Wananchi katika jimbo la Karatu wamekosoa uamuzi wa aliyekuwa mbunge wa
jimbo hilo, Dk Slaa kumshambulia mgombea urais kwa tiketi ya Chadema Edward
Lowassa.
Wakazi hao wa Karatu wamemkataa Dk Slaa kwa kudai kuwa uamuzi aliouchukua
hausaidii katika harakati za kuikondoa CCM madarakani bali inazirudisha nyuma
juhudi hizo.
Kwa mujibu wa The Citizen, wananchi waliofanya mahojiano kwa nyakati tofauti
wameeleza kuwa hawatabadili msimamo wa kuiunga mkono ngome ya Ukawa kama
alivyotaka Dk Slaa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 15
tangu mwaka 1995.
“Ni bora tuwe na mafisadi wachache walioko upinzani kuliko kuwa na mafisadi
zaidi ya 100 ambao bado CCM inawakumbatia,” alisema Isack Philip, mkazi wa kata
ya Rhotia, Karatu.
Wananchi wengine walifika mbali kwa kuonesha jinsi wasivyounga mkono CCM
wakidai wako tayari hata kuchagua jiwe badala ya chama hicho tawala.
“Tuko radhi kuchagua jiwe badala ya CCM ambayo tangu tupate uhuru imekuwa
ikituangusha katika kupata maendeleo,” alisema muendesha bodaboda
aliyejitambulisha kwa jina la Emanuel Bayo na kuongeza kuwa madai ya Dk Slaa
hayana mashiko wakati huu.
Wananchi wengi waliofikiwa na gazeti hilo walieleza kuwa nia yao ni
kuhakikisha wanaona CCM ikiondolewa madarakani na sio vinginevyo.
Hata hivyo, mwenyekiti wa zamani wa CCM katika wilaya hiyo, alimtetea Dk
Slaa na kueleza kuwa anatoa mawazo na mtazamo wake kwa lengo la kuwaonesha
watanzania hali halisi.
Hivi karibuni, Dk Slaa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema alijitokeza
hadharani na kupinga uamuzi wa chadema kumpokea Edward Lowassa na kumpa nafasi
ya kugombea urais licha ya kukiri kuwa yeye ndiye aliyelipeleka wazo hilo kwa
uongozi wa chama chake ambacho kilikuwa kimemteua yeye kugombea nafasi hiyo. Chanzo, http://dar24.com/karatu-yamwaga-dk-slaa/
No comments:
Post a Comment