Hali ya kiuchumi nchini Saudia imezidi kuwa mbaya
kiasi kwamba nchi hiyo imelazimika kuomba mkopo kutoka kwa mashirika ya
kimataifa ya fedha.
Mtandao wa Intaneti wa The Wall
Street Journal wa nchini Marekani uliandika katika toleo lake la tarehe
10 mwezi huu wa Oktoba kwamba, ufalme wa Saudia umekuwa ukitegemea sana
pato lake kutokana na uuzaji mafuta ghafi nje ya nchi, lakini bei ya
bidhaa hiyo muhimu imeporomoka tangu katikati ya mwaka 2014 na kuifanya
Saudia ivunje rekodi katika nakisi ya bajeti yake, kwa kukumbwa na
nakisi ya dola bilioni 98 za Kimarekani kwenye bajeti yake ya mwaka
jana.
Pia liliandika: Mwaka jana Saudia ilipata mkopo wa dola bilioni 10
kutoka kwa mashirika ya fedha ya kimataifa.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa,
kutokana na vita vya Yemen na uungaji mkono wake kwa magenge ya kigaidi
kuigharimu fedha nyingi serikali ya Saudia sambamba na kuporomoka bei ya
mafuta katika soko la dunia, nchi hiyo ya kifalme imelazimika kuomba
mikopo katika mashirika ya kimataifa ya fedha ili kukabiliana na mgogoro
wa kiuchumi ilioikumba.
Duru nyingine za habari likiwemo shirika
la habari la IRNA nazo zimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, utawala
wa Aal Saud umeamua kuomba mkopo kutoka kwa Benki za HSBC na Citigroup
za Marekani na kuchapisha dhamana za madeni (Eurobond).
Kwa upande wake, Benki Kuu ya Saudia
imetoa mkopo wa dola bilioni nne wa masharti machache kwa benki za ndani
ya Saudia ili kuzuia kufilisika baadhi ya mashirika makubwa nchini
humo.
Takwimu zinaonesha kuwa, dhamana za madeni za Saudia kwa ajili ya
kukabiliana na matatiso ya kiuchumi ya nchi hiyo zinaweza kupindukia
dola bilioni 15 kiwango ambacho hakijawahi kufanyika nchini humo katika
historia ya miongo kadhaa ya nchi hiyo.
Nakisi ya bajeti, mgogoro wa matumizi ya
fedha taslimu, kuporomoka soko la hisa na kiujumla matatizo ya kifedha
katika mfumo wa kibenki wa Saudia katika kipindi cha miaka miwili
iliyopita, yote ni mambo yaliyoathiriwa na njama za utawala wa Saudia za
kupunguza thamani ya mafuta katika soko la dunia.
Saudia ilifanya njama
hizo kutoa pigo kwa baadhi ya nchi wapinzani wake kama vile Iran na
Russia, lakini madhara ya njama hizo zimeirejea mwenyewe hivi sasa.
No comments:
Post a Comment