Tuesday, February 21, 2017

Muungano wa Uturuki, Saudia na Israel katika propaganda chafu dhidi ya Iran

Muungano na misimamo ya aina moja dhidi ya Iran ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Waziri wa Vita wa utawala ghasibu wa Israel na mwenzao wa Uturuki katika Mkutano wa Usalama wa Munich si jambo jipya wala lililotokea kwa sadfa. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu matamshi yaliyotolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir na bwabwaja za Waziri wa Vita wa Israel kwa kusema kwamba, tawala hizo mbili zinadhani kuwa ili kuweza kufidia kufeli na kushindwa kwao mara kwa mara katika Mashariki ya Kati zinapaswa kuchochea anga ya kimataifa dhidi ya Iran. 

Bahram Qasemi ameongeza kuwa, lugha iliyotumiwa na mawaziri hao wawili pia ni ya kukaririwa na inayoakisi kufilisika na kukata tamaa kunakoambatana na machungu na maumivu.
bahram Qasemi
Katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Usalama wa Munich, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia amesema kuwa: Eneo la Mashariki ya Kati limejaa mivutano. Migogoro ya Syria, Iraq, Yemen na Libya inazidi kupambana moto, tunakabiliwa na ugaidi, uharamia na matatizo ya kiuchumi... Tunapaswa kufanya jitihada za kupatanisha kati ya Waarabu na Israel..", mwisho wa kunukuu.

Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia katika upande mmoja yanaakisi sehemu ya hali halisi ya Mashariki ya Kati. Hata hivyo kuna shaka kubwa kuhusu alichodai kuwa ni sababu za kujitokeza changamoto hizo. Katika matamshi yake hayo Adel al-Jubeir amefanya jitihada kubwa za kuituhumu Iran kuwa inaunga mkono ugaidi na kusema, Tehran inaingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. 

Matamshi hayo kwa hakika ni aina fulani ya kubadili na kugeuza ukweli na hali halisi ya mambo. Vilevile kunaonekana ushirikiano mkubwa na mfanano wa aina yake katika matamshi hayo na yale yaliyotolewa na maafisa wa serikali ya Israel katika Mkutano wa Usalama wa Munich.

Katika hotuba yake kwenye mkutano huo, Waziri wa Vita wa Israel, Avigdor Lieberman ameituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inavuruga amani na usalama wa eneo la magharibi mwa Asia na kudai kuwa: Iran ndiyo nchi inayoongoza katika kuunga mkono ugaidi duniani. 

Avigdor Lieberman amedai kuwa, maudhui ya Palestina si tatizo muhimu la eneo la magharibi mwa Asia kwa sasa. Matamshi kama haya haya pia yametolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlüt Çavuşoğlu katika mkutano wa Munich.
Avigdor Lieberman na Adel al Jubeir
Jumla ya misimamo hiyo kwa hakika ni mithili ya vipande vya fumbo na chemsha bongo ambayo picha yake ya mwisho ni kudhihirisha sura ya kutisha kuhusu Iran. Hata hivyo na licha ya mshabaha unaoshuhudiwa katika matamshi na misimamo hiyo ya Saudi Arabia, Israel na Uturuki lakini kila mmoja wao anafuatilia malengo yake makhsusi.

Marekani kwa upande wake inafuatilia malengo ya kuzusha hofu na wahka kwa nchi za Kiarabu ili kuweza kuuza silaha zaidi kwa nchi hizo na kuyaingizia faida kubwa makampuni ya kuuza silaha ya nchi hiyo.

Lengo kuu la utawala haramu wa Israel katika mchezo huo mchafu ni kufuta kabisa kadhia ya Palestina. Hivyo basi kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir aliyedai kuwa maudhui kuu ya eneo la Mashariki ya Kati kwa sasa ni kujenga suluhu na mapatano baina ya Waarabu na Israel, yanaonekana kuhudumia ipasavyo malengo ya utawala huo ghasibu unaoendelea kuukalia kwa mabavu Msikiti wa al Aqsa na kibla cha kwanza cha Waislamu.

Hapa bado haijajulikana vyema nafasi ya Uturuki katika kundi hili lenye pande tatu. Inaoneka kuwa, Uturuki imenasa katika nafasi kadhaa na kukosa msimamo thabiti na wa wazi. Katika upande mmoja, Ankara inataka kuwa na nafasi katika matukio ya Syria, siku moja inalisaidia na kulihami kundi la kigaidi la Daesh na kesho yake inafanya mashambulizi dhidi ya kundi hilo na kuwatia nguvuni raia wa Uturuki kwa madai ya kuunga mkono na kushirikiana na kundi hilo!

Katika hatua yake nyingine Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan amezitembelea nchi kadhaa za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi ambako ametangaza uungaji mkono wa nchi yake kwa nchi hizo na wakati huo huo Waziri wake wa Mambo ya Nje amehutubia Mkutano wa Usalama wa Minich na kuituhumu Iran kuwa inaunga mkono ugaidi na kuchochea mapigano ya kimadhehebu!  
Mevlüt Çavuşoğlu na Adel al Jubeir
Madai haya yametolewa wakati hakuna asiyejua kwamba, Uturuki na Saudi Arabia ni miongoni mwa vinara waliokuwa mstari wa mbele katika kuanzisha mgogoro wa sasa wa eneo la Mashariki ya Kati. 

Kwa mfano tu Uturuki imetuma kinyume cha sheria majeshi yake katika ardhi ya nchi za Iraq na Syria na kukiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi hizo. Nchi hiyo hiyo siku chache zilizopita ilitia saini taarifa ya pande tatu na Iran na Russia ambayo imesisitiza suala la kuheshimiwa ardhi ya Syria. 
Mtoto wa kiume wa Erdoğan, Bilal akiwa pamoja na vinara wa Daesh 
Alaa kulli hal, pande hizo tatu (Saudia, Israel na Uturuki) na washirika wao zinaelewa vyema kwamba, Iran haikubaliani na mchezo huo mchafu na wa kinafiki; kwa sababu hiyo zimeungana na kupiga ngoma za propaganda dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

 Hata hivyo walimwengu wamekomaa na wanaelewa vyema ni kina nani walioanzisha makundi ya kigaidi kama Daesh na Jabhatu Nusra, kuyapa silaha, kuyaruhusu kutumia ardhi na mipaka yao kuingia Syria na Iraq na hatimaye kujitokeza hali inayoshuhudiwa sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na kwengineko duniani.   

No comments: