Monday, September 5, 2016

Waliohusika na maafa ya Mina wafikishwe mahakamani

Afisa wa ngazi za juu wa Iran amesema taasisi za haki za binadamu zinataka serikali ya Saudi Arabia iwajibike, ilipe fidia, na iwashtaki wale waliohusika na maafa ya Mina katika ibada ya Hija mwaka jana.

Sayyid Mohammad Ali Husseini, Mshauri wa Masuala ya Kimataifa wa Katibu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran ameashiria maafa ya kuogofya ya Mina na hatua ambazo zimechukuliwa na Iran ili kuhakikisha familia za waathirika wa maafa hayo wanapata haki zao na kusema:

 "Baada ya kupita mwaka mmoja tokea yajiri maafa ya kuogofya ya Mina ambapo maelfu ya Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu walipoteza maisha kidhalimu, serikali ya Saudia si tu kuwa haijawajibika hata kidogo kutokana na maafa hayo, bali pia imezuia na imeweka vikwazo na kuwazuia maelfu ya watu kutekeleza nguzo ya Kiislamu ya Hija mwaka huu."

Husseini ambaye aliwahi kuwa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, hata kama tutakubali kuwa serikali ya Saudia haikuwa imepanga kutekeleza kwa makusudi maafa ya Mina, lakini ilipaswa kukubali kuwajibika kutokana na usimamizi wake mbovu.
 
Sikukuu ya Eid al-Adha ya mwaka jana ilishuhudia maelfu ya mahujaji wa nyumba ya Mwenyezi Mungu wakiwemo mahujaji 464 wa Iran wakipoteza maisha yao katika ibada ya Hija wakati wa kutekeleza ibada ya kumpiga mawe shetani katika eneo la Mina.

 Maafa hayo yalisababishwa na usimamizi mbaya wa viongozi wa utawala wa Aal Saud. Baada ya kutokea maafa hayo ya kusikitisha, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliitaja serikali ya Saudia kwamba, ndio mhusika mkuu wa maafa hayo ya kutia uchungu na imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali za kisiasa na kisheria ili kuhakikisha familia zilizokumbwa na msiba huo kutokana na maafa ya Mina zinapatiwa haki zao.

No comments: