Kufuatia uamuzi wa Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu nafasi ya
uenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), watu mbalimbali wamekuwa na
mtazamo tofauti huku wengi wakitaka kujua hatua hiyo imepokelewa vipi na
viongozi wa Ukawa.
Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia ameelezea jinsi alivyopokea taarifa za hizo akiwa mwenyekiti mwenza wa Ukawa.
Akiongea katika mahojiano maalum na waandishi wa habari, Mbatia
amesema kuwa uamuzi huo ni wa kawaida kwa kuzingatia mfumo wa vyama
vingi nchini na kwamba Profesa ametumia uhuru wake kwa mujibu wa sheria.
Hii ni sehemu ya kauli ya James Mbatia:
“Ibrahim Lipumba kujiuzulu nafasi ya uenyekiti katika wa Chama
Cha Wananchi CUF ni jambo la kawaida, ni mambo ya kawaida kabisa! Kwa
sababu tangu mfumo mzima wa vyama vingi vya siasa ulipoanza hapa
Tanzania mwaka 1992 na vikaanza kuruhusiwa kufanya kazi kisheria, kwa
mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, ni kwamba kila chama cha siasa ni
chama shindani cha mwenzake.
“Profesa Lipumba amegombea urais mwaka 1995, 2000, 2005, ni
kiongozi anaefahamika Tanzania hapa na katika siasa za vyama vingi na
mchango wake mkubwa kwa taifa. Lakini hatua aliyofikia…amefikia hatua
yake yeye binafsi ndani ya chama chake cha CUF. Lakini tujue kwamba kuna
haki ya kuchagua na kuchaguliwa. Kauli yake aliyoitoa leo ni kwamba
ataendelea kuwa mwanachama wa CUF lakini amepumzika kwenye uongozi ili
apatikane mwanachama mwingine aweze kukiongoza chama hicho.
“Hivi vyama vya siasa ni Taasisi, binadamu sisi tupo tunapita tu
na muda wetu ukifika tunafariki, lakini Taasisi zinabaki. Mwalimu
Nyerere ndiye muasisi wa TANU na CCM, mwalimu hayupo lakini CCM bado
ipo. Kwa hiyo hii ni changamoto tu ya kisiasa inayotokea na hapa kwetu
Tanzania mtu kutoka chama kimoja kwenda chama kingine imezoeleka”
No comments:
Post a Comment