Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Serikali ya
Wokovu wa Kitaifa ya Yemen kwa mara nyingine tena sambamba na kumtaka
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kufanya safari
nchini Yemen ili ashuhudie kwa karibu hali ya nchi hiyo ameitaka taasisi
hiyo ya kimataifa iunde kamati huru ya kutafuta ukweli.
Hisham Sharaf Abdullah amesisitiza
kuwa, ripoti iliyotolewa na ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu
wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na matukio ya wiki mbili zilizopita katika
mji wa Mokha huko Yemen imefumbia macho jinai zilizofanywa na muungano
wa nchi za Kiarabu dhidi ya raia katika mji huo.
Waziri wa Mashauri ya
Kigeni wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesisitiza kuwa, ni
vyema ofisi hiyo ijihusishe zaidi na ukiukaji wa wazi wa sheria za
kimataifa unaofanywa na ndege za kijeshi za muungano wa Kiarabu ambazo
kila siku zimekuwa zikifanya mashambulio 300 katika maeneo mbalimbali
ya nchi hiyo huku zikitumia silaha zilizopigwa marufuku ambazo unazipata
kutoka Uingereza, Marekani na Canada; hatua ambazo zimenyamaziwa kimya
na jamii ya kimataifa ambao haionyeshi radiamali yoyote ile.
Tangu kuanza vita nchini Yemen, viongozi wa Yemen na walimwengu
wamekuwa wakimtaka mara kwa mara mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa
katika masuala ya haki za binadamu afanye safari nchini Yemen ili
akajionee uhalisia wa mambo kuhusiana na ukiukwaji wa sheria za
kimataifa unaofanywa na Saudi Arabia.
Hata hivyo hadi sasa takwa hilo
halijatekelezwa. Ripoti za hivi karibuni kuhusiana na jinai za utawala
wa Aal Saud huo Yemen zimewafanya walimwengu wafahamu mambo ya kutisha
yaliyofanywa na Saudia kutokana na kutumia kwake mabomu yaliyopigwa
marufuku ya fosforasi na vishada dhidi ya wananchi wa Yemen.
Kwa hakika kile ambacho kimeandaa uwanja
na mazingira ya Saudia kuendelea kutenda jinai nchini Yemen na kuwaua
wananchi madhulumu wa nchi hiyo ni upuuzaji wa maafisa wa Umoja wa
Mataifa na kutouchukulia hatua utawala wa Aal Saud.
Kwa mfano, Ban
Ki-moon, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa aliitoa Saudia katika
orodha ya nchi zinazokiuka haki za watoto, hatua ambayo ilikuwa na
nafasi muhimu katika kuupa kiburi utawala wa Saudia cha kuendeleza jinai
zake huko Yemen.
Utendaji huo mbovu wa Umoja wa Mataifa unaonyesha ni kwa kiwango gani
taasisi hiyo ya kimataifa imeathiriwa na uingiliaji wa madola makubwa
ya Magharibi pamoja na pesa za mafuta za watawala wa nchi za Kiarabu.
Nukta nyingine muhimu ni kwamba, wakati Saudia imetenda jinai kubwa
nchini Yemen ambazo ni mfano hai na wa wazi wa jinai za pande tatu
zilizoainishwa katika Hati ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, yaani
jinai dhidi ya binadamu, jinai dhidi ya amani na jinai za kivita, kwa
uungaji mkono na madola ya Magharibi imechaguliwa tena kuwa mwanachama
wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na hata kuwahi kuwa
mwenyekiti wa kamati ya wataalamu wa umoja huo!
Umoja wa Mataifa unaojulikana kuwa eti
mlinzi wa amani na usalama wa dunia, katika kutekeleza majukumu yake,
badala ya kuwahami wananchi wa Yemen, umeathiriwa na lobi za Wasaudia na
kubadilisha msimamo kwa kupuuza uvamizi na jinai za Saudia huko nchini
Yemen. Hali ya kuwa mmoja wa wadau muhimu wa kushughulikia mizozo ya
kivita kimataifa ni Umoja wa Mataifa na asasi zinazofungamana na umoja
huo. Umoja wa Mataifa katika fremu ya nguzo zake kuu yaani Baraza Kuu na
Baraza la Usalama una jukumu la kufuatilia mizozo ya
utumiaji silaha kimataifa.
Baadhi ya nguzo zisizo kuu za Umoja wa Mataifa zina majukumu ikiwemo
kuwafikishia misaada wakimbizi, watoto, wanawake na waathiriwa wa vita;
na baadhi ya nguzo nyingine zina jukumu la kutafuta ukweli na kuandaa
ripoti kuhusuiana na ukiukaji wa haki za binadamu katika mapigano hayo,
ambapo katika hili pia Umoja wa Mataifa haujawa na utendaji mzuri, si
katika kuwafikishia misaada wananchi wa Yemen wala kuakisi jinai za
Saudia dhidi ya wananchi hao.
Hatua pekee ambayo imechukuliwa na Umoja
wa Mataifa kuhusiana na Yemen ni ile ambayo haikuwa na taathira yoyote
ya Ismail Ould Cheikh Ahmed mwakilishi wa UN katika masuala ya Yemen ya
kuitisha mazungumzo ya kitaifa. Mazungumzo hayo nayo hayajawa na natija
yoyote katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo kutokana na
mwakilishi huyo kutokuwa na nia safi kwa upande mmoja na hatua za
ukwamishaji mambo za Saudia na mamluki wake kwa upande wa pili.
Watawala wa Aal Saud kwa kufahamu vyema
kigugumizi na hatua za kusitasita za Umoja wa Mataifa na kutokuweko
irada ya kweli ya maafisa wa umoja huo katika kukabiliana na jinai za
Saudia, wamekuwa wakiendelea na jinai zao nchini Yemen bila ya wasiwasi
wowote.
No comments:
Post a Comment