Saturday, August 20, 2016

Waziri Simbachawene awataka Watendaji wanaosimamia Uendeshaji wa Elimu kuzifanyia kazi taarifa za Wadhibiti Ubora wa Elimu.

EM1 
Waziri wa Nchi  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George Simbachawene amewataka Watendaji wanaosimamia uendeshaji wa Elimu katika ngazi ya Mkoa, Halmashauri na Shule kuzingatia kwa ukamilifu ushauri unaotolewa na Wadhibiti Ubora wa Elimu wanaoutoa kutokana na kasoro kadhaa wanazobaini katika maeneo wanayoyakagua ili kuhakikisha kuwa watoto na vijana wanapata elimu bora siyo tu kwa maisha yao ya baadaye bali pia itakayowawezesha kulitumikia taifa kwa weledi na uadilifu
.
Akifungua kikao cha siku mbili kati ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( OR-TAMISEMI) na Maafisa Elimu wa Mikoa,Wakuu wa shule Kongwe na Wakuu wa zilizoungua moto kinachofanyika mjini Dodoma tarehe 18-19 Agosti mwaka 2016, Mhe. Simbachawene amesema kushindwa kufanyia kazi kasoro zinazojitokeza au kutambuliwa na Wadhibiti Ubora ni sawa na kuhujumu jitihada za serikali za kuwaandalia maisha bora vijana wake.

“Nitumie wasaa huu, kuwaagiza watendaji wote mnaohusika katika eneo hilo kushughulikia kikamilifu kasoro zote zinazotambuliwa hususani zile ambazo ziko ndani ya mamlaka za uwezo wenu na kama ziko juu ya uwezo wenu, basi ziwasilisheni kwa wakati kwa mamlaka husika. Wizara yangu haitasita kuchukua hatua stahiki kwa wale wote watakaozembea kutimiza wajibu wao. Alisisitiza Mhe. Simbachawene.
EM2
Mhe. Simbachawene alisema  serikali ya awamu ya tano imeifanya elimu kuwa ni moja ya vipaumbele vyake na kuwekeza mabilioni ya fedha katika kuendesha na kutekeleza miradi  ya mbalimbali ya elimu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

Alisema miongoni mwa mambo ambayo serikali imeyafanya katika kuboresha elimu nchini ni pamoja na kuwaendeleza walimu kazini kupitia Mipango mbalimbali, kutoa fedha za Ruzuku, kutoa fidia ya ada, chakula na maabara kila mwezi, kuwanunulia  pikipiki  Waratibu Elimu Kata wote, kutengeneza madawati kwa shule za msingi na sekondari,kusambaza vitabu kwa darasa la Kwanza pamoja na kusambaza vitabu vya Sayansi na Hisabati kwa shule za Sekondari.

Mambo mengine aliyoyataja ambayo yamefanywa na Serikali katika kuboresha elimu kuwa ni pamoja na Ujenzi wa Maabara, Ukarabati wa shule kongwe, ukarabati wa shule za ufundi, utoaji wa mafunzo ya uongozi kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata pamoja na utoaji wa Posho ya Madaraka kwa Walimu Wakuu wa shule na Waratibu Elimu Kata ambapo alisema kutokana na mambo hayo  hakuna sababu za msingi za shule kutofanya vizuri.

Alisema kwa muda mrefu sasa, matokeo ya mitihani yanaonyesha kuwa taaluma ya shule kongwe inaendelea kushuka na baadhi ya shule hizo kuwa za mwisho katika mitihani ya kidato cha sita ambapo alitolea mfano wa shule za sekondari za Tabata na Iyunga kuwa za mwisho katika mitihani ya kidato cha sita mwaka 2015 na shule za sekondari za Kwiro na Azania kuwa za mwisho kwa mwaka 2016.

Aliwataka washiriki wa kikao hicho kujadili na kuona kuwa jukumu na wajibu wa kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu kwa ujumla pamoja na kujadiliana ili kupata mapendekezo ya mbinu na mikakati ya kuondokana na changamoto za uendeshaji na usimamizi wa shule ambazo hivi sasa zinaendelea kuporomoka kitaaluma.

Mhe. George Simbachawene aliyataja maeneo ambayo yanaweza kutoa mchango hasi katika utoaji wa elimu kwa shule kongwe za sekondari na msingi kuwa ni usimamizi dhaifu katika ngazi ya shule za kata,kutowachukulia hatua stahiki na wakati walimu wasio wajibika,kutozifanyia kazi taarifa za ukaguzi, maandalizi duni ya walimu kabla ya kufundisha pamoja na walimu wa masomo ya sanaa kushindwa kuwajibika kikamilifu licha ya idadi yao kuwa kubwa.
 EM2
Alisema matukio ya kuungua kwa shule kutokana na ajali za moto ambazo zimekuwa zikitokea hivi karibuni zimekuwa zikiisononesha serikali , wanafunzi, wazazi  na watanzania wote kwa ujumla kwakuwa maeneo yaliyopatwa na majanga ya moto yameathirika kwa kiasi kikubwa.

“ Taarifa za uchunguzi za awali ambazo tumekuwa tukizipokea zimeonyesha kuwa chanzo cha ajali nyingi za moto ni hitilafu ya umeme. Pamoja na taarifa hizo , tumeendelea kupata mashaka zaidi pale ambapo shule nyingine zilizopatwa na janga la kuungua moto hazina hata  miundombinu ya umeme. Tunashukuru kwa ushirikiano tunaoupata kutoka kwenye vyombo vyetu vya usalama ambavyo mpaka sasa vinaendelea na uchunguzi wa kina ili kupata chanzo halisi cha matukio hayo. 

Alisema Mhe. Simbachawene.
Kikao hicho cha siku mbili kinalenga katika kujadiliana juu ya Usimamizi na Uendeshaji wa shule kongwe za sekondari za serikali na kuangalia ni kwa jinsi gani kiwango cha elimu katika shule hizo katika shule hizo kinainuliwa.

Kikao hicho pia kililenga katika kujadiliana kuhusu matukio ya kuungua kwa moto kwa shule za sekondari za bweni na zenye hosteli katika sehemu mbalimbali hapa nchini.

Akimkaribisha mgeni rasmi kufungua kikao hicho, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na  Serikali za Mitaa Bw. Bernard Makali amesema kuwepo kwa udhaifu katika usimamizi wa elimu katika ngazi ya shule ambao umesababisha ufundishaji katika shule kongwe kuwa wa kusuasua na kusababisha shule mhizo kushuka kitaalamu na kushika nafasi za mwisho kwenye mitihani ya kitaifa ambapo aliwataka washiriki kutumia kikao kupata mbinu sahihi ili kuweza kuinua kiwango cha ufaulu katika shule za serikali na za binafsi.
Kwa picha zaidi Click http://tamisemi.blogspot.com/

No comments: