Monday, September 21, 2015

Shule zafungwa Kenya kutokana na mgomo wa Walimu

Wanafunzi wengi Kenya wamelazimika kusalia nyumbani baada ya serikali kuagiza kufungwa kwa shule zote za umma na za kibinafsi leo kutokana na mgomo wa walimu.
Ingawa shule za umma zimefungwa, baadhi ya shule za kibinafsi zimekaidi agizo la serikali na kuendelea na masomo.
Chama cha shule za kibinafsi kimesema kitawasilisha kesi mahakamani leo kupinga agizo hilo la serikali lililotolewa na Waziri wa Elimu Jacob Kaimenyi Ijumaa wiki iliyopita.
Wazazi wanaowapeleka watoto wao katika shule za kibinafsi, nyingi ambazo hutoza karo ya juu, wametoa hisia kali kutokana na tangazo hilo wakishangaa ni kwa nini shule hizo zinafungwa.
Katika shule za umma, ni watahiniwa wanaojiandaa kufanya mitihani ya kitaifa waliosalia shuleni.
Kwa mujibu wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) kuna watahiniwa 937,467 wanaojiandaa kufanya mtihani wa darasa la nane KCPE utakaoanza Novemba 10 na kumalizika Novemba 12.
Watahiniwa wanaojiandaa kufanya mtihani wa kidato cha nne KCSE utakaoanza rasmi Oktoba 12 ni 525,802.
Baraza hilo limesema mitihani hiyo haitaahirishwa.
Kwenye hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga, Rais Uhuru Kenyatta na baadaye kutumwa kwa vyombo vya habari alisema haiwezekani kwa walimu kuongezewa mishahara na kuwataka warejee kazini.
Mahakama ya Juu Kenya iliitaka serikali kutii agizo la mahakama ya rufaa iliyoitaka serikali kutii uamuzi wa mahakama ya kiviwanda na kuwalipa walimu nyongeza ya asilimia 50 hadi 60.
Serikali kupitia Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) imepinga agizo hilo.
Mahakama ya Viwanda inatarajiwa kutoa uamuzi Ijumaa wiki hii kuhusu iwapo mgomo huo wa walimu, uliotatiza masomo Kenya tangu zifunguliwe kwa muhula wa tatu, ni halali au la. chanzo bbc-swahili

No comments: