Thursday, October 15, 2015

Kumbukumbu ya Mwaka Mpya wa Kiislam

Sheikh Hemed Jalala, Mmoja wa Viongozi Wakuu wa Kiroho wa Waislam, Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania. Kushoto kwake ni Naibu Mkuu wa Chuo cha Kiislam cha Imam Swadiq (a.s).Leo Masjid Ghadir, Kigogo-Post Dar es salaam


Hawa ni baadhi ya wanahabari wakiwa makini katika kumsikiliza Sheikh Hemed Jalala
Habari Kamili


Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufikia mwaka 1437, baadhi yetu tukiwa wazima, pia Mwenyezi Mungu awape afya wale wenye maradhi na awatie nguvu wale wanyonge.

Usiku wa leo ni tarehe 1 muharram 1437, sawa na tarehe 15 Oktoba 2015. Lakini siku ya leo, watanzania wanaadhimisha siku aliyofariki baba wa taifa hili Mwl. J.K Nyerere (14/Oktoba). Tunatoa mkono wa pole kwa familia ya Mwl. Nyerere, kwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watanzania wote.

Baba wa taifa anakumbukwa kwa mambo mengi katika historia ya nchi yetu. Kama waziri mkuu wa kwanza wa Tanganyika, Kama rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kama miongoni mwa viongozi walioongoza mapambano ya kumuondoa mkoloni Tanzania na afrika kwa ujumla.

Tunafanya haya kwakurejea maneno ya Imam Ali (a.s) katika nahjul balagha, maneno yaliyonukuliwa na aliyekuwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Bwana Koffi Annan (1997-2006) kuwa “ watu ni aina mbili, aidha  ni ndugu yako katika dini au ni ndugu yako katika damu (nasabu). Kwahiyo tunakila sababu ya kutoa mkono wa pole kwa watanzania.

Pili, leo katika historia baada ya maghrib, waislam kwa kuzingatia kalenda ya mwezi (lunar calender) tunaukaribisha mwaka mpya wa kiislam (1437 .H). Katika kuukaribisha, hatuna budi kufahamu pia kuwa mwaka uliopita (1436 H) ulimwengu wa kiislam ulikumbana na changamoto nyingi. 
Kuna haja ya kujifunza kutokana na changamoto hizo. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na maafa ya mahujaji ambapo maelfu ya mahujaji wamepoteza uhai wao, hatutosita kuzitaka mamlaka husika kuwajibika kwa hilo.

Pili, vita nchini Syria na Yemen ambazo msingi wake mkuu ni kukithiri kwa ubepari /ubeberu ulimwenguni na kuibuka kwa makundi ya kukufurishana (takfiir groups).

Tatu, kumomonyoka kwa maadili miongoni mwa wanajamii hasa baada ya kutangazwa kwa uhalali wa ndoa za jinsia moja kwa nchi za magharibi, hivyo kuathirika kimaadili na kiuchumi kwa nchi nyingi tegemezi.

Tatu, kushuka kwa bei ya nishati ya mafuta duniani ambayo kwa kiasi kikubwa nchi nyingi zilizoathirika ni za ukanda wa ASIA ambazo zinaidadi kubwa ya waislam.

Nne, ni kukithiri kwa mauaji ya watu wenye albinism, hali iliyopelekea wajihisi kuwa ni raia wa daraja la tatu nchini Tanzania.

Tano, kuchomwa kwa baadhi ya nyumba za ibada na kudhuriwa kwa baadhi ya viongozi wa dini nchini Tanzania.

Mwisho, leo (usiku, 15/10/2015 sawa na 1 Muharram 1437) katika ulimwengu wa kiislam, waislam na wapenda haki wote duniani tunakumbuka matukio ya kuuwawa kikatili mjukuu wa Mtume (s.a.w.w), Imam HUSSEIN (a.s). 
Kwa ufupi, Imam Hussein  ni kiongozi aliyeonesha dira ya namna ya kupambana  na DHULMA ulimwenguni kama Mahatma Gandhi (Baba wa Taifa la India) na Rabindranath Tagore walivyomulezea Imam Hussein katika maandishi mbalimbali wakihusianisha mafanikio ya harakati nyingi za kudai haki na Imam Hussein (A.S).

  Kwa huzuni kabisa, tunatoa mkono wa pole kwa Mtume (s.a.w.w) na familia yake (Ahlulbayt), pia kwa waislam wote ulimwenguni na wapenda haki pasina kujali imani zao.

Imam Hussein ni kielelezo cha utu, uadilifu, na amani. Pia ni ishara ya ukombozi wa viumbe na ni kielelezo cha kupinga dhulma ulimwenguni.

Kaulimbiu ya mwaka huu:

IMAM HUSSEIN (A.S) NI DARASA JUU YA UHURU WA BINAADAMU NA UPINGAJI WA DHULMA.



IMETOLEWA Na: Sheikh Hemed Jalala

Mmoja wa Vingozi  Wakuu wa kiroho wa waislam dhehebu la shia Ithnasheriya Tanzania.

No comments: