Ujumbe maalumu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai
(ICC) unaelekea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) kwa
madhumuni ya kuchunguza jinai za kivita zilizofanywa na utawala wa
Kizayuni katika vita vya siku 50 dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Duru za habari zimeripoti kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel
unajiandaa kuupokea ujumbe huo ambao unatazamiwa kufanya uchunguzi
kuhusu tuhuma za jinai za kivita ambazo utawala huo haramu unatuhumiwa
kuzifanya wakati wa vita vya mwaka 2014 dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
Safari ya ujumbe huo wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ambayo
itafanyika hivi karibuni imetokana na ombi la Mwendesha Mashtaka Mkuu wa
mahakama hiyo Bi Fatou Bensouda na lengo lake ni kutoa fursa kwa
wajumbe wa jopo hilo la ICC kuwa na uelewa wa jinsi mfumo wa vyombo vya
mahakama vya utawala wa Kizayuni unavyofanya kazi.
Hapo kabla Mamlaka ya Ndani ya Palestina iliitaka Mahakama ya
Kimataifa ya Jinai ichukue hatua ya kuchunguza jinai za kivita
zilizofanywa na utawala wa Kizayuni, hatua ambayo iliwafadhaisha mno
viongozi wa utawala huo ghasibu.
Mbali na Mamlaka ya Ndani, shakhsia mbalimbali wa
Kipalestina wamekuwa wakitoa wito wa kuchunguzwa jinai za kivita
zilizofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa
Gaza.
Mustafa Barghuthi, Katibu wa Harakati ya Ubunifu wa Kitaifa ya
Palestina alisema hivi karibuni kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai
imekuwa ikisuasua katika kuchukua uamuzi wa kuanzisha uchunguzi kuhusu
vita vya Gaza.
Barghuthi alisisitiza kuwa kuna ulazima wa kufanyika
uchunguzi wa suala hilo na kuongeza kwamba haipasi kuiruhusu Israel
ijivue na mas-ulia na dhima ya jinai ilizotenda katika vita vya siku 50
dhidi ya Gaza.
Zaidi ya Wapalestina 2,300 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto
wadogo waliuawa shahidi na maelfu ya wengine walijeruhiwa katika
mashambulio ya siku 50 mtawalia yaliyofanywa na jeshi la utawala wa
Kizayuni mwaka 2014 dhidi ya Ukanda wa Gaza.
No comments:
Post a Comment