Monday, June 26, 2017

Sheikh Jalala atoa Salam za Eid Fitri, awataka Watanzania kudumisha Amani na Umoja.

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala akiongea na Waandishi wa Habari katika kutuma Salama za kheri na fanaka za Eid fitri, iliyofanyika jana Masjid Ghadir Kigogo Post Dar e alaam. 
 Dar es salaam
Sisi kama Uongozi wa Masjid Ghadir, sisi kama Uongozi wa Chuo cha Imam Swadiq vilivyopo Kigogo Post Dar es salaam, vilevile sisi kama Viongozi, Maimam katika Madhehebu ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania.

Tunawatakia Watanzania wote kwa Ujumla, pasina kujali dini zao, pasina kujali madhehebu zao, tunawatakiwa kheri ya Eid, tusheherekee Eid hii kama wafuasi wa Dini tofauti tukiwa na sifa nzuri ambazo anazipenda mwenyezimungu (swt).

Katika kuipokea Eid napenda niiseme falsafa kubwa ya fungu anayoizungumzia mwenyezimungu ndani ya Qur’an, anaema malengomakubwa ya funga ili watu wawe wachamungu,ndio falsafa kubwa ya funga.

Sasa funga yetu hii ya mwaka huu ya 2017, funga hii itupelekee watanzania wale tuliofunga kuwa wachamungu, na nitaongea sifa tano kwa harakaharaka ambazo sifa hizi ni sifa za mchamungu.

Sifa ya kwanza ya jamii inayomcha mungu wanakuwa na mapenzi yaani wanapendana, kwahiyo funga yetu tulioifunga kwa mwaka huu iwe ni chachu ya watanzania wale waliofunga na wale ambao hawakufunga iwe ni chachu na sababu ya wao kupendana.Iwe ni sababu ya wao kushikamana, iwe ni sababu ya wao kuelewana.

Watanzania waislamu na wasiokuwa waislamu Wakristo na Madhehebu mengine watakapo pendana, watakapo shikamana, watakapo kuwa kitu kimoja, watajaribu kuondoa matatizo mengi yaliyopo katika jamii yao. 

Katika matatizo hayo watajitahidi kuhakikisha ufakiri, Umasikini unasambaratika katika jamii yaliyomo, kwa sababu waswahili wanasema seku zote kwamba kidole kimoja hakivunji chawa, kwa hivyo mapenzi yao baina yao, mapenzi yao, mshikamano utasababisha wapambane waondoe ufakiri, umoja wao utasababisha  wapate suluhisho la wajane tuliokuwanao Tanzania.

Umoja wao na mapenzi yao utasababisha watafute suluhisho na dawa ya mayatima, vilevile watatafuta dawa ya kuwasaidia walemavu, watu wanaoishi katika mazingira magumu, nasisi kama Waislamu wa Tanzania na waisokuwa waislamu wa Tanzania tutakapo leta mshikamano huo, basi ninauhakika haya yote tutaweza kuyafanya na itakuwa ile funga anayokusudia Mungu (swt) imefikia malengo.

Jambo la pili funga inasababisha kuleta kuvumiliana, mungu anaposema kwamba ameleta funga ili muwe wachamungu, moja ya sifa ya wachamungu wanatabia ya kuvumiliana, kwa hivyo watanzania wanaombwa na kitabu cha mwenyezimungu (Qur’an) ambacho kimeshuka katika mwezi wa ramadhani kwamba funga ifikie mahala watu wanavumiliana.

Tofauti zao za Madhehebu, tofauti zao za dini, tofauti zao za mitazamo, zinawafanya hawawezi kubaguana, hawawezi kugombana, hawawezi kupigana, wala hawawezi kusutana, hii ni sifa ya watu waliofunga na matarajio ya funga ya athiri kwa namna hiyo.

Jambo la tatu mungu anaposema ametufaradhishia kufunga ili tuwe wachamungu, moja ya maana ya uchamungu, ni watu kuwa kitu kimoja, na umoja hapa napenda niuzungumzie umoja wa aina mbili:
Kwanza Umoja wa Waislamu wenyewe kwa wenyewe, kamataneni na kama ya mwenyezimugu yote kwa pamoja wala msifarikiane, nyote muwe kitu kimoja kuwakitu kimoja ni dalili ya uchamungu.

Kuwa kitu kimoja ni dalili ya kuwa mnamuabudu mungu wenu mmoja, kwahivyo  ili funga yetu ikubaliwe, na ili funga yetu ilete athari katika jamii, lazima waislamu ni watu wanaokusanywa na mwamvuli mmoja Lailah ilallah, Muhammad Rasulullah, wafanye kila bidii kuhakikisha kwamba wamekuwa kitu kimoja na siki zote umoja ni sababu ya nguvu  katika jamii.

Pili ni Umoja wa kati ya Watanzania pasina kujali na kujali dini zao, pasina kujali madhehebu zao, mwenyezimungu anapotutaka tuwe wachamungu moja ya sifa ya wachamungu ni watu wanopenda kuwa kitu kimoja.

Watanzania waliofunga mwezi mtukufu wa Ramadhani na wale ambao hawakufunga wanaitwa wawe kitu kimoja wungane , washikamane,  umoja tuliokuwa nao ambao hatujuani kwa makabila yetu, hatujuani kwa madhehebu zetu, hatujuani kwa dini zetu,bali tunajuana kwa anuani ya utanzania.

Mwisho naitakia Tanzania yenye kheri na Baraka na fanaka , naitakia Tanzania izidi kuwa kisiwa cha amani na maelewano na pale ambapo panakosa amani basi mwenyezimungu aparudishe pawe na amani kwa haraka iwezekanavyo, nawatakia Eid njema, yenye Baraka yenye kheri, yenye mafanikio na Eid ipite kwa salama salmini na zile sifa nzuri tuliokuwa nazo kipindi cha swaum ya ramadhani ziendelee kuwepo katika jamii ya watanzania ili ziweze kuwaathiri watu wote na nje ya mipaka yetu, namshukuru mungu .Asanteni sana.

Imetolewa na:
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Itnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala
Waandhisi wa Habari wakiwa makini katika majukumu yao katika salamu za fanaka zinazotokewa na Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala

No comments: