Hatimaye aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa ametangaza
kustaafu rasmi siasa baada ya chama hicho kumpokea Edward Lowassa na
timu yake anayodai ni timu ya mafisadi.
Alifafanua kuwa alihoji maswali mengi na kutaka majibu kama wangetaka
akubaliane na mapendekezo yao. Suala kubwa alilohoji ni iwapo ujio wa
Lowassa na watu wake ni mtaji kwa chama hicho au ni mzigo kwa chama
hicho lakini hakupewa majibu.
Amesema baada ya viongozi hao wa Chadema kumshawishi kuwa Lowassa
angekuja na timu kubwa ya wabunge 50 walioko madarakani hivi sasa kwa
tiketi ya chadema pamoja na wakuu wa wilaya kadhaa, aliwataka wamletee
majina yao pamoja na sharti la kuwataka kutangaza kuhama CCM kabla ya
mchakato wa kura za maoni za kuwapata wabunge.
Amesema hata hivyo walishindwa kufanya hivyo na kisha kuamua kushiriki
mchakato wa kura za maoni huku wakihama baada ya majina yao kukatwa
jambo ambalo amedai limefanya Chadema kuendelea kupokea ‘makapi’ ya CCM.
Alisema Lowassa ndiye kinara aliyelazimisha kampuni hewa la Richmond
kupewa tenda ya kufua umeme wa dharura ingawa Tathmini ya Tenda
ilionesha kuwa kati ya makampuni 8 yaliyofikia hatua ya tathmini,
kampuni hiyo ilikosa vigezo na kupata marks 0. Kwamba alitumia uwaziri
mkuu kuhakikisha wanapata tenda hiyo iliyoitia hasara kubwa serikali.
Aidha, Dk. Slaa amesisitiza kuwa kamati Mwakyembe ilitoa ripoti ya
kweli na kwamba yapo baadhi ya mambo ambayo hawakuyaweka wazi na
vielelezo anavyo kwa kuwa vigogo 27 walihusika na wizi huo.
Amemtaka Lowassa kujitokeza hadharani na kutaja kwa majina ya
viongozi wa ngazi za juu anaodai kuwa walishinikiza kusainiwa kwa
mkataba wa Richmond badala ya kuendelea kuwaficha.
“Ajitokeze asema kwa majina hao viongozi wa ngazi za juu zaidi ya
waziri mkuu ni nani na nani, aseme kwa majina kwa sababu waio juu ni
Rais na makamu wa rais, nani aliyeelekeza? Amtaje,” amesema Dk. Slaa.
Dk. Slaa alihitimisha kwa kutangaza rasmi kustaafu siasa za vyama na
kueleza kuwa ataendelea kushiriki katika harakati za kulikomboa taifa
bila kujihusisha na chama chochote cha siasa huku akimtaka Lowassa
kujitokeza hadharani kujibu alichokisema na kwamba akifanya hivyo
atamrudia tena na mengine ambayo hajayatoa hadharani.
No comments:
Post a Comment