Friday, June 7, 2019

Watanzania watakiwa kuwa Wakweli na Watii baada ya Mwezi wa Ramadhani | Maulana Sheikh Jalala

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akiongea na Waandishi wa Habari punde tu baada ya Swala ya Eid al Fitir, katika Viwanja vya Pipo Kigogo Dar es salaam.

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala amewataka Watanzania kuwa wakweli, watii, wasikivu, wapenda amani na wenye kupendana na kuelewana ikiwa ni mwendelezo wa athari iliyopatiana katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Baada ya kumalizika Mwezi wa Ramadhani tuwe Watanzania Wakweli, tuwe watanzania wenye Utii, tuwe ni watanzania wenye usikivu, tuwe ni watanzania wenye kupendana, tuwe ni watanzania wenye kuelewana, hayo yote ni maelekezo yaliyoko ndani ya Qur’an”

Maulana Sheikh Jalala amesema hayo wakati akiuongea na waandishi wa Habari katika kutoa Salamu za kheri na fanaka baada ya Swala ya Eid al Fitiri, iliyoswaliwa katika Viwanja vya Pipo Kigogo jijini Dar es salaam.

Aidha Maulana Sheikh Jalala amesema kuwa Tumeona ndani ya ardhi yetu ya Tanzania ndugu zetu wakristo wakiandaa futari wakiwaalika waislamu, wakikaa meza moja wachungaji, Maaskofu na Masheikh pamoja na Waislamu wengine hii ni dalili nzuri yakuonyesha upendo na Mshikamano. Kama tulikuwa tunakaa waislamu na wakristu tukifuturu pamoja katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, haya ni malezi yanatakikiana yaendelee baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani”

Mjumbe wa Baraza la Ulamaa wa Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania (T.I.C) Sheikh Mulaba Swalehe akiongea na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam 
Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza la Ulamaa wa Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania (T.I.C) Sheikh Mulaba Swalehe amesema kuwa lengo la Mwezi wa Ramadhani ni watu kuwa Wachamungu utakaopelekea Binadamu kuishi kwa amani na Salama katika Ulimwengu.

“Leo tunamshukuru Mungu kwa kukamilisha mwezi wa Ramadhani ambao ulikuwa ni mwezi lengo lake kubwa ni  kufikia Uchamungu, ni wajibu wa kila mmoja kuweza kumsaidia ndugu yake na kumpenda ndugu yake, kwani kwa hali hii ili tuweze kuishi kwa amani na salama katika dunia hii.
Mwisho Maulana Sheikh Jalala amesema kuwa anamuomba Mwenzimungu (swt) upendo tuliokuwanao katika Mwezi wa Ramadhani, Mahusiano mazuri tuliokuwanayo katika mwezi wa Ramadhani kama watanzania, mahusiano haya yazidi kuboreka, yazidi kuendelea, utulivu na amani tuliouonyesha ndani ya Mwezi wa Ramadhani amani hii na utulivu huu namuomba mwenyezi mungu uendelee katika ardhi ya Tanzania katika masiku mengine, Eid njema.
Waumini wa Dini ya Kiislamu wakijumuika pamoja na Waislamu wengine duniani katika kushiriki Swala ya Eid al Fitir, katika Viwanja vya Pipo Kigogo Dar es salaam. 

Waumini wa Dini ya Kiislamu wakiomba dua katika swala ya Eid al Fitir, iliyoswaliwa katika Viwanja vya Pipo jijini Dar es salaam


No comments: