Saturday, April 25, 2015

Mawlana Sheikh Jalala: Rajab Ni Mwezi Wa Mwenyezi Mungu

Maulana Sheikh Hemed Jalala akihutubia waumini wa Kiislam, Msikitini Ghadir,Kigogo-Post.






Katika khutba ya Ijumaa iliyotolewa na Maulana Sheikh Hemedi Jalala,  katika Msikiti wa Ghadiir –Kigogo Dar es slaam, Maulana aliwataka waislamu kuheshimu Mwezi huu wa Rajabu kwa kuwa ni mwezi katika Miezi mitukufu katika uislaam, akinukuu hadithi ya mtume (s.a.w.w) alisema “hakika Rajabu ni mwezi wa Mwenyezi Mungu, haukaribii Mwezi wowote kwa utukufu na heshima, kupigana na makafiri ni haraam”.

Aliendelea kusema kuwa Kabla ya Uislaam, makafiri walikua wakiuheshimu kwa kusimamisha vita, na Uislaam kwa kuwa ni dini ya amani ulikuja kuenzi Mwezi huu na mingineyo, Maulana alisikitika kwa kuwaona baadhi ya waislaam wanapigana, na kumwaga damu ya Waislaam wasio na hatia ndani ya mwezi huu, ambapo uislaam umeharamisha vita na uadui katika mwezi huu. Hao wanaobeba bendera ya uislaam, wanapigana ndani ya mwezi wa Rajabu na kuuana, wakati ni haraam .

Akielezea faida za mwezi huu, Maulana alisema: “yeyote atakaefunga siku moja Mtume (s.a.w.w) anasema mtu huyo anastahili radhi za Mwenyezi Mungu, atawekwa mbali na ghadhabu za Mwenyezi Mungu, mlango mmoja katika milango ya motoni utafungwa, na atakaa mbali na moto kwa masafa ya mwaka mmoja”.

Akitaja matukio ya kihistoria ya kiislaam, yaliyotokea katika mwezi huu alisema ”ndugu zangu waislamu Mwezi huu ni mtukufu na fadhila zake ni nyingi mno na una matukio mazito, miongoni mwa matukio hayo ni:
  1. Mwezi Mosi Rajab ilikua ni siku ya mazazi ya Imam wa Tano (5) Muhammad Baqir (as)
  2. Mwezi Tatu Shahada ya Imam wa Kumi  Ali Naqi (as)
  3. Mwezi 13, ni mazazi ya kiongozi wa waumini, imam Alii bin Abii Twalib (as) ambae alizaliwa ndani ya alkaaba tukufu, alizaliwa siku tukufu, tarehe tukufu, mwezi mtukufu na mahala patukufu.
  4. Mwezi 15, shahada ya bi Zainab (as) bint Alii (as) samba wa karbalaa.
  5. Mwezi 25 Pia kuna shahada ya imam musa kadhim (as) na vita ya khaybar
  6. Mwezi 26 ni shahada (kifo ) cha mzee Abii Twalib, baba na mlezi wa mtume Muhammad (s.a.w.w.)
  7. mwezi 27, ni tukio la kihistoria la Israa na Miiraj (safari ya mtume s.a.w.w) kwenda Jerusalem na kisha kwenda mbingu saba, na ni siku aliyopewa utume, mtume Muhammad (s.a.w.w).
    Waumini wa Dini ya Kiislam wakiwa makini katika kusikiliza Hotuba ya Maulana Sheikh Hemed Jalala.

  8. Pia maulana aliwafahamisha baadhi ya dua na aamal za kufanywa katika mwezi huu na akawataka wanaouona mwezi huu ni kama wa kawaida, kuachana na dhana hizo, kwani Mwenyezi Mungu mwenyewe ameutukuza na kuwataka waislaam wauheshimu, vipi wanauona wa kawaida, “ watambue kuwa si Mwezi wa kawaida, bali ni Miongoni mwa miezi Mitukufu una mazuri, matukufu na fadhila nyingi sana kwa watakao uadhimisha.

No comments: