Uchaguzi wa mabaraza ya miji unafanyika leo nchini Saudi Arabia
huku wanawake wa nchi hiyo wakishiriki katika uchaguzi kwa mara ya
kwanza kabisa katika historia ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Wanawake wa nchi hiyo leo wameelekea katika masanduku ya kupigia kura
kuwachagua wawakilishi wao wa mabaraza ya miji kwa mara ya kwanza
kabisa baada ya kupata haki ya kupiga kura na pia kusimama kugombea
nafasi za mabaraza ya miji.
Katika uchaguzi wa leo ambao ni wa aina yake kwa wanawake wa Saudi
Arabia, zaidi ya wagombea elfu tano wanaume na wagombea 980 wanawake
wanachuana kuwania viti vya mabaraza ya miji.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, wanawake laki moja na thelathini elfu
walijiandikisha kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi wa leo huku
wanaume milioni moja na laki tatu na nusu wakiwa nao wamejiandikisha
kama wapiga kura.
Mabaraza ya Miji ndio bodi pekee ya serikali ambayo wananchi wa
Saudia wanaruhusiwa kuchagua wawakilishi wao huku nyadhifa nyingine
muhimu serikalini zikiwa ni za kurithishana baina ya ukoo wa Aal Saud na
wananchi hawana nafasi yoyote katika uteuzi huo.
Licha ya wanawake wa Saudia kuruhusiwa kuwa wagombea na wapiga kura,
wachambuzi wa mambo wanasema kwamba, wana nafasi ndogo mno ya kushinda
na kuwa wawakilishi wa mabaraza ya miji.
Wanawake wa Saudi Arabia wanaruhusiwa kupiga kura katika mabaraza ya miji ilihali hadi leo bado hawajaruhusiwa kuendesha gari.
No comments:
Post a Comment