Tuesday, September 8, 2015

Zitto Kabwe "Ufafanuzi kuhusu Ulutheri na Uraisi"

Katika Ukurasa wake wa Facebook amesema kuwa, Kwanza; niombe radhi kwa wale ambao kwa njia moja au nyingine wamekwazika kwa maneno ambayo yametafsiriwa na baadhi ya watu kama 'udini' wakati naongea na waumini mjini Tabora siku ya Jumapili na kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Pili; niseme kwa uwazi kabisa mimi sio mdini hata kidogo. Mimi ni mcha Mungu na mojawapo ya mambo ambayo imani yangu imenifundisha ni upendo kwa kila mtu bila kujali dini yake.
Tatu; mimi kama mgombea ni jukumu langu kuomba kura kwa kila mtanzania bila kujali dini yake. Hili ni jambo ambalo mimi binafsi naliamini kwa dhati kabisa pamoja na chama changu.
Nne; naomba nifafanue kidogo tu nikichokisema na kumaanisha wakati wa Ibada. Lengo langu kuu lilikuwa ni kuomba waumini wenzangu waniombee kwa sala zao katika safari yetu ya kuikomboa Tanzania. Sikuwaambia wanichague au wanipigie kura kwa sababu mimi ni Mlutheri. Hapana.
Nilichowaomba na wote mmesikia ni sala zao. Sijawaambia wamchague Mlutheri mwenzao. Ni kweli kwamba hakuna Mlutheri ambaye amewahi kuwa Raisi. Sidhani kama nimesema uongo. Lakini nisisitize kwamba Ulutheri sio kigezo cha kuwa Raisi. Dini sio kigezo. Maombi yangu kwao waumini wenzangu ni sala zao na hili jambo yeyote mwenye imani anaruhusiwa kulifanya.
Nimalizie kwa kuwaomba radhi tena wale ambao wamekwazika na kauli yangu. Najua baadhi ya watu ambao wanapinga harakati zetu watajitahidi sana kuchochea na kulikuza jambo hili. Sababu zao tunazijua. Naomba muwapuuze tusonge mbele. Watanzania watachagua sio kwa sababu ya dini, kabila, ukanda au jinsia. Watachagua kwa kuangalia uwezo wa mtu na utekelezaji wa ahadi kutokana na mipango ambayo tumeiweka.
Nawashukuru sana.

No comments: