Saturday, April 9, 2016

Waislam Hongereni kwa Kuzaliwa Imam Baqir (a.s) Khalifa wa Mtume Muhammad (s.a.w.w)

Jina : Muhammad
Kuniya : Abu Ja’afar
Lakabu yake : Al-Baqir
Baba yake : Ali Ibn Hussein
Mama yake : Fatimah Bint Hassan
Kuzaliwa kwake : 1 Rajab, Mwaka wa 57, Madina
Nasaba ya Imam Muhammad Ibn Ali (a.s) ni ya kipekee sana, kwa sababu yeye ndie Imam pekee amabe ameunganishwa  na Fatima Zahra(a.s) Bint Muhammad (s.a.w.w) kupitia kwa Baba na Vile vile kwa Mama, Baba yake ni Mtoto wa Imam Hussein Ibn Ali (a.s) na Mama yake ni Mtoto wa Imam Hassan Ibn Ali (a.s). Kwa sababu hiyo alikuwa akijulikana mtoto wa Wema wawili pia akijulikana “Al-Baqir” mchunga (wa Elimu ya Mtume).

Mwaka wa 57 baada ya hijra ya Mtume (s.a.w.w) kuelekea Madina, katika siku ya kwanza ya mwezi uliojaa fadhila wa Rajab, ulimwengu ulipambazuka kwa kuzaliwa nuru. Katika siku hii yenye baraka, mtoto kutoka Nyumba ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) alizaliwa na kama walivyokuwa Ahlul Bayt wengine wa Mtume (s.a.w.w), akawa tawi katika matawi maridadi katika historia ya Uislamu.

Uimamu wa Imam Mohammad Baqir (a.s) ulianza katika kipindi ambacho, ummah wa Kiislamu ulikuwa unakabiliwa na changamoto kubwa za kiitikadi na kifiqhi baina ya makundi mbali mbali ya Kiislamu. Kuwepo Imam Baqir (a.s) katika medani kulipelekea kuchukuliwa hatua muafaka katika kubainisha mitazamo ya Ahlul Bayt wa Mtume (s.a.w.w).

Katika kipindi cha Imam Baqir (a.s), hujuma ya kiutamaduni iliyokuwa imeratibiwa kwa mpangilio maalumu na Bani Umayyah ililenga kuvuruga itikadi za kidini za ummah wa Kiislamu. Aidha katika kipindi hicho, jamii ya Kiislamu ilishuhudia kuibuka nadharia zisizo sahihi za kifalsafa kuhusu misingi ya itikadi.
Licha ya shughuli nyingi za kielimu na kiutamaduni alizokuwa nazo, Imam Baqir (a.s), hakughafilika na masuala ya kisiasa na alikuwa akiwakosoa sana watawala wa kiimla na madhalimu wa zama zake. Katika harakati zake za kuwazindua Waislamu kisiasa, Imam alibainisha sifa za viongozi wema ili kuwafanya watu waweze kuwatia kwenye mizani watawala na kufahamu udhaifu na upotofu wao.
Sheikh Tousi, mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu amewataja wanafunzi bingwa wa Imam Baqir (a.s) kuwa ni watu 462. Vigogo na shakhsia wakubwa wa kielimu wa zama hizo wote walifika mbele ya Imam Baqir (a.s) ili kupata angalau tone moja la bahari yake pana ya elimu. Watu kama vile Jabir bin Yazid Ju'fi, Zuhri , Abu Hanifa, Anas bin Malik na Shafi ni kati ya wanazuoni walionufaika na hazina kubwa ya kielimu ya Imam Baqir AS. Muhammad Ibn Talha Shafi'i katika kuelezea sifa za Imam Baqir anaandika: “Alikuwa mwenye kuchana na kunawirisha elimu.
Imam Baqir anasema: “Uongozi wa jamii unamustahiki mtu mwenye sifa tatu. Kwanza ni ucha Mungu ili takwa iweze kumkinga na mitihani na madhara ya madaraka kama vile kutumbukia katika mtego wa ufisadi. Pili awe mstahimilifu ili aweza kuzuia hasira zake. Tatu aamiliane na watu anaowatawala kama baba mkarimu na awe na tabia nzuri”.
Imam anasema katika sehemu nyingine: "Hakuna mja yoyote muumini asiye na nukta nyeupe na yenye nuru kwenye moyo wake. Kila mara anapofanya dhambi nukta nyeusi hudhihiri kwenye nukta hiyo nyeupe. Kwa hivyo iwapo atatubu baada ya kufanya dhambi nukta hiyo nyeusi hutoweka, la sivyo akidumu kwenye maasi nukta nyusi huongezeka na kuenea hadi kufunika kabisa nukta hiyo nyeupe. Baada ya kufunikwa kabisa nukta hiyo nyeupe mtu aliye na moyo kama huo kamwe hatawezi kuona uso wa saada."
Wapenzi wasomaji kwa mara nyingine ninatoa mkono wa pongezi, kheri na fanaka kwa mnasaba wa kuzaliwa Imam Baqir (a.s), Imam wa Tano katika Maimam aliowataja Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuwa Makhalifa baada yake, wakwanza akiwa ni Imam Ali Ibn Abu Taalib (a.s), Wapili ni Imam Hassan Ibn Ali (a.s), watatu ni Imam Hussein Ibn Ali (a.s), wa nne ni Imam Ali Ibn Husein -Sajjad (a.s) na Wa tano ni Imam Muhammad Ibn Ali al Baqir (a.s).
Imetolewa na
Twalha Zuberi Ndiholeye
Kiongozi Mkuu wa Baqir Media
Tarehe 09/04/2016, Sawa na 2, Rajab, 1437

No comments: