Harakati ya Jihad Islami imesema, 'tunaamini kuwa watu wa Morocco watapinga vikali uamuzi huo wa kuanzisha uhusiano na Israel."
Naye msemaji wa Hamas Hazem Qassem ameutaja uamuzi wa Morocco kuwa ni dhambi.
Kwa upande wake, Bassam As-Salhi, mwanachama wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina amelaani uamuzi huo wa Morocco. Amesema haikubaliki kwa nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano na utawala wa Israel ambao unakalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Jana Alhamisi, Mfalme wa Morocco Mohammed VI alimwarifu rais Donald Trump wa Marekani kwenye mazungumzo kwa njia ya simu kuwa amekubali kurejesha mawasiliano ya kiserikali na kuanzisha uhusiano wa kibalozi na utawala wa Israel haraka iwezekanavyo.
Marekani nayo imesema itatambua mamlaka ya Morocco katika eneo la Sahara Magharibi la nchi hiyo ambalo limejitangazia uhuru.
Mfalme huyo pia amempigia simu Rais wa Mamlaka ya Ndani wa Palestina Mahmoud Abbas na kudai kuwa Rabat inaunga mkono kile kinachotajwa kuwa ni utatuzi wa mgogoro wa Palestina kwa msingi wa kuundwa 'nchi mbili"
Itakumbukwa kuwa, katika hatua inayopingana kikamilifu na malengo matukufu ya watu wa Wapalestina ya ukombozi wa nchi yao, tarehe 25 Septemba, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House mjini Washington na kuhudhuriwa na rais wa Marekani Donald Trump na waziri mkuu wa utawala haramu wa Israel Benjamin Netanyahu. Sudan pia imefuata mkumbo huo na kutangaza utayarifu wa kuanzisha uhusiano na utawala huo bandia.
Hatua hizo za nchi za Kiarabu zinaendelea kukosolewa na kulaaniwa vikali na viongozi wa Palestina pamoja na wapenda haki kote duniani wakisema kuwa ni usaliti wa wazi kwa harakati za kupigania ukombozi wa Palestina.
No comments:
Post a Comment