Gazeti la al-Watan la nchini Misri limeandika
kuwa, utawala wa Aal-Saud ndio mdhamini mkubwa wa fedha na silaha kwa
makundi ya kigaidi na Kiwahabi yanayofanya jinai na mauaji makubwa
katika nchi za Syria na Yemen.
Alkhamis ya jana gazeti hilo liliandika ripoti hiyo kwa mara ya
kwanza dhidi ya Saudi Arabia na kubainisha kwamba, utawala wa Saudi
Arabia ndio muungaji mkono mkubwa kwa magenge ya kigaidi.
Sambamba na kushadidi mgogoro katika uhusiano wa Misri na Saudia
kuhusiana na kadhia ya Syria, gazeti hilo la al-Watan limeandika kuwa,
kwa muda wote Saudia imekuwa ikiyasaidia kijeshi na kifedha kwa makundi
ya kigaidi likiwemo kundi la kigaidi na kitakfiri la Jab'hatu Nusra na
mengine mengi ya Kiwahabi huko Syria na Yemen. Kwa mujibu wa gazeti
hilo, Uturuki ni mhusika mkuu katika kuwasilisha misaada hiyo kutoka
Saudia kwa makundi hayo nchini Syria.
Limeenda mbali zaidi na kuandika kuwa, nchini Yemen baada ya Saudia
kuunda muungano wa kijeshi ilioupa jina la 'Kimbunga' iliunda pia
makundi ya kigaidi na kuyapa silaha na fedha kwa lengo la kupambana na
harakati ya wananchi ya Answarullah.
Mgogoro kati ya Misri na Saudia ulishtadi baada ya Misri kuupigia
kura ya ndio muswada wa Russia kuhusiana na kadhia ya Syria mbele ya
Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment