Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema nchi za
Magharibi zimeshindwa kuvumilia uhuru wa kujitawala Syria na ndiposa
zikaanza kuunga mkono harakati za kigaidi nchini humo.
Rais Assad aliyasema hayo jana katika mazungumzo na ujumbe wa
wabunge kutoka Ugiriki mjini Damascus na kuongeza kuwa, kampeni za
muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani nchini humo eti wa
kukabiliana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh zimegonga mwamba
kwa kuwa lengo la kampeni hizo ni kuyumbisha uhuru wa Syria. Rais wa
Syria amenukuliwa na shirika la habari la SANA linalopeperusha matangazo
yake kwa lugha ya Kiarabu akisema kuwa:
"Tatizo la nchi za Magharibi ni
kukerwa na uhuru wa kujitawala taifa la Syria na ni kwa sababu hii
ndiposa zimekuwa zikiwasaza magaidi na kulenga maeneo ya raia katika
hujuma zake."Mapema mwezi huu, raia 120 waliuawa katika moja ya hujuma za muungano
huo wa kijeshi katika kijiji cha Tukhan al-Kubra mjini Manbij.
Syria ilitumbukizwa kwenye mgogoro mkubwa wa ndani mwezi Machi mwaka
2011 kufuatia magaidi wa kigeni kutoka kona mbalimbali za dunia
walipomiminwa nchini humo ili kufanya mauaji dhidi ya raia na maafisa wa
serikali halali iliyochaguliwa na wananchi ya Rais Bashar al-Assad.
Takwimu rasmi zinaonesha kuwa zaidi ya watu laki nne na elfu sabini
wameuawa nchini Syria na nusu ya watu milioni 23 wa nchi hiyo
wamelazimika kuwa wakimbizi.Chanzo:parstoday
No comments:
Post a Comment