Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Russia na
Uturuki wametoa taarifa ya pamoja na kutangaza kuwa nchi hizo tatu
zinaunga mkono utawala, uhuru na kulindwa mipaka yote ya Syria.
Baada ya mkutano wao mjini Moscow Jumanne ya leo, mawaziri
Mohammad Javad Zarif wa Iran, Sergei Lavrov wa Russia na Mevlut
Cavusoglu wa Uturuki wametoa taarifa ya pamoja na kusuema: "Nchi hizi
tatu zinaamini kuwa mgogoro wa Syria hauna utatuzi wa kijeshi." Aidha
wametilia mkazo nafasi ya Umoja wa Mataifa katika kutatua mgogoro wa
Syria kwa mujibu wa azimio nambari 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Iran, Russia na Uturuki zitashiriki
katika jitihada za pamoja huko Aleppo mashariki mwa Syria kwa lengo la
kuwaondao kwa hiari raia na pia kuwaondoa kwa taratibu wapinzani wenye
silaha."
Nchi hizo tatu pia zimesisitiza umuhimu wa kusitishwa vita, kutoa
huduma za kibinadamu na kuwawezesha Wasyria kufika maeneo yote ya nchi
yao pasi na pingamizi lolote.
Halikadhalika wametangaza kuwa tayari kuandaa mazungumzo baina ya
wapinzani na serikali ya Syria huku wakisisitiza azma yao ya pamoja ya
kupambana na makundi ya kigaidi ya ISIS na Al Nusra. Mawaziri hao watatu
pia wamesisitiza ulazima wa baadhi ya nchi za Magharibi na eneo la
Mashariki ya Kati kusitisha mara moja uungaji mkono kwa makundi yenye
silaha nchini Syria.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutolewa taarifa hiyo,
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran amesema ugaidi haupaswi kutumiwa kufikia
malengo ya kisiasa hata kama ni ya muda mfupi kwani ugaidi ni tishio
hatari na watu wote wanapaswa kushirikiana kuuangamiza.
No comments:
Post a Comment