Sheikh Mkuu wa al Azhar nchini Misri amesema, kuwakufurisha
Waislamu wa madhehebu ya Shia kunakofanyika kupitia kanali za
televisheni za satalaiti ni kitendo kisichokubalika na jambo hilo
haliwezi kuhalalishwa au kutetewa kwa kutumia kitabu kitakatifu cha
Qur’ani, Suna na mafundisho ya dini.
Sheikh Ahmad al Tayyib amesema Waislamu wa madhehebu ya
Suni wanaswali nyuma ya maimamu wa madhehebu ya Shia na kuongeza kuwa:
Baina ya Shia na Suni hakuna hitilafu kubwa zinazoufanya upande mmoja
uukufurishe na kuutoa katika dini upande mwingine na kwamba
kinachoshuhidiwa kwa sasa na kutumiwa vibaya na kwa malengo ya kisiasa
baadhi ya hitilafu za kimitazamo.
Sheikh al Tayyib amesema wadhifa mkuu
wa al Azhar ya Misri ni kufanya jitihada za kuunganisha Umma wa Kiislamu
licha ya hitilafu za kimitazamo zilizopo katika ulimwengu wa Kiislamu.
Sheikh Mkuu wa al Azhar amesema yuko tayari kusafiri na kwenda eneo
lolote lile duniani kwa ajili ya kuimarisha umoja wa Waislamu.
Kwa kutilia maanani hali ya sasa ya nchi za Waislamu,
inaonekana kuwa umoja wa Waislamu ndiyo wenzo muhimu zaidi ya
kuwawezesha kuvuka salama fitina na njama za ubeberu na maadui wa dini
hiyo ya Mwenyezi Mungu. Wakitumia mbinu mbalimbali, maadui hao wa
Uislamu wamelifanya suala la kuanzisha vita na mapigano kati ya Waislamu
wa madhehebu za Shia na Suni kuwa ndiyo ajenda yao kuu kama njia ya
kugawa na kuzusha hitilafu katika Umma. Nyenzo zinazotumiwa na maadui
hao kwa ajili ya kupenya baina ya Waislamu ni kutumia wasaliti
waliopotoka kutoka madhehebu mbalimbali za Waislamu na kisha kuhubiri
tafsiri zisizo sahihi za kisiasa.
Kufasiri na kuhubiri Uislamu wa Kimarekani ni njama ambayo
lengo lake ni kuzusha mpasuko na hitilafu katika safu za Waislamu na
kuzuia ulimwengu wa Kiislamu kuwa nguvu kubwa katika siasa za kimataifa.
Maadui wa Umma wa Kiislamu wanadhamini maslahi yao haramu kwa kuzusha
na kukuza hitilafu ndogondogo baina ya Shia na Suni. Kwa njia hiyo
maadui wa Umma wanawashughulisha Waislamu na masuala yasiyokuwa na
umuhimu na kuwaghafilisha na mauala ya asili ya muhimu sana hususan
kadhia ya Quds tukufu. Maadui hao wanaupambanisha Uislamu halisi na
sahihi unaosisitiza umoja na mshikamano na ule wa fikra mgando
unaowakilisha ujahili na ukatili. Mfano wa uislamu mgando ni ule wa
makundi ya kigaidi ya Daesh, al Qaida na Boko Haram ambayo yote
yanaungwa mkono kwa njia moja au nyingine na Marekani na utawala wa
Kizayuni wa Israel.
Kama anavyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
Ayatullah Ali Khamenei, katika maktaba na mfumo wa kifikra wa Imam
Khomeini, Uislamu wa mashekhe vibaraka wa watawala, Uislamu wa Daesh,
Uislamu usijali na unaokaa kimya mbele ya jinai zinazofanywa na Marekani
na Israel na kunyoosha mkono wa udugu na urafiki kwa madola ya kibeberu
unatokana na chanzo kimoja na hauwezi kukubalika.
Kwa msingi huo Waislamu wanapaswa kuwa macho na wasiruhusu maadui kutumia vibaya hitilafu zao za kimaoni na kimitazamo.
No comments:
Post a Comment