Tuesday, December 20, 2016

Kambi ya upinzani Congo yawataka wananchi kupinga utawala wa Kabila

Kambi kuu ya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewataka wananchi kutomtambua tena Joseph Kabila kama rais wa nchi hiyo na imewahimiza kuonesha upinzani wao dhidi ya Kabila kwa njia ya amani.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), Etienne Tshisekedi, ameitaja hatua ya Rais Kabila ya kuwa madarakani kwa awamu ya tatu kuwa ni kinyume na sheria na kwamba jitihada zake za kutaka kubakia madarakani ni mapinduzi ya kijeshi.

Tshisekedi pia ameitaka jamii ya kimataifa kutoamiliana na Joseph Kabila kama Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
 
Ripoti mbalimbali zinasema kuwa maandamano yameshuhudiwa katika maeneo na miji mbalimbali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kama Lubumbashi na Goma.
Hali ya wasiwasi ilionekana katika miji na maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na milio ya risasi imesikika mapema leo katika mji mkuu, Kinshasa. Baadhi ya ripoti zinasema raia wawili waliuawa kwa kupigwa risasi na jeshi la serikali ya Kabila katika usiku wa kuamkia leo katika kitongoji cha Kingabwa mjini Kinshasa.
Joseph Kabila
Awamu ya pili ya uongozi wa Rais Joseph Kabila ambaye anaiongoza Congo kwa miaka 15 inamalizika rasmi leo. Kabila alichukua madaraka ya nchi mwaka 2001 baada tu ya kuuliwa baba yake, Laurent Kabila.

No comments: