Bismillah Rahmani Rahimu
“Amani iwe
juu yangu siku niliyozaliwa, siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa” Quran
19 aya 33.Maneno ya Nabii Issa (a.s) au Yesu Kristo
Watanzania
wenzangu Waislamu na Wakristo, Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu nyote.
Katika siku hii ya leo sisi kama Waislamu wa Madhehebu ya
Shia Ithnasheriya Tanzania tunapenda kutoa Mkono wa Kheri , Mkono wa Baraka,
Mkono wa Fanaka kwa watanzania wote wakristo na wale wasiokuwa wakristo kwa
mnasaba huu na kwa eid hii kubwa ya kuzaliwa Yesu Kristo au Issa Ibn Mariam.
Tunatoa Mkono huu wa Kheri, Mkono huu wa Baraka uliojaa
Mahaba, uliojaa Upendo, uliojaa Ushirikiano, uliojaa uzawa, uliojaa Utanzania,
uliojaa kupenda nchi yetu kama watanzania sote tunaokusanywa na jina la
Tanzania nan chi ya Tanzania, Namuomba Mungu wakristo wote wa Tanzania,
Waafrika na Duniani Waisheherekee Eid hii kubwa ya Mazazi ya Yesu Kristo kwa
kuzidi Upendo , kwa kuzidi Maelewano na kuzidi Mshikamano.
Napenda katika tukio hili wa Eid hii ya Krismas, Furaha hii
ya Krismas kwa ndugu zetu wakristo wa Tanzania na wengine, napenda ninakili
Quran takatifu katika sura ya 19 aya ya 33, Quran 19 aya 33 Mwenyezi Mungu
anazungumzia Mazazi ya Nabii Issa (a.s) au Mazazi ya Yesu Kristo anasema Maneno
yafuatayo “Maneno haya anayatamka Yesu
Kristo au Issa ibn Mariam (a.s) ndani ya Quran Surat Mariam aya ya 33 anasema
Yesu au Issa.
“Na amani iwe kwangu Mimi siku niliyozaliwa na siku nitakayo
Kufa na siku nitakayofufuliwa nikiwa hai” Maneno haya ameyatamka Nabii Issa
(a.s) au Yesu Kristo wakati amezaliwa bado ni Mtoto Mdogo, Mayahudi wanamtilia
Shaka Mariya Bikira au Mariamu ,kwamba
Vipi umempata Mtoto kabla ya kuolewa? Anadhibitisha Yesu Kristo au Issa (a.s)
yakwamba Amani iwe juu yangu siku hii ya leo na siku nitakapo kufa na siku nitakapo
fufuliwa.
Maneno haya yanatufunza nini? Na huu ndio ujumbe Muhimu wa
Krismas yetu hii ya mwaka 2018 na 2019, kwamba Yesu Kristo na Mitume wengine
wote, Yesu Kristo au Issa (a.s) anazaliwa, anachozaliwa nacho anasema
nimezaliwa kuenzi amani ndio kitu cha
kwanza ametoka nacho, kwahiyo huu ni Ujumbe Mkubwa unaozungumzwa ndani ya Quran
katika siku hii ya mazazi ya Yesu Kristo au Issa (a.s), mafunzo ya kuenzi
amani, lakini kuenzi amani katika Nyanja gani?
Ni katika Nyanja tano Muhimu lazima kuenziwa amani, Nyanja ya kwanza lazima
kuenziwa amani kwenye Nyanja na kiwango cha mtu mmoja mmoja, lazima kila
Mwanadamu aishi kwa amani kama alivyoitangaza Issa (a.s) au Yesu Kristo siku
anayozaliwa , amani iwe kwangu siku nilipozaliwa , siku nitakapo kufa na siku
nitakapo fufuliwa , maisha yangu yote ni maisha yanayogubikwa na amani na
mitume wote maisha yao yaligubikwa na amani mpaka siku yao ya mwisho.
Kwahiyo ni lazima tuenzi amani kwa kiwango cha mtu mmoja
mmoja, mtu anapofanya kazi anapotekeleza wajibu wake huyo amekaa kwa amani, Mtu
anapomuabudu Mungu, Jumapili akaenda Kanisani, Ijumaa akaenda Msikitini huyo
anaishi kwa amani, mtu anaekaa Vizuri na Jiraani na wenzake huyo anaishi kwa
amani.
Pili kuishi kwa amani kwa kiwango cha familia, familia yoyote
inayopendana , baba anaependana na watoto wake, anaependana na mkewe, hiyo ni
familia inayoishi kwa amani. Familia yoyote inayowafundisha watoto
inayowapeleka watoto shule wasome ,wajifunze, ni familiya inayoishi kwa amani.
Familiya inayoishi katika kulinda ada,kulinda taratibu za Kiafrika, za
Kikabila, ,mambo mazauri tuliyokuwa nayo ya kiafrika kuyaenzi huku ni kuenzi
amani.
Jambo la tatu ni amani kwa ustawi wa Kijamii, Jamii amabyo
haitumii madawa ya Kulevya, jamii ambayo haina mambo ya Ushoja, jamii
iliyosalimika na mambo ya mahusiano machafu na mabaya, hiyo ni jamii inaishi
kwa amani.kwa hiyo jamii iliyosalimika na hayo ni jamii inayoishi kwa amani.
Kwahivyo siku hii ya Mzazi ya Issa (a.s) au Yesu Kristo
ametangaza kwamba yeye amezaliwa kwa amani, ameishi kwa amani na atakufa kwa
amani Tuienzi amani tutakuwa tumemuenzi Issa (a.s) , tukienzi amani tutakuwa tumemuenzi Yesu
Kristo.
Jambo la Nne ni kuilinda amani au ni kuitazama amani kwenye
kiwango cha Kitaifa, Taifa linaloenzi amani ni taifa la aina gani? Ni Taifa
linalojitahidi kufuta Ujinga kwa wtu wake, taifa linaloishi kwa amani ni taifa
linalojitahidi kufuta maradhi katika jamii yake, taifa linalohimiza watu wake
wafanye kazi kwa bidii, taifa ambalo linawatumikia watu wake, hilo ni taifa
linaloenzi amani na linaloishi kwa amani.
Mwisho ni kuenzi amani kwa mustawa wa Kimataifa, yoyote yale
ambayo yameathiri mataifa mengine, yamesababisha uvunjifu wa amani uwepo katika
mataifa mengine, kuenzi amani kimataifa nikujitahidi yale yote mabaya yasifike
katika ardhi ya Tanzania. “Amani iwe juu yangu siku niliyozaliwa, siku nitakayokufa
na siku nitakayofufuliwa” Quran 19 aya 33.
Huu ni Ujumbe wa Yesu Kristo au Yesu (a.s) ndani ya Quran
siku aliyozaliwa , ni Mtu wa Amani ni mpenda amani, ni mpenda watu nan i mpenda
jamii na hayo ndio maisha ya Mitume wote akiwemo Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Nawatakieni Krismas Njema, nawatakieni watanzania wanaoienzi
amani, wanaopenda amani, wanaokaa Vizuri, wanaoelewana na wanaoshikamana,
asanteni sana na Mungu awabariki katika Krismas yenye Baraka na kheri tele,
Mungu ibariki Tanzania.
Imetolewa na: Maulana
Sheikh Hemed Jalala Kiongozi Mkuu wa Waislamu Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania
No comments:
Post a Comment