiwemo
uchumi wa muqawama, kuendeleza kwa kasi harakati ya kielimu na kuipa
kinga kiutamaduni nchi, taifa na vijana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza bayana kwamba
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuwa na maelewano na ulimwengu
mzima isipokuwa Marekani na utawala wa Kizayuni.
Aidha amevielezea kuwa ni vya kisiasa tu vita vinavyoendelea hivi
sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na kutahadharisha kwa kusema:
Maadui wa Uislamu wanajaribu kuzigeuza hitilafu hizi kuwa za kimadhehebu
ili zisiweze kuhatimishwa kirahisi, hivyo haipasi sisi kuwasaidia
kufikia lengo hili hatari"chanzo irib
No comments:
Post a Comment