Huku shughuli za kumzika Mkuu wa Halmashauri
ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu hapa nchini, Ayatullah Akbar
Hashemi Rafsanjani, shakhsia na viongozi mbali mbali wameendelea kutoa
salamu zao za rambirambi kufuatia kifo cha mwanachuoni huyo.
Miongoni mwa shakhsia waliotuma salamu zao za rambirambi kwa
familia, jamaa, na marafiki wa marehemu Rafsanjani pamoja na serikali na
taifa la Iran kwa ujumla ni Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast na
mwenzake wa Cuba, Raúl Castro.
Wengine wa hivi punde kutuma salamu zao za pole ni Rais Bashar
al-Assad wa Syria, Karen Karapetyan, Waziri MKuu wa Armenia,
Mfalme Abdullah II wa Jordan na Rais wa eneo la Kurdistan nchini
Iraq Masoud Barzani.
Katika ujumbe wake uliotumwa kwa Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran, Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria amesema, taifa na
serikali ya Algeria inatoa mkono wa pole kwa taifa na serikali ya Iran
kutokana na kifo cha Ayatullah Rafsanjani.
Awali pia Rais Jacob Zuma wa
Afrika Kusini alituma salamu zake za rambirambi na kusema: "Afrika
Kusini inamshukuru Rais (Mstaafu) Rafsanjani kwa moyo wake wa kujitolea
kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kisiasa na nchi za Afrika ikiwemo
Afrika Kusini hususan wakati alipokuwa Rais wa Iran"
Hali kadhalika Josh Earnest, Katibu wa Masuala ya Vyombo vya Habari
ya Ikulu ya Marekani White House ametuma rambirambi zake akimtaja
Rafsanjani kama shakhsia wa aina yake katika historia ya Iran.
Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani alifariki dunia juzi usiku akiwa na umri wa miaka 82, baada ya kukumbwa na mshtuko wa moyo.
No comments:
Post a Comment