Kundi la wanazuoni wa Kiislamu wa madhehebua ya
Shia nchini Bahrain limesema tuhuma dhidi ya msomi mwenzao Ayatullah
Sheikh Isa Qassim hazina msingi na kwa mantiki hiyo, kesi inayotazamiwa
kuanza hii leo dhidi ya mwanachuoni huyo ni bandia.
Taarifa ya wasomi hao wa Kiislamu nchini Bahrain imesema kuwa,
mashitaka anayolimbikiziwa msomi huyo mashuhuri ambaye utawala wa Manana
umemvua uraia ni ya kubuni na wala hayana mashiko na kwamba kesi dhidi
yake inakiuka katiba, haki za binadamu zilizoanishwa katika sheria za
nchi hiyo na hata za kimataifa.
Wanazuoni hao wa Bahrain wamesema kesi
dhidi ya Ayatullah Qassim ni sawa na kesi dhidi ya Waislamu wote wa
madhehebu ya Shia duniani.
Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha pamoja Madhehebu za Kiislamu,
Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, shirika la
kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch na Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran ni baadhi ya nchi na asasi za kimataifa zilizotoa taarifa ya
kulaani kupokonywa uraia Ayatullah Qassim, kwa madai kuwa ametumia
vibaya nafasi yake kwa maslahi ya madola ya kigeni.
Aidha hatua hiyo
imekabiliwa na wimbi la maandamano kutoka nchi mbali mbali kama vile
Iraq.Sheikh Qassim anatazamiwa kupandishwa kizimbani hii leo, ambapo utawala
wa Manama umemfungulia mashitaka matatu ya kupokea pesa kinyume cha
sheria, ufuaji wa pesa na eti kusaidia harakati za kigaidi.
No comments:
Post a Comment