Wednesday, April 15, 2015

Marufuku wanachama wa ACT - Wazalendo kushabikia Ukawa.



Kiongozi wa Chama cha ACT-Tanzania, Zitto Kabwe akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mwembetogwa, Iringa 

Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kila mwanachama anapaswa kuwaunga mkono wagombea watakaopitishwa na chama hicho katika nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao, kwani kinyume chake ni kukisaliti na adhabu yake ni kufukuzwa.

Mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira alisema mwishoni mwa juma kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, chama hicho kinahitaji nguvu za pamoja.

“Sisi bado hatujajiunga na Ukawa, hivyo wanachama wetu wanapaswa kulitambua hilo na kuepuka kushiriki kwenye ushawishi wa kufanya kampeni za wagombea wa vyama vingine. 

Hata kwenye katiba yetu tunasema sasa tunalenga zaidi katika kujiimarisha ili kutoa ushindani mzuri wa kisiasa katika uchaguzi huu,” alisema.
 
Kiongozi wa Chama cha ACT-Tanzania, Zitto Kabwe akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mwembetogwa, Iringa
Katiba ya ACT, imeeleza wazi kuwa pamoja na sababu nyingine na kwa mujibu wa kanuni zitakazotungwa na Halmashauri Kuu, mwanachama yeyote ambaye atasaidia kushawishi, kujiunga, kutoa tamko la kuunga mkono chama kingine au mgombea wakati chama kimeweka mgombea wake kwa mujibu wa sheria za nchi, atakuwa amepoteza uanachama wake.

ACT- Wazalendo tayari imetoa ilani yake ya uchaguzi ikionyesha kwamba iwapo itaingia madarakani, itawajibika kwa wananchi kwa kuweka kipaumbele katika maeneo manne ambayo ni hifadhi ya jamii, uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira nyingi na bora, afya na elimu.

Kauli hiyo ya ACT linakuja huku kambi ya vyama kadhaa vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ikiwa kwenye mchakato wa kuunganisha nguvu ili kusimamisha mgombea mmoja wa urais na kuachiana majimbo katika baadhi ya maeneo.

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia amewahi kunukuliwa akisema kuwa umoja huo unaoundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD umehamishia nguvu zake kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Mbatia alisema tayari umoja huo umeunda kamati maalumu kutafuta namna ya kumsimamisha mgombea mmoja wa urais na kuachiana majimbo.
 
Kiongozi wa Chama cha ACT-Tanzania, Zitto Kabwe akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mwembetogwa, Iringa 
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema tayari kamati zimeundwa na zinaendelea na kazi ya kuratibu mpango huo mahsusi, unaolenga kuiondoa CCM madarakani.

“Lengo letu ni kuhakikisha Ukawa ina nguvu ya kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na katika mpango huo, vyama vitaachiana majimbo na viti vya udiwani kulingana na nguvu ya chama katika sehemu husika,” alisema.

Mkakati huo uliopangwa na Ukawa, unaelezwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa ni kombora kwa CCM, kwani endapo utafanikiwa, utakiweka chama hicho tawala katika wakati mgumu katika Uchaguzi Mkuu uliopangawa kufanyika Oktoba mwaka huu.
 Chanzo;Mwananchi.com

Zarif: Mashambulizi ya Saudia si suluhisho huko Yemen


Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mashambulizi ya kijeshi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen si suluhisho la mgogoro wa nchi hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya IranMuhammad Javad Zarif


Muhammad Javad Zarif ambaye alikuwa akihutubia maafisa wa serikali ya Uhispania mjini Madrid amesema kuwa historia imethitisha kuwa hakuna nchi ya kigeni iliyowahi kuidhibiti Yemen na kwamba mashambulizi ya mabumu yanayofanywa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo yanaharibu miundombinu tu. 

Zarif ametaka kusitishwa mashambulizi hayo mara moja na kuruhusu misaada ya kibinadamu kupelekwa nchini Yemen.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amezungumzia kadhia ya nyuklia ya Iran na kusisitiza kuwa Tehran daima imekuwa ikifanya jitihada za kupata teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani. 

Amesisitiza kuwa Iran haijawahi kukengeuka sheria katika jitihada zake za kupata teknolojia ya nishati ya nyuklia.

Tuesday, April 14, 2015

Nguvu za kijeshi haziwezi kusimamisha nyuklia ya Iran



Serikali ya Marekani kwa mara nyingine tena imesema kuwa, chaguo bora kabisa kwa Washington la kuamiliana na Iran ni kupitia njia za kidiplomasia na kwamba, nguvu za kijeshi katu haziwezi kusimamisha miradi ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 
 

Wendy Sherman, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani

Wendy Sherman, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ambaye pia ni mkuu wa timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Marekani amesema bayana kwamba, njia itakayokuwa na taathira nzuri zaidi ni ya kidiplomasia. 

Amedai kuwa, hatua yoyote ile ya kijeshi ya Israel au Marekani dhidi ya Iran itaweza tu kuirejesha nyuma Iran miaka miwili au mitatu hivi. 

Sherman alikuwa akisema hayo katika mazungumzo yake na ujumbe wa kidiplomasia wa Israel ikiwa ni katika juhudi za Washington za kuifikishia Israel na lobi za Kizayuni ujumbe wake kuhusiana na makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni huko Lausanne Uswisi kati ya Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na Marekani, Uingereza, Ufaransa, Russia, China pamoja na Ujerumani.

Monday, April 13, 2015

Majambazi wamuua sista, wapora fedha



Majambazi wamemuua kwa risasi Sista wa Kanisa Katoliki Clencensia Kapuli (50) na kupora kiasi kikubwa cha fedha ambacho hakijajulikana.
 
Wananchi wakiangalia sehemu ambayo majambazi walimpiga risasi Sista Clencensia Kapuli Ubungo, Riverside, Dar es Salaam jana. Picha na Michael Matemanga 

Pia, katika tukio hilo lililotokea jana saa nane mchana eneo la Riverside, Ubungo, Dar es Salaam, dereva aliyekuwa akimwendesha Sista Kapuli, Patrick Mwarabu alikatwa kidole gumba kwa risasi.

Sista Kapuli wa Shirika la Mtakatifu Maria wa Parokia ya Mwenyeheri Anwarite, Makoka Jijini Dar es Salaam alikuwa mhasibu wa parokia hiyo ambayo inamiliki Shule ya Sekondari Mwenyeheri Anwarite na Chuo cha Ufundi Stadi Makoka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura aliyefika katika Kituo cha Polisi Urafiki kufuatilia tukio hilo alisema Sista Kapuli na sista mwenzake wakiwa katika gari aina ya Toyota Hilux, walikuwa wakitoka Benki ya CRDB, Tawi la Mlimani City kuchukua fedha na walipita Riverside ndipo walipopatwa na mkasa huo.

“Bado hatujajua ni kiasi gani cha fedha kimechukuliwa kwa kuwa Sista Kapuli ndiye alikuwa mhasibu na ndiye aliyekwenda kuchukua fedha hizo, subirini tutakapokwenda benki kuuliza ni kiasi gani cha fedha alichukua na tutawajuza,” alisema Wambura.
Kamanda huyo alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ukisubiri taratibu za mazishi.


Israel yakataa uchunguzi wa mauaji ya vita vya Gaza



Utawala wa Kizayuni wa Israel umepinga kufanyika uchunguzi kuhusu mauaji ya Wapalestina yaliyofanywa na jeshi la utawala huo katika vita vya siku 50 dhidi ya Ukanda wa Gaza. 


Danny Eifruni, mwendesha mashtaka mkuu wa jeshi la utawala wa Kizayuni ameliambia gazeti la Kizayuni la Haretz kuwa wanapinga kufunguliwa faili la uchunguzi kuhusu mauaji ya raia wa Palestina yaliyofanywa na wanajeshi wa Israel katika vita vya siku 50 vya mwaka uliopita dhidi ya Ukanda wa Gaza. 

Katika vita hivyo vya mwezi Julai mwaka 2014, zaidi ya Wapalestina 2,300 waliuliwa shahidi na zaidi ya wengine elfu 11 walijeruhiwa, wengi miongoni mwao wakiwa ni wanawake na watoto.

Wakati huohuo harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imesisitiza kuwa muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni utaendelea, lengo likiwa ni kuzikomboa ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. 

Sheikh Bassam as Saadi, mmoja wa maafisa waandamizi wa harakati ya Jihadul Islami ametoa sisitizo hilo kufuatia kuuawa shahidi Wapalestina wawili katika shambulio la hapo jana la askari wa utawala haramu wa Israel huko Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan. 

Amesema, taifa la Palestina halitoiacha amana ya Jihadi na muqawama bali litaendeleza harakati na njia ya mashahidi…/