Wednesday, April 11, 2018

Kamati ya Mshikamano wa Tanzania na Palestina Wamelani Kauli iliyotolewa na Chief Rabbi kuhusu Waafrika.

Mkuu wa dini ya Wayahudi nchini Israel, Chief Rabbi Yitzhak Yosef ambaye, wakati wa mahubiri  aliwafananisha Waafrika na kima.
KAMATI YA MSHIKAMANO WA TANZANIA NA PALESTINA

Dar es Salaam
Risala kwa Vyombo vya Habari

Israel ni nchi ya Ukaburu inayodhalilisha Waafrika

KAMATI ya Mshikamano wa Tanzania na Palestina inalaani vikali matusi yaliyotamkwa na mkuu wa dini ya Wayahudi nchini Israel, Chief Rabbi Yitzhak Yosef ambaye, wakati wa mahubiri  aliwafananisha Waafrika na kima.

Yosef ni mmoja kati ya wachungaji wawili wakuu wanaoteuliwa na serikali ya Israel. Alipokuwa akihubiri katika hekalu la Kiyahudi hivi majuzi aliwazungumzia Waafrika na akatumia neno “kushi” amabalo katika lugha ya Kiibrania ina maana ya “kima” .

Hii si mara ya kwanza kwa mchungaji huyu mkuu wa Israel kutumia maneno ya kuwadhalilisha Waafrika. Katika mahubiri yake ya Mei mwaka jana alisema wanawake wana tabia ya wanyama kwa sababu ya mavazi yao. Halafu mnamo Machi 2016 alitangaza kuwa watu wasio Wayahudi hawapaswi kuishi nchini Israeli

Mawazo ya mchungaji huyu hayakubaliki, lakini hayashangazi sana kwa sababu wakati wote Israel yenyewe imekuwa na msimamo wa kuwabagua na kuwadhalilisha Waafrika na wazawa Wakipalestina. Ukaburu huu umekuwa ukiongezeka, siyo tu miongoni mwa Wayahudi wa Israeli bali hata miongoni mwa serikali ya Israel na watendaji wake.


Ndio maana hivi sasa Israel iko mbioni kuwafukuza maelfu ya Waafrika wanaoishi na kufanya kazi huko. Tayari onyo limetolewa kuwa kuanzia tarehe 1 Aprili 2018 kama Waafrika hao hawataondoka basi watakamatwa na kufungwa gerezani bila kikom.

Israel imetangaza kuwa Waafrika wanaoishi ni tishio kwa utambulisho wa Kiyahudi. Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyau amekuwa akitaka wafukuzwe na kusema kuwepo kwao nchini Israel ni tishio kwa “amani na usalama”. Amesema Waafrika hao ni magaidi

Naye waziri wake wa mambo ya ndani, Eli Yishai amesema Waafrika walio Israel wanapaswa wajue kuwa nchi “hii ni yetu sisi watu weupe”. Na waziri wa utamaduni na michezo , Miri Regev amesema Waafrika ni sawa na maradhi ya “saratani”

Hii ni Israel, nchi ya kikaburu ambako wanafunzi katika chuo cha uhandisi wanaulizwa suali kuhusu mapanya wanaopaswa kukamatwa na kuangamizwa. Mapanya hao si wengine bali ni Waafrika

Hii imefanyika katika chuo kikuu cha Ben-Gurion ambako mkuu wa kitivo cha uhandisi, “Profesa” Moshe Kaspi ametoa suali kwa wanafunzi wake likisema katika kazi ya kuchimba mtaro ili kujenga reli ya chini ya ardhi jijini Tel Aviv, wanakutana na mapanya wengi. Inaamuliwa kuwasafirisha panya hao hadi Afrika ambako wanahitajika katika utengenezaji ya chanjo ya kichaa cha mbwa. 

Na ndio maana duniani kote kumekuwepo na kampeni ya kulaani ukaburu huu wa Israel katika mtandao wa jamii  (#IsraeliApartheidWeek). Huko Afrika Kusini kampeni hii iliendeshwa kati ya tarehe 12 na 18 Machi pamoja na mikutano katika miji kadha. ili kupata habari kamili kuhusu huu ubaguzi na ukaburu wa Israel dhidi ya Waafrika

Hata katika jiji la Tel Aviv watu takriban 25,000 wamekusanyika kupinga sera ya Israel ya kuwafukuza Waafrika ambao wameomba hifadhi. 

Mabango yalibebwa yakisema “Hakuna tofauti kati ya damu zetu, ni kwa sababu sisi sote ni wanadamu”
Walikuwa wanapinga sera ya Israel ya kuwasafirisha Waafrika hadi Rwanda na Uganda . Kati yao ni watu karibu 38,000 kutoka Eritrea na Sudan ambao tayari wamepewa notisi yaa kuondolewa na kupelekwa Uganda na Rwanda.

Hata Waafrika walioingia Israel kwa kudai wao ni Wayahudi nao wanakabiliwa na tishio la kufukuzwa. Chini ya ukaburu wa Israel sasa wanaambiwa wao sio Wayahudi
Almuradi Israel si tofauti na Afrika Kusini wakati wa utawala wa makaburu. 

Ndio maana ulimwengu leo unaendesha kampeni ya kuwawekea vikwazo kama ilivyofanyika wakati ule wa makaburu wa Afrika Kuini (BDS)

Aidha, Kamati inaungana na jumuiya ya Kimataifa katIka maadhimisho ya siku ya ARDHI YA PALESTINIA kwa kulaani uendeleaji wa uporaji wa ardhi ya Wapalestina. Katika maandamano ya Amani ya kuadhimisha siku ya ARDHI  yaliofanyika huko Ukanda wa Gaza Wapalestina 17 waliuliwa
Maandamano hayo yanaendelea huko Gaza na jumla ya Wapalestina 30 wameuliwa na mamia kujeruhiwa na wanajeshi wa Israel wanaotumia risasi za moto, vifaru na mabomu ya machozi. 

Kati ya waliouawa ni mwanahabari wa Kipalestina aliyevaa nguo zilizomtambulisha kuwa ni mwandishi. Waandishi wengine watano wamejeruhiwa
Tunalaani kwa nguvu zote mauwaji hayo. Kamati inasikitika  kwa jumuiya za kimataifa kukaa kimya licha ya mauaji haya ya waandamanaji wasio na silaha yanayoendelea hadi  leo.

Kamati inaiomba serekali na Jamii ya Watanzania kuzidi kupaaza sauti zao katika kulaani na kupinga ukandamizwaji na mauwaji wanaofanyiwa ndugu zetu wa Palestina na watawala wa Israel
Kamati inawaomba Watanzania wasikae kimya katika suala hili na tukumbuke maneno yafuatayo ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Ikiwa kweli tunataka kumuenzi tuyatekeleze maneno yake kwa vitendo.

"Hatujawahi kusita katika kuunga mkono haki ya watu wa Palestina kuwa na ardhi yao. Kizazi chetu kilikuwa ni kizazi cha harakati za kitaifa kwa ajili ya uhuru wa nchi yetu na hivyo ndivyo tulivyokuwa. Lakini masaibu ya Wapalestina ni mabaya zaidi na yasiyo halali, wanaporwa nchi yao, wao ni taifa bila ardhi. Na kwa hivyo wanastahili uungwaji mkono wa Tanzania na Dunia kwa ujumla."
-Mwalimu Nyerere

AHSANTENI
ABDULLAH M.OTHMAN
MWENYEKITI.
KAMATI YA MSHIKAMANO WA TANZANIA NA PALESTINA

Saturday, March 10, 2018

“Siku ya Kuzaliwa B.Fatma Zahra (a.s) ndio Siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani” Maulana Sheikh Jalala

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akiongea na Waandishi wa Habri katika Kikao cha kuzungumzia kumbukumbu ya Kuzaliwa Mtoto wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), ambae ni Bi,Fatma Zahra (a.s), kulia kwake ni Sheikh Muhammad Abdu.
Tarehe kama ya leo (20, Jamadal Akhirah,1439 sawa na 09-03-2018) leo amezaliwa bint wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambae ni Bibi Fatma Zahra (a.s),Mtoto huyu au Bint huyu au Mama huyu kwasababu ya daraja lake alilokuwanalo ndani ya Uislamu, Viongozi wa Dini ya Kiislamu, Masheikh wakaitangaza siku ambayo aliozaliwa Mama huyu ni siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani,siku hiyo tumekuwa tukiikumbuka kila mwaka, siku aliyozaliwa mama huyu ni siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani kote.
 
Yanayotufanya tumkumbuke mama huyu, kwanza ni mwanamke mtakatifu, pili ni mwanamke aliegubikwa na sifa nyingi nzurinzuri zilizojaa ndani ya kitabu kitakatifu cha Quran, lakini vilevile mama huyu amegubikwa na sifa nyingi kutoka kwenye kinywa cha Mtume Muhammad (s.a.w.w), Mama huyu alikuwa kipenzi cha mtume Muhammad (s.a.w.w).

Tunapozungumza Wanawake watakatifu kama vile mama Asia, kama vile mama Khadija, kama vile Mariam aliemzaa Nabii Issa / Yesu (a.s), tunamzungumza vilevile Bi Fatma Zahra ni katika gurupu la wanawake hao.

Bi Fatma Zahra alikuwa na Elimu, Maarifa bila shaka tunahitajia Mama zatu na Dada zetu leo wawe na maarifa na Elimu nzuri,Dunia leo inatafuta maadili mema, dunia leo inachangamoto kubwa ya kupoteza maadili yao, ambayo Mungu amewaumba nayo, Bi Fatma Zahra (a.s) alisifika na maadili mema katika Nyanja zote, pia alisifika na Ukarimu.

Tunaamini vilevile Nyumba ya watu wenye Imani, Nyumba ya Watu wanaomtambua Mungu, Nyumba ya watu wenye hofu na Mungu, Nyumba hiyo inakuwa nyumba salama, bila shaka nyumba inapokuwa salama, jamii inakuwa salama, jamii inapokuwa salama Taifa nalo linakuwa salama, kwahivyo Nyumba ya Bi Fatma Zahra (a.s) ni Myumba ya Mwanamke ambae alikuwa akimuabudu Mungu.

Katika siku hii ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani napenda nigusie jambo zima la haki za Mwanamke ndani ya Uislamu, ziko baadhi ya fikra zinazoona Uislamu haukumpa Mwanamke haki zake, laa, napenda nisieme katika siku hii ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani kwa kukumbuka kuzaliwa kwa Binti ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), niseme yakwamba Uislamu unamuangalia Mwanamke na Uislamu unampa Mwanamke haki zake zote.

Mwanamke anayohaki ya kurithi ndani ya Uislamu, Dini ya Uislamu inampa Mwanamke haki ya Kumiliki kama vile mwanaume anavyomiliki,Haki ya kufanya Kazi,Haki ya kuendesha gari,haki ya usawa na haki zingine ambazo ziko kwa mujibu wa dini ya Uislamu.

Katika siku ya leo siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani napenda nizungumzie jambo la kuvaa sitara au hijabu, Hijabu au Sitara katika Uislamu hakiwekwa kama jambo la kumdhalilisha mwanamke laaa, sitara au hijabu ambayo yakuigwa kutoka kwa Bint ya Mtume Fatma Zahra (a.s), Sitara au hijabu yake haikumzuia kufanya kazi, sitara yake haikumzuia kufanya mambo ya Kiislamu, 


sitara yake haikumzuia kuingia darasani kusomesha, sitara yake haikumfanya aache kutoa Hotuba mbele ya Maswahaba wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), kwa hivyo sitara au hijabu ni kitu cha kumsitiri mwanamke, ni heshima kwa mwanamke,ni adabu kwa mwanamke, bali mwanamke amekuwa na dhamani kubwa kwa sababu ya sitara yake.

Mwisho napenda kugusia jambo muhimu sana ambalo ni jambo la kuigwa kutoka kwa binti ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambae ni Fatma Zahra (a.s), Jambo la Malezi, Mwanamke moja ya kazi aliyokuwa nayo ni kulea jamii iliyokuwa njema,Kama tunataka tutengeneze jamii ya Wachamungu, jamii ya wakweli, jamii ya watu wenye imani, jamii ya watu wanaopenda kusaidiana, ni lazima hili lianze katika ngazi ya familia, na hakuna analolitengeneza hilo isipokuwa ni Mama.

Mama ndio mwenye nafasi ya kutengeneza jamii yenye wakweli, mama ndio mwenye nafasi ya kutengeneza wabunge ambao kesho watatuwakilisha katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ahadi zao walizotuahidi na kuzitekeleza, kwasababu gani, Mwakilishi huyu ameleleka katika nyumba ambayo inapoahidi inatekeleza, 


kama tunataka kutengeneza Wachapa kazi ambao hawachoki, kama tunataka kuunda watu ambao ni hapa kazi hilo linarudi katika ngazi ya familia na unaona Bi Fatma Zahra (a.s)  angalia alivyowalea na kuwatengeneza Watoto wake kama Imam Hassan (a.s), Imam Hussein (a.s) na Bi Zainab (a.s).

Bi.Fatma Zahra ni Mtoto wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Mama yake ni Bi.Khadija, Mume wake ni Sayyidina Ali (a.s), Watoto wake ni Imam Hassan (a.s), Imam Hussein (a.s) na Bi.Zainab (a.s), Babu yake ni Abdallah, Bibi yake ni Amina.

Imetolewa na
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania
Maulana Sheikh Hemed Jalala


Sunday, January 28, 2018

Bi. Aitaka Serikali kupitisha Sheria Maalumu kwa ajili ya Wajane.





Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu     Bi. Helen Kijobi Simba ameitaka Serikali kupitisha Sheria maalumu kwa ajili ya Wajane kwa kufuta Mila na Desturi ambazo ni kandamizi kwa wajane zinazosababisha kukosa haki zao na kupelekea kunyanyaswa na familia husika.

Aidha Bi Simba ambae pia ni Mjumbe wa Bodi ya Chama cha Wajane Tanzania ameiomba serikali kuwachukulia hatua kali za Kisheria kwa wale wote wanaoendekeza Mila na Desturi Kandamizi kwa wajane pia kusaidia kwa kutoa elimu katika hizo Mila na Desturi zilizopitwa na wakati ili ziweze kuondoka.
 
Wito huo ulitolewa jana katika Kongamano la Kimataifa lililoandaliwa na Chama cha Wajane Tanzania, Dar es salaam, taasisi mbalimbali zinazohusiana na kutetea haki za binadamu na Mambo ya Uchumi zilishiriki.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Wajane Tanzania Madam Rose Sarwat alisema lengo kuu la Kongamano hili la Kimataifa ni kuweza kukaa Wajane wan chi nzima kuangalia changamoto za wajane  zinaweza kutatuliwa vipi? Na chanzo cha changamoto ni nini? Na jinsi gani tunaweza kuungana kama wajane wa Tanzania na nchi jirani kutatua changamoto zetu.
 
Kongamano hili la Kimataifa  limewakutanisha Wawakilishi wa Chama cha Wajane kutoka Mikoa yote ya Tanzania, Kutoka nchi za Jirani kama Kenya, Malawi na DRC-Congo, kongamano hili limeanza Jana, na linatarajiwa linatarajiwa kudumu kwa kipindi cha siku tatu katika Mwezi huu wa Januari 2018.

Sunday, December 24, 2017

SALAMU ZA KRISMAS NA MWAKA MPYA KWA WAKRISTO WOTE TANZANIA NA DUNIA-JALALA

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akitoa salamu za Krismas na Mwaka Mpya, leo Dar es salaam.
TAARIFA KWA UMMA
SALAMU ZA KRISMAS NA MWAKA MPYA KWA WAKRISTO WOTE TANZANIA NA DUNIA.

24/12/2017
Amani ya Mwenyezimungu iwe juu yenu nyote.Salam hizi za Mkono wa Krismas kwa ndugu zetu Wakristo wa Tanzania na Wakristo wote Duniani wanaosheherekea Mazazi (Kuzaliwa) kwa Nabii Issa   (a.s) Mtume wa Mungu kwa ndugu zetu wakristo ni Yesu Kristo.

Mkono huu wa Kristmass, Mkono huu wa Eid ni Mkono uliobeba Umoja, ni mkono uliobeba Mshikamano ni Mkono wa Eidi, ni mkono wa Krismaa uliobeba amani na Maelewano. Lakini kubwa zaidi la kujiuliza na huenda wengi wakajiuliza swali hii kwamba kwanini Viongozi wa Dini wa Kiislam katika siku hii ya kuzaliwa Yesu Kristo au Nabii Issa (a.s) kwa Wiaslam, viongozi hawa wa Kiislam hususan Wafuasi wa Madhehebu ya Ahlulbayt (a.s) au Mashia watoe Mkono wa Krismas,mkono wa kheri, 

mkono wa Baraka kwa ndugu zao wakristo Watanzania na wa Dunia kwa ujumla ni kwasababu chache za harakaharaka nitakazozieleza
Sababu ya kwanza tutambue sisi Waislam na ndugu zetu Wakristo sote tunakusanywa na neon moja kwamba sisi ni Waumini, 

sote tunamuamini Mungu mmoja ambae ndie aliyeumba Mbingu na ardhi na akawaumba wanadam wote hilo la kwanza, Sote tunaamini kwamba kuna vitabu vya Mungu vilivyoshushwa hapa duniani, tunaamini uwepo utumwa mitume wa Mungu na vilevile tunaamini siku ya mwisho.

Kwahivyo kuyaamini haya yanatukusanya sisi watanzania Waislam na Wakristo chini ya mwamvuli mmoja wa imani, kwahivyo leo hii waislam tunapotoa mkono wa Krismas, mkono wa eid kwa ndugu zetu wakristo ni kwasababu ni waumini wenzetu katika kumuamini Mungu mmoja, katika kuamini siku ya mwisho na katika kuamini mitume waliotumwa na kutuletea ujumbe hili la kwanza.

La pili kwanini mkono wa Krimsaa kwa ndugu zetu Wakristo, ni kwasababu sisi wote tunakusanya  na anuani ya Utanzania, Waislam tulioko hapa ni Watanzania, wakristo tulioko hapa ni Watanzania, kama sote ni watanzania ni wajibu wetu sote kuilinda Tanzania yetu. Kama sisi Wislam na Wakristo ni Watanzania ni wajibu wetu umoja na mshikamano wetu kama Watanzania, kama sisi sote ni watanzania ni makosa makubwa kufungua mwanya wowote wa mvutano kati ya Waislam na Wakristo hapa Tanzania, kwanini kwa sababu sote tunakusanywa  ni Utanzania.

Kwasababu sisi sote ni watanzania ni lazima tuwe na sifa ya kuvumiliana, itikadi zetu, fikra zetu na mitazamo yetu isitugawanye kwa kuwa sisi tunakusanywa na neon Utanzania,Na Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwa sisi waislam anasema “kupenda inchi yako ni katika imani” kwahivyo leo hii sisi kama Viongozi na kama Waislam na kama Waislam Shia Ithnasheriya tunapotoa Mkono wa Krisma, mkono wa Baraka na mkono wa Eid kwa ndugu zetu Wakristo moja ni kuenzi huu Utanzania tuliokuwanao ambao ni kitu muhimu na ni kitu kikubwa,Lingine ni kwanini tunatoa mkono wa Krismas, 

ni kwasababu sisi Waislam, Dini ya Uislam ni dini ya Mapenzi, Dini ya Uislam ni dini ya kufahamiana, Dini ya Uislam ni dini ya amani, Dini ya Uislam ya kupendana, anaeueleza Dini ya Uislam sio dini ya kupendana huyo hajauelewa Uislam.

Kwahivyo Uislam ni dini ya Mapenzi, ni dini ya Maelewano ni dini ya Maelewano,Mtume Muhammad (s.a.w.w) anatufunza siku zote anasema “ penda watu wapate kile ambacho unachopenda ipate nafsi yako” kwahivyo Uislam ni dini ya upendo, uislam ni dini ya Maelewanoni dini ya masikilizano leo hii tunapotoa mkono wa Baraka na mkono wa kheri na fanaka katika Eid ya Krismass malengo makubwa ni kuwaonyesha ndugu zetu wakristo kwamba Uislam ni dini inayompenda kila mtu, Uislani dini iliyohimiza ujirani mwema na ujirani huu mwema hauwezi kudhibitika wala kufanyika pasi na watu kupendana.

Kwahivyo mkono huu wa Krismass ni mkono wa kuwaonyesha ndugu zetu Wakristo Wayanzania kwamba Uislam ni dini ya mapenzi, kwamba uislam ni dini ya kuelewana, Sayyidina Ali (a.s) kiongozi baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) anawausia watoto wake anawambia “Hala hala nawahusieni majirani” Sayyidina Ali (a.s) alipokuwa anawahusia watoto wake swala la Majirani, hajawaambia Majirani Waislam, hajawaambia Majirani wachamungu la, kawaambia Majirani yaani majirani wote ima wachamungu, Wakristo, Waislam na hata wasiokuwa na Dini.

Kwahivyo kitendo cha leo cha sisi kutoa Mkono wa Krismass, mkono wa Kheri na Baraka kwa ajili ya ndugu zetu watanzania wasiokuwa Wiaslam ni kutaka kuwaonyesha kuwa Uislam ni dini ya mapenzi uislam ni dini ya maelewano.Nukta nyingine muhimu kwanini Mkono wa Krismass,mkono wa Kheri na Baraka kwa ndugu zetu Wakristo  kwa sababu hakuna uadui kati ya Uislam na Ukristo, hakuna Uadui kati ya Waislam na Wakristo, 

Ukimsoma Mtume Muhammad (s.a.w.w) na ukiisoma Qur’an yetu na ukisoma mwenendo wa watu waliokuja baada ya mtume Muhammad (s.a.w.w) utapata yakwamba wanavyoueleza Uislam, Uislam na Ukristo sio uadui kati yao bali ni Udugu na maelewano kati yao.

Iangalie Qur’an inavyowasemesha Wakristo inawaitaje, inawaita “Ahlul Kitabu” enyi watu waliopewa Injili, enyi watu mliopewa Taurat, enyi watu mliopewa Zaburi hivi ndivyo Qur’an inavyowasemesha Wakristo, kwahivyo Mkono huu wa Kheri na Baraka ni kuonyesha ya kwamba hakuna Uadui hata kidogo kati ya Uislam na Ukristo, kati ya Waislam na Wakristo.

Ukiisoma Qur’an, Qur’an ina sura nzima inayoitwa suratul Mariam yaani sura ya Mariam, mariam ambae kwa ndugu zetu Wakristo wanamwita “Bikira Maria” sisi kwetu Waislam tunamwita “Mariam Mtakatifu” ni sura nzima inayobeba jina la Mariam, kwahivyo lau Uislam ungelikuwa na Uadui na Ukristo kusinge kuwa na sura inayoitwa sura ya Maria.

Vilevile ndani ya Qur’an kuna sura ya Ruum yani sura ya Roma, Roma ni Wakristo ndani ya Qur’an, na Waislam wanaisoma sura hiyo kila siku ya asubuhi na mchana
Mwisho nimalizie kwa nukta yakwamba Kitendo cha sisi kutoa Mkono wa Kheri ya Krismass kwa ndugu zetu Wakristo watanzania ni kuonyesha yakwamba Uislam ni dini ya Amani, Uislam ni dini inayopenda watu wakae vizuri, Uislam ni dini inayopenda mahusiano mazuri kati yao na ndugu zao Wakristo, 

na kwamba Uislam katika vitu inavyovipiga vita ni kitu kinachoitwa Ugaidi, Uislam na Ugaidi ni vitu viwili tofauti, ni kuontesha ya kwamba Uislam hauna kitu ukatili kwa wasiokuwa Waislam
Kitendo hiki cha kutoa mkono wa Krismas kwa ndugu zetu Wakristo ni kuonyesha kwamba Uislam hauna chinja chinja kwa Wakristo, Uislam hauna ukatili kwa Wakristo, 

Uislam ni amani na maelewano kwa Waislam na wasiokuwa Waislam.mwisho niwatakie ndugu zetu wakristo Watanzania Eid njema, Krismass njema ya kusheherekea kuzaliwa Yesu Kristo au Nabii Issa (a.s).

Na vilevile ni itakie amani serikali yetu ya awamu ya tano ambayo imeweza kutufikisha hapa kwa utulivu na kwa maelewano sisi Waislam Watanzania na Wakristo wa Tanzania, na ninamuomba Mwenyezimungu Serikali hii awape hekima, awape busara ili waendelee kutuongoza kwa salama na kwa amani na 

vilevile mwenyezimungu nchi hii azidi kuboresha maelewano kati yetu sisi Waislam na kati ya ndugu zetu Wakristo, na yeyote ambae anania ya kuleta chokochoko ya kuvunja amani hii, basi chokochoko yake isiweze kuingia katika nchi yetu ya Tanzania na katika taifa hili, Mungu azidishe kulibakiza Taifa hili la Tanzania katika Amani na kisiwa cha amani na mahala pa maelewano.Asanteni sana na Mungu awabariki.

Imetolewa Na:
Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala