WANANCHI wanaoishi katika Vijiji vya
Mkenda na Mitomoni vilivyopo kandokando ya mto Ruvuma wilayani Nyasa
mkoani Ruvuma wamesema changamoto kubwa waliyonayo ni
mazingira magumu ya miundo mbinu ambayo inasababisha ugumu wa ufikishaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kutoka Bohari ya Dawa (MSD).
Wakazi hao wamesema kuwa, mazingira ya
kufikisha dawa kwenye vijiji hivyo hutegemea zaidi usafiri wa kuvuka mto
Ruvuma ambapo hulazimika kutumia boti,ambapo hata hivyo maisha yao
yanakuwa na mashaka ndani ya mtumbwi hiyo ambayo iko wazi kutokana na
mto huo kuwa na mamba wengi.
"Changamoto yetu kubwa ni usafishaji wa
dawa kuja hapa kijijini kutokana na kutegemea zaidi mto huu ambao una
mamba wengi, hata mwaka huu mwanzoni mtumbwi huu mnaouona ulipinduka na
watu wakiwapo wauza mitumba waliuawa na mamba; lakini tunashukuru
Bohari ya Dawa (MSD) kwani wao wanaweza kutuletea dawa kwa wakati"
alisema Mwenyekiti wa kamati ya Afya wa kijiji cha Mitomoni Omar Hassan.
Alisema ili kuondoa changamoto hiyo,
wanaiomba serikali kuhakikisha inaboresha miundombinu ya barabara, ili
dawa hizo zisafirishwe kwa njia ya barabara badala ya kutegemea mto
huo.
Alisema yeye na kamati yake wamekuwa wakipokea dawa mara nne kwa mwaka kutoka MSD na kuzihakiki kwa ajili ya matumizi.
"Pamoja na changamoto ya miundombinu
lakini tumekuwa tukihakikisha dawa zinazoletwa na MSD zinafika kituoni
na kutumika ipasavyo,"alisema.
Alisema kutoka Songea mjini hadi Kijiji
cha Mitomoni, Songea vijijini, katika kituo hicho cha afya ni km 135 na
MSD imekuwa ikihakikisha dawa hizo zinafika.
Alisema changamoto zinakuwa kubwa zaidi
kipindi cha mvua kwa kuwa miundombinu ya barabara hadi kufika kivukoni
ni tatizo na kuna wakati dawa zinafika usiku na zinatakiwa kuvushwa
usiku huo huo.
Hassan alisema changamoto hiyo ya mamba
katika mto huo anaijua vizuri kwani mtoto wake Sanifu Omar (27),
alipoteza maisha kwa kuliwa na mamba wakati alipokuwa akisafirisha
abiria kwa kutumia mtumbwi.
Mkazi wa Kijiji cha Mitomoni Khadija
Salum alisema wamekuwa wakipata dawa zote muhimu katika kituoni hicho
ikiwemo za mama mjamzito na mtoto bila ya ubaguzi na kwa wakati.
"Mimi nina watoto watano kuanzia
ujauzito wa kwanza sijawahi kukosa dawa hapa pamoja na ugumu wa
miundombinu lakini dawa zinafika hivyo serikali ione haja ya kuboresha
barabara zetu," alisema.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mitomoni,
Ivo Hekela, alisema kijiji hicho kinahudumia agonjwa 12,000 kutoka
vijiji vitano ambavyo ni Mitomoni, Mipotopoto,Konganywita,Mkenda,Uhuru
na Mozambique.
Meneja wa MSD Kanda ya Iringa, John
Sipendi, alisema wamekuwa katika changamoto ya kufikia vituo hivyo vya
pembezoni ikiwa ni pamoja na kutumia muda mrefu kufikisha dawa na wakati
wa mvua kukwama kwa magari njiani na gharama za usafirishaji kuogezeka.
Madereva wa MSD Kanda ya Iringa wamesema wamekuwa wakishindwa kushusha dawa wakati wa mvua za masika kutokana na mto huo kujaa maji hivyo hulazimika kulala kijijini hapo kwa siku mbili hadi tatu.
No comments:
Post a Comment