Saturday, April 14, 2018

"Siku ya Israa na Miiraj ni Siku ya Kuienzi Amani iliyopotea Mashariki ya Kati na Palestina" Maulana Sheikh Jalala

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala, akiongea na Waandishi wa Habari katika tukio na Siku ya Israa na Miiraj ya Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w), Masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es salaam, Kulia kwake ni Naibu Mkuu wa Chuo cha Kiislam Hawzat Imam Swadiq (a.s) Sheikh Muhammad Abdu.

Bismillah Rahmani Rahimu
Ndugu zangu katika Imani
Asalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatu (Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu nyote)
Kumbukumbu ya tukio, Siku ya Israa na Miiraj ya Mtume Muhammad (s.a.w.w)
13.04.2018/1439, Masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es Salaam.
Kikao na Waandishi wa Habari.

Siku hii ya leo kwa kalenda ya Dini ya Kiislamu ni siku ambayo tunakumbuka tukio muhimu katika Uislamu nalo ni tukio la Israa na Miiraj, tukio hili maarufu ambalo limekuwa likienziwa na Waislamu hususan kwa kusoma historia nzima la tukio hili, Tukio hili la Israa na Miiraj ni tukio linaloelezea misafara miwili, Msafara wa Kwanza ni Msafara wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kutoka Makka Masjid Haraam (Masjid Mtakatifu wa Makka)  na kupelekwa moja kwa moja Masjid Al Aqswa ulioko katika ardhi ya Palestina, huu ndio ulikuwa msafara wa Kwanza. 

Msafara huu huwa tunauita  Msafara wa Israa, Mtume Muhammad (s.a.w.w) baada ya kufika Msikiti Mtakatifu ulioko Palestina au Msikiti Masjid Al Aqswa, Mtume Muhammad (s.a.w.w) akachukuliwa pale akapelekwa msafara mwingine, Msafara wa Mbinguni, Misafara hii miwili  tunaita Msafara wa Israa na Msafara wa Miiraj,Msafara huu ni Msafara Maarufu katika jamii ya Kiislamu na katika Ulimwengu wa Kiislamu na umekuwa ni Msafara ukisomwa na kuelezwa visa vyake kwa kirefu kitu gani kilitokea katika Msafara huo. Msafara huu Mwenyezi Mungu anauzungumza ndani ya Qur’an anaposema “Surat Al Israa: 1”


 Aya hii inauzungumzia Msafara huu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), ulioanza Makka na kufikia Palestina na kutokea Palestina kwanda katika Mbingu za juu. Msafara huu ambao Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliufanya kutoka Makka kwenda Palestina itambulike ya kwamba Masjid Al Aqswa ilioko Palestina ndio Qibla cha Kwanza cha Waislamu, yaani Waislamu Duniani kipindi hicho walipokuwa wanataka Kuswali, wanapotaka kusoma Dua, wanapotaka kufanya aina yoyote ya Maombi wanaelekea katika Msikiti Mtakatifu ulioko Palestina, itambulike vilevile msafara wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ulipotoka Makka ukafikizia Palestina, Mnyama ambae ndio Mtume Muhammd (s.a.w.w) aliokuwa akisafiria ambae aliitwa Buraaq, Mtume alimfunga Mnyama huyo pale nadni ya Msikiti wa Palestina (Masjid Al Aqswa).

Lakini sio hivyo tu Pale Masjid Al Aqswa, Mwenyezimungu aliwafufua Mitume wote (a.s) aliowatuma na wakaswali wote pale swala ya Jamaa,aliyoiongoza swala ile alikuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) na baada ya hapo msafara uliaanza kutokea pale, kwahivyo siku hii ya leo ya siku ya kukumbuka msafara wa Israa na Miiraj tunaamini ya kwamba ni msafara mkubwa na ni msafara muhimu. Lakini Mwenyezimungu anaisemea ardhi ya Palestina, kwamba ni ardhi iliyobarikiwa, Mungu anaisemea ardhi ya Mashariki ya kati, ardhi ile ni ardhi yenye Baraka, nini maana ya maneno haya? Maana ya maneno haya kwanza, Ardhi ya Palestina na ardhi iliyoko kandokando ya Palestina hii ni ardhi iliyobarikiwa, kwanza ni ardhi ya Mitume (a.s). 

Mitume wengi au Mitume wote waliotumwa na Mungu wengi wao wameishi katika ardhi hii ya Mashariki ya Kati, lakini sio hivyo tu, Mtume kama vile Ibrahimu (a.s) ambae ndie baba wa Waislamu, ndie Baba wa Wakristo, ndie baba wa Wayahudi amezikwa katika ardhi ya Palestina, si hapo tu ardhi hii kuonyesha ardhi yenye Baraka, Mitume (a.s) wakubwa kama Vile Ibrahimu (a.s), Ishaq (a.s) Yaquob / Yakobo (a.s) pamoja na kizazi cha Banii Israiel hawa waliishi katika ardhi ya Kan’aan kwenye nchi ya Palestina. Kwahivyo ni ardhi yenye Baraka, ni ardhi ya Mitume.Lakini vilevile ardhi hii ya Mashariki ya Kati, Mungu ameipa Utajiri asili ambao unapotetereka utajiri wa pale Dunia inatetereka.


Hii nataka kuweka kitu kimoja muhimu katika tukio hili muhimu la leo la Israa na Miiraj, Kwamba Mitume wote waliotumwa na Mungu, walitumwa na Ujumbe mmoja muhimu, nayo ni Ujumbe wa kueneza Amani, kueneza mshikamano, na kueneza kuvumiliana.Nabii Ibrahimu (a.s) ambae ndie aliemzaa Nabii Ishaka (a.s), Nabii Ishaka ndie aliemzaa Nabii Yaquob / Yakobo (a.s) ambae ni Israel, kwa upande mwingine yupo huku Nabii Ismail (a.s) ambae ndie kizazi cha Mtume Muhmmad (s.a.w.w), unapata yakwamba Ibrahimu (a.s) alietokea katika ardhi ya Palestina ambae ndie baba wa dini tatu kubwa Uislamu, Ukristo na Uyahudi.

Nabii Ibrahimu (a.s) huyu alikuja kufunza na kuelekeza maelewano, Vitabu vya Mungu, ambavyo vimeshuka katikaardhi ya Palestina na katika eneo la Mashariki ya Kati ambavyo ni Taurati iliyomshukia Mtume wa Mungu Nabii Mussa / Mosses (a.s), Zaburi iliyomshukia Nabii Daud (a.s), Injiri iliyomshukia Nabii Issa / Yesu (a.s) na Qur’an / Furqan iliyomshukia Mtume Muhammad (s.a.w.w), Vitabu hivi vine vya Mungu, vyote vimekuja kuhimiza amani, vimekuja kuhimiza Maelewano na Mshikamano.

Kwahivyo katika siku hii ya leo siku ya Israa na Siku ya Miiraj ni siku ya kuienzi Amani iliyopotea Mashariki ya Kati iliyopotea Palestina, siku hii ya leo siku ya Israa na Miiraj ni siku ya mshikamano kwa dini zote, Uislam, Ukristo na Uyahudi, dini hizi kubwa zilizoko Mashariki ya Kati na Duniani. Siku hii ya Israa na Miiraj kwanini tutaikumbuka, tunaikumbuka kwasababu Utulivu, Amani, kukaa Vizuri, kukaa pamoja kumetoweka katika ardhi ya Palestina na Mashariki ya kati ardhi iliyobarikiwa ambayo mitume wote walioshuka pale wamekuja kuenzi amani, vitabu vyote vilivyoshuka pale vimekuja kuleta utulivu.

Kwahivyo utulivu wa Mashariki ya Kati, utulivu wa Palestina naamini ndio utulivu wa Dunia, ndio amani ya Dunia,ndio amani ya Tanzania.Tanzania tumekuwa kisiwa cha amani, tumekuwa ni mahala Wakristo, Waislamu, Wayahudi na Wapagani tunakaa vizuri, hayo ndio mafundisho ya Nabii Ibrahimu (a.s) ambae anatokea Palestina, haya ndio mafundisho ya Israel Yakub (a.s) ambae ameishi katika ardhi ya Palestina, haya ndio mafundisho ya Mitume wote walioishi katika ardhi ya Mashariki ya Kati na Palestina.


Kwahivyo tunaviomba vyombo vya Usalama, uwe ni Umoja wa Mataifa, uwe ni Umoja wa nchi za Ulaya, ilitilie Umuhimu jambo la Amani, maelewano, mapatano na Mshikamano katika ardhi ya Palestina na Mashariki ya Kati, kwasababu ardhi ile ya Palestina na Mashariki ya Kati itakapopata Amani, Maelewano, Mapatano na Mshikamano ndio itapatikana Amani ya Dunia na sehemu zote.

Mwisho nakuomba Mwenyezi Mungu katika siku hii ya Israa na Miiraj uifanye na uiendeleze Tanzania izidi kuwa kisiwa cha amani,Watanzania wazidi kuwa ni watu wanaopendana, wazidi kuwa watanzania ni watu wanaoshikamana, wahajui kubaguana, kilugha zao, kikabila zao, Mwenyezi Mungu wanaotuongoza katika nchi hii uwape hekima,uwazidishe hekima, uwazidishe Busara na utulivu waweze kuiongoza Tanzania ya Upendo na Mshikamano na Tanzania ya watu wa kushikiana na kuvumiliana pamoja na madhehebu zao na dini zao tofauti.

 Hongereni sana Waislamu wote Duniani na wasiokuwa Waislamu hususani Watanzania kwa siku hii kubwa siku ya Israa na Miiraj
Asanteni sana,na Mungu awabariki.

Maulana Sheikh Hemed Jalala
Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania.

No comments: