Serikali imejenga vituo 22 vya
kutolea huduma za makataba katika Mikoa mbalimbali hapa nchini ili
kuimarisha mfumo wa kutoa elimu kwa wananchi.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es
salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mipango toka Bodi ya Huduma za makataba
(BOHUMATA) Bw. Comfort Komba wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Komba amesema kuwa huduma za
maktaba zimefika katika Mikoa 22,Wilaya 19 na tarafa 2 ikilinganishwa na
vituo 17 vilivyokuwa Mikoani na 15 katika Wilaya mwaka 2005.
“BOHUMATA imeshirikiana na
Halmashauri za Wilaya za Ruangwa,Chunya,Masasi,Mbulu na Ngara katika
kuanzisha na kuimarisha Maktaba Mpya katika Halmashauri hizo.”
Alisisitiza Komba.
Aliongeza kuwa uanzishwaji wa
maktaba katika maeneo mbalimbali hapa nchini umesaidia kuongeza na
kuhamasisha utamaduni wa kujisomea miongoni mwa wanajamii ikilinganishwa
na hali ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa kwa maktaba hizo .
Akitaja mafanikio mengine Komba amesema ni ongezeko la kiwango cha elimu,maarifa,taarifa na ujuzi miongoni mwa wanajamii .
Pia Komba alitoa wito kwa
watanzania na wasio watanzania kujenga utamaduni wa kutumia maktaba za
umma kwa kuwa zipo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote.
Bodi ya Huduma za maktaba Tanzania
(BOHUMATA) ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 6 mwaka 1975 ikiwa na
jukumu la kuanzisha,kusimamia,kuongoza,kuimarisha,kutunza na kuendeleza
maktaba za umma ili kujipatia elimu,maarifa,taarifa,mbalimbali
zitakazowasaidia katika kujiletea maendeleo.
No comments:
Post a Comment