Saturday, May 18, 2019

Wajane watakiwa kuwa Wajasiliamali na kuchangamkia Fursa


Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akizungumza na Wajane takriban 350 wa kata ya Kigogo katika Futari ya pamoja  wakati wa kuadhimisha kumbukumbu ya Kifo cha Bi Khadija (a.s) Mke wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), iliyoandaliwa na Kitengo cha Kinamama wa Chuo cha Imam Swadiq (a.s), iliyofanyika Masjid Ghadir Kigogo Post Dar es salaam. 

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala amewataka Wajane kujishugulisha kwa kufanya Biashara mbalimbali za kujiletea maendeleo na kutokata tama ya maisha kwasababu wanae kiigizo ambaye ni Bi Khadija Mke wa Mtume Muhammad (s.a.w.w).

 “Kitendo cha Bibi Khadija (a.s) kujishughulisha kufanya Biashara, kuwa Mjasiliamali, kufanya harakati za uzalishaji ni dalili tosha na ni kiigizwa tosha cha kwamba Mwanamke Mjane, kumbe anaweza kuwa mjasiliamali, kumbe anaweza kujifanyia Biashara zake ndogondogo, na kuendesha Maisha yake na watoto alioachiwa na mwenzake” alisema Sheikh Jalala

Akizungumza Jana na Wajane takriban 350 wa kata ya Kigogo katika Futari ya pamoja  wakati wa kuadhimisha kumbukumbu ya Kifo cha Bi Khadija (a.s) Mke wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), iliyoandaliwa na Kitengo cha Kinamama wa Chuo cha Imam Swadiq, iliyofanyika Masjid Ghadir Kigogo Post Dar es salaam.

Aidha Sheikh Jalala amewataka Viongozi wa Dini kutumia Misikiti na Makanisa kuwa ni sehemu ya kuwakusanya wajane na Watanzania bila kujali dini zao kufanya hivyo ni kujenga Amani, Upendo, Umoja na Mshikamano, Misikiti na Makanisa isitumike kuwagawa Wajane na Watanzania.

“Leo hii wamekusanyika wajane pasina kubagua dini zao, wajane waislamu wako hapa, wajane wakristo wako hapa, ni somo nzuri na la kupendeza kwamba Misikiti yetu, Makanisa yetu yawe ni Sehemu ya kuwakusanya Waislamu, yawe ni sehemu ya kuwakusanya Wakristo na waka Misikiti yetu na Makanisa yetu yasiwe ni nyumba ya kuwagawa watanzania wetu” Alisisitiza Sheikh Jalala

Mkurugenzi wa Mtendaji wa Sadeline Heath Care Trust Mhe Sara Emmanuel  akizungumza na Wajane takriban 350 wa kata ya Kigogo katika Futari ya pamoja.
Nae Mkurugenzi wa Mtendaji wa Sadeline Heath Care Trust Mhe Sara Emmanuel amewataka Wajane kujiandisha na kuwa wanachama  kwenye Chama cha Wajane Tanzania (TAWIA) kwani  kuna fursa nyingi, ukishakuwa mwanachama kule Miradi mingi ambayo Serikali inatoa inapita kule na fursa nyingi zinapita kule” Alisema Sara Emmanuel

Mwenyekiti wa Chama cha Wajane Tanzania (TAWIA) Mhe. Mariam Aswile na wajane wenzake katika futari ya pamoja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wajane Tanzania (TAWIA) Mhe. Mariam Aswile amewatka wajane kutolala na kuhuzinika badala yake wamtumikie Mungu, kujitoa na kuchichangaya na wajane wenzie ili kutafuta fursa mbalimbali ambazo zitasaidia Ujane kuwa mwepesi katika maisha ya kila siku.

 “Napenda kusema kwamba, Wajane kama tumevyosikia somo la Ujasiliamali kwamba tusilale, tukakaa, tukaendelea kuhuzunika, ila tunapidi  kumtumikia Mungu, kujitoa na kujichanganya kama leo tumevyojichanganya mambo yetu yatakuwa ni Rahisi zaidi, hata huo Ujane utakuwa ni Mwepesi” Alisema Aswile.
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania (T.I.C) Sheikhat Fatma Mwiru (kulia) ambae pia ni Mwanaharakati Kitengo cha Kinamama cha Hawzat Imam Swadiq (a.s) akiwa katika Semina pamoja na futari ya Wajane kwa kumbukumbu ya Kifo cha Bi Khadija (a.s).

Afisa Mtendaji wa Kata ya Kigogo Mkwajuni Mhe. Raphael Mchomvu akiongea na Wajane (hawapo pichani ) katika futari ya pamoja ikiwa ni kumnukumbu ya Kifo cha Bi Khadija (a.s) Mke wa Mtume Muhammad (s.a.w.w),.

Sunday, April 21, 2019

Tunapokumbuka Mazazi ya Imam Mahdi (a.s), tunakumbuka Mambo 5 ya Utawala Bora | 20.04.2019 | Sheikh Jalala


                               
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala, akiongea na Waandishi wa Habari Jana Masjid Ghadir Kigogo Post Dar es salaam katika kutoa Salamu na Kheri za Shererehe na kumbukumbu ya mazazi ya Imam 12 ambae ni Imam Mahdi (a.s).
Bismillah Rahman Rahimu 

           Ndugu zangu Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu nyote.
Tunapokumbuka Mazazi ya Imam Mahdi (a.s), tunakumbuka Utawala Bora.
Napenda nianze kikao change hiki kwa maneno ya Mwenyezi Mungu (swt) yaliyopo katika Qur’an takatifu Suratul Raad aya ya 7, Mwenyezi Mungu anasema mwisho wa hii aya : “na hakika hapana vingine wewe Muhammad (s.a.w.w) ni mwenye kuhofisha na kila watu wanakiongozi wao”

Katika aya hii inakwenda sambamba na tukio la leo la mwezi 15 shabani siku ambayo waislamu duniani na hususan Waislam Shia Ithnasheriya wanasheherekea na kukumbuka mazazi ya kuzaliwa Imam wa 12 ambae ndie muokozi atakaekuja kuwaokoa na kuwaongoza walimwengu.

Katika tukio hili la kuzaliwa Imam wa 12 , kwanza napenda kutoa mkono wa hongera na Baraka na fanaka kwa waislamu wote duniani kwa mazazi ya Imam Mahdi (a.j.t.s), lakini pia napenda kutoa mkono wa heri fanaka na Baraka kwa watanzania wenzangu wote, pia kwa wanazuoni na maulamaa wote duniani na marajiin wetu hususani Kionngozi wa Vyuo vya Kidini Duniani Sayyid Sistani, pia natoa mkono wa Hongera na kheri iliyojaa fanaka kwa Kiongozi wetu na Naibu wa Imam wa 12, Kiongozi wa Waislam Duniani Imam Khamenei.

Katika tukio hili la kukumbuka kuzaliwa Imam wa 12 Imam Mahd (a.s) napenda kuzungumza yakwamba wamekubaliana waislamu wote yakwamba atadhihiri zama za mwisho Kiongozi anaeitwa Mahdi (a.s) na kwa hili wamekubaliana vilevile dini zote, Wakristo, Mayahudi, Mabudha na dini za Kimisri za zamani, kwamba Dunia haiwezi kumalizika lazima atakuja kudhihiri Mtu ambae ndie atakaeihakikishia duniani imekuwa mahala pa Amani, mahala pa Upendo na mahala pa mshikamano.

Kwahiyo itikadi ya kudhihiri muokozi hii ni itikadi ya dini zote, je muokozi huyo ni nani?, sisi waislamu tunasema muokozi huyo ni Imam Mahdi (a.s) na sisi Waislamu Shia Ithnasheriya btunasema kwamba ndio huyuhuyu aliezaliwa siku kama ya leo ya mwezi 15 shabani, ambayo tunaiitwa kwa lugha nyingine siku ya kugawa riziki ambayo waislamu wote hukesha Misikitini na kuomba dua maalumu.

Lakini kubwa lakuzungumzwa ni malengo ya Imam huyu,na jambo analotaka kulifanya ni jambo gani?.  Hadith zinasema bwana huyu atakapodhihiri ataijaza dunia uadilifu, ataijaza dunia haki, ataijaza dunia amani. Kwahivyo niseme yakwamba Imam Mahdi (a.s) atakapodhihiri atakachokileta ataleta Utawala Bora, atakacholeta ataleta Utawala anaostahiki mtawala au watawala wawe.

Utawala huo atakaokuja nao Imam Mahdi (a.s) atakuwa ni mtawala ambae dunia ameijaza uadilifu, ameitajaza amani, ameijaza haki. Katika utwala bora wa Imam Mahdi (a.s) ni utawala utakao kuwa vitu vitano vifuatavyo: 


Jambo la kwanza: Ubaguzi, Bwana huyu atakapodhihiri atapambana na kuondoa Ubaguzi, atapambana kuhakikisha ubaguzi haupo, nah ii ni moja katika siri ya Utawala Bora.Aina zote za Ubaguzi atazisambaratisha, Ubaguzi wa mweupe na mweusi kwake kutakuwa hakuna katika utawala wake kwamba mweupe ni bora mweusi si bora au mweusi ni bora mweupe sio bora hilo litakuwa hakuna.

Ubaguzi wa Ukabila, kabila fulani ndio kabila bora kabila fulani sio kabila bora kwenye utawala wake bora, ubaguzi huo hautakuwepo.kuwabagua watu kwa dini zao huyu ni mwislam, huyu ni mkristo, huyu ni Yahudi, ubaguzi huo utakuwa haupo.ataondoa ubaguzi hata ndani ya madhehebu hakutokuwepo huyu ni bohora, huyu ni Mwiithnasheriya, huyu ni Mwiismailia, huyu ni sunni, huyu ni Shia, huyu ni Ibaadhi, huyu ni shafii, huyu ni kadiria, aina hizo za ubaguzi kwenye utawala wake bora zitakuwa hazipo.

Kwahivyo leo tunapokumbuka mazazi ya Imam Mahdi (a.s) tunakumbuka Utawala Bora atakaouleta bwana huyo. Sihivyo tu Utawala wake hautakuwa na Ubaguzi wa Mitaa, wilaya na Mikoa kwamba kuna mkoa fulani ni bora zaidi, mkoa wa tanga ni bora, mkoa wa Dar es salaam ni Bora, mkoa wa Arusha ni bora mikoa mingine si bora, Taifa fulani ni bora, nchi fulani ni bora.kwake yeye la, ubaguzi wa hata wa aina hiyo wa kimaeneo kwake yeye haupo. Hii ni moja na siri ya Utawala bora, Utawala bora ni Utawala ambao unalenga maeneo yote katika kupeleka huduma na kuwaangalia watu.

Jambo la pili:Kuwatumikia watu, bwana huyu atakapodhihiri atahakikisha anawatumikia wanadamu,Mtume Muhammad (s.a.w.w) anasema bora ya Jambo ni kuwatumikia watu, Utawala wake utawatumikia watu kwa kila mambo muhimu, huduma za kijamii, kama vile huduma ya elimu itakuwa kwa watu wote, haitobagua watu.

Utawala wake ni utawala hautokuwa na wajinga,ni Utawala wa kuhakikisha unafuta ujinga,ni Utawala ambao watu wake watakuwa na masomo yao ya mwanzo mpaka masomo ya juu, kupatikana Profesa, Injinia, watu wenye PHD katika jamii yake ni kitu cha kawaida nah ii ndio siri ya Utawala bora. Babu yake Imam Mahdi (a.s) ambae ni Mtume Muhammad (s.a.w.w) anasema anaetaka dunia lazima awe na elimu, na anaetaka akhera lazima awe na elimu.

Katika utawala wake Tiba itaboreshwa kwa hali ya juu, maji salama na safi ndio watakao kunywa wanadamu, maisha yatakuwa mazuri kwa watu, nah ii ndio siri ya Utawala bora.Mtawala bora ni Yule anaejali watu wake, ni Yule anaetaka huduma ziwafikie wanadamu wote na watu wake wote, hivyo ndivyo atakavyokuwa Imam Mahdi (a.s).

Jambo la tatu:Mivutano, bwana huyu atakapodhihiri atahakikisha kwamba anaondoa mivutano iliyopo kwa walimwengu wote na hiyo ndio sifa ya Utawala bora, Utawala bota ni ule utawala ambao unahakikisha hauna mivutano, ni utawala wenye maelewano.ataondoa mivutano ndani ya Jamii, ndani ya Taasisi, ndani ya nyumba za ibada,zitakuwa hazina mivutano, ataelekeza watu wapendane, watu washikamane na wamtumukie mungu mmoja, wasitumikie waungu wengi ambao ndio sababu ya mivutano tulionayo katika jamii yetu.

Jambo la nne:Ufisadi, bwana huyu atakapodhihiri atahakikisha anaondoa ufisadi, Ufisadi katika Nyanja zote na ufisadi wa waina yoyote,.Yeye atapambana na Ufisadi, atahakikisha Rushwa hailiwi katika jamii yake, na kataika utawala wake, na ndio maana tukauita utawala wa Imam Mahd (a.s) ni Utawala bora, Rushwa itakuwa ni Marufuku, Mikataba feti kwake itakuwa hakuna.

Wafanyakazi hewa katika Utawala wake kutakuwa hakuna, hakutokuwa na matengenezo ya ujanja ujanja kitu kimetengenezwa kwa kitu kidogo lakini mahesabu ni mengi, hapana, Ubabaishaji huo katika Utawala wake kutakuwa hakuna kwa sababu, watu wanamtambua Mungu, watu wanamuelewa Mungu, Utawala wake ni Utawala unaolinda mali za Umma, unaolinda mali za Watu.

Jambo la tano : Amani, na la mwisho atahakikisha amani inatawala kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji, tarafa , Kata, wilaya, Mkoa, Taifa na dunia yote itakuwa ni mahala pa utulivu na amani. Katika Utawala wa Imam Mahdi (a.s) Amani itakuwa inachukua nafasi ya kwanza,riwaya zinatuambia yakwamba katika Utawala wa Imam Mahdi (a.s) katika Utawala wake Bora utakuwa Mtu unatembea masaa 24 hakuna mtu atakaekunyanganya kidani chako cha dhahabu, mama hawezi kunyanganywa herein yake alievaa hata usiku wa manane.

Kwahiyo atahakikisha amani imeboreka kwa ngazi zote na kwa dunia, Amani kwa mtu mmoja mmoja, amani kwa upande wa Familia, amani kwa upande wa jamii, amani kwa mji mzima, amani kwa mabara yetu na amani kwa dunia nzima, itakuwa ni wakati ambao Amani imetanda , upendo umetawala, watu wanamtambua mungu mmoja, wanamuabudu mungu mmoja, hivi ndivyo utakavyokuwa utawala wa Imam Mahdi (a.s).

Hayo ni mambo matano Imam Mahdi (a.s) atakapodhihiri atapambana nayo na kuhakikisha yanatawala, na ndio maana tukasema Utawala wale ni Utawala bora, Kwahivyo katika siku hii tunayokumbuka mazazi ya Imam Mahdi (a.s) ni siku ya kukumbuka na kujifunza utawala bora,Utawala wa Imam Mahdi (a.s) ambapo utawala huo utakapokuwepo mahali popote, basi mahali hapo itakuwa ni pepo na mahali hapo.

Asanteni sana, namuomba Mwenyezi Mungu (swt) kwa Baraka ya Kuzaliwa Imam Mahdi (a.s), Mwenyezi Mungu atupe nguvu za kuweza kuienzi amani, maelewano mazuri, Tanzania iendelee kubakia kisiwa cha amani, mahala pa watu wanaopendana, mahala panapokimbiliwa na watu, kwasababu ya hali yake nzuri ya hewa lakini kwasababu ya watu wake wanavyowapenda watu,na kwasababu ya watu wake wanavyopenda amani, asanteni sana na Mungu awabariki.

Imetolewa na:
Maulana Sheikh Hemed Jalala
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania
Tare:Jumamosi, 20.04.2019 Sawa na 14 Shaban 1440.

Wednesday, April 3, 2019

Siku ya Israa na Miiraj ni siku ya kuwafunza Watanzania Elimu,Maadili Mema, Umoja wa Dini zote na kuenzi Amani-Sheikh Jalala


                                           
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akiongea na Waandishi wa Habari katika unasheherekea kwa shangwe na furaha kubwa tukio la Israa na Miiraj, tukio la Mtume Muhammad (s.a.w.w) kupelekwa usiku kutoka Makka mpaka Masjid al Aqswa ulioko Jurusalem nchini Palestina, na baada ya hapo msafara wa kutoka Masjid al Aqswa kwenda Mbungu za juu, jana Masjid Ghadir Kigogo Post Dar es salaam.
                            Bismillah Rahmani Rahimu
                         Ndugu zangu Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kweny nyote                                      

Siku ya Israa na Miiraj ni siku ya kuwafunza Watanzania Elimu,Maadili Mema, Umoja wa Dini zote na kuenzi Amani.

“SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona” 17. SURA AL ISRAAI,aya ya 1.

Siku hii ya leo tunasheherekea kwa shangwe na furaha kubwa matukio mawili makubwa, tukio la kwanza ni tukio la Israa na Miiraj, tukio la Mtume Muhammad (s.a.w.w) kupelekwa usiku kutoka Makka mpaka Masjid al Aqswa ulioko Jurusalem nchini Palestina, na baada ya hapo msafara wa kutoka Masjid al Aqswa kwenda Mbungu za juu.

Na tukio la pili ni tukio la Mtume Muhammad (s.a.w.w) kukabidhiwa Utume na kupelekwa kama Mtume kwa walimwengu wote, matukio haya mawili, kwanza kwa matukio haya mawili na kwa sherehe hizi mbili, napenda kutoa Salamu zangu za dhati kwa Viongozi wa Dini wote, na kwa Marajii wetu wote wakubwa akiwemo Ayatullah Sayyid Sistan.

Lakini vilevile natoa salamu katika siku hii ya leo ya Israa, Miiraj na Siku ya Biidha kwa Kiongozi wa Umma wa Kiislamu Duniani Imam Khamenei,Mwenyezi Mungu amuhafidhi na ambakishe, lakini vile vile natoa salamu zangu za dhati na hongra na pongezi zangu kwa Imam wa Zama hizi Imam wa 12 Imam al Mahd (a.j.t.s).Tukio la Israa, Miiraj na Biidhaa lina tafsi nyingi na lina ishara nyingi, lakini nitapenda kusema tukio hili linaweza kutupa ishara 5 Muhimu.

Ishara ya Kwanza: ni ishara ya Umuhimu wa Elimu, tukio la Mtume Muhammad (s.a.w.w) la kutoka Makka na kupelekwa Jerusalem nchini Palestina kwenye msikiti mtakatifu  wa al Aqswa ni tukio la kielimu, ni tukio la kisayansi, ni tukio la kiteknolojia. Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuondoka Masjid al Aqswa kwenda kwenye sayari za juu, ni ishara ya Elimu, ni ishara ya Sayansi,ni ishara ya Teknolojia.

Na mwenyezi Mungu amelizungumza katika Qur’an “Kama mnaweza kwenda katika sayari za juu, basi mnaweza kwenda lakini huko kunahitajia Elimu”. Tukio la Mtume Muhammad (s.a.w.w) kukabidhiwa Utume kwa neon “Soma” ni dalili ya elimu, kwa hivyo tukio la Israa na Miiraj moja ya funzo yake muhimu ni funzo ya elimu. Kwa kuwa Israa na Miiraj na kwa kuwa Bi’idha, kupelekwa ni funzo la elimu ni nafasi yetu na ni muda wetu kutilia umuhimu jambo la Elimu.

Sisi kama Watanzania, sisi kama Waislamu lazima kuhakikisha watoto wetu wanasoma, watoto wetu wanakwenda Shuleni, watoto wetu wanakwenda Vyuo, watoto wetu wanakwenda Madrasa, wanakwenda kujisomea kuhakikisha wanakuwa na elimu. Ilakuwa ni kuwadhulumu haki zao kufikia kwamba kutakuwa na watoto wa kitanzania ambao hawapelekwi Shuleni.

 Hawaendi kusoma au wako majumbani kwasababu yoyote itakayopatikana, imefikia muda kwa sisi kama waislamu na kama watanzania kuhakikisha watoto wetu wote wanakwenda masomoni pasina kuwabagua  wawe watoto wa kiume wawe watoto wa kike kwasababu wote wanahaki ya elimu.

Ishara ya pili: ni ishara ya Umuhimu wa Akida, katika ishara ya za tukio la Israa na Miiraj pamoja na Bi’idha ni akida, tendo la Mtume Muhammad (s.a.w.w) kutoka Makka msikitini na kufikizia Masjid al Aqwa hii ni ishara ya kwamba msikiti mtakatifu wa Masjid al Aqswa ulioko Juerusalem ni msikiti wa Waislamu, ni mali ya Waislamu na ni haki ya Waislamu, nan i Lazima (Wajibu) kwa waislamu kuutaka Msikiti wao, kuunadi Msikiti wao,kuhakikisha ya kwamba msikiti wao upo katika mahali pa amani, kuhakikisha msikiti wao huu unabakia kumbukumbu yao hii inabakia, Masjid Aqswa msikiti ambao Mtume Muhammad (s.a.w.w) ndie alievikizia baada ya kutoka msikiti wa Makka.

hii ni ishara kubwa ya kwamba msikiti huu hauna tofauti na msikiti wa Makka, na kwamba utukufu baada ya Msikiti wa Makka unafuatia msikiti wa al Aqswa. Kwa hivyo katika fursa hii tunachukua nafasi kuwaeleza maimam wa Misikiti, kuwaeleza Masheikh kwamba imefikia muda wa kuwaeleza waumuni wao ni upi msikiti mtakatifu, msikiti mtakatifu ni mali ya nani? Na ni sehemu ya nani katika ardhi ile ambao upo msikiti mtakatifu.

Ishara ya tatu: ni ishara ya maadili mema, Msafara wa Israa na Miiraj pamoja na Bi’idha ni msafara unaotupa funzo la Maadili, msafara unaotupa funzo la maadili mazuri, tendo la mtume Muhammad (s.a.w.w) tendo la kuingia peponi, tendo la mtume Muhammad (s.a.w.w) kuwaangalia moto na adhabu zilizopo ndani ya moto na kubainisha Mtume Muhammad (s.a.w.w) ya kwamba watu walioko mototni ni watu wa aina gani.

Na kwanini walikuwepo ndani ya moto? Na kwanini ipo pepo?, kwanini Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikutana na baadhi ya mambo njiani, alikutana na Maidhriti na akapewa maneno ya kuyasoma, alikutana na watu wabaya lakini akapewa kinga ya kujikinga na watu wabaya, alipewa vinywaji akachagua kinywaji kizuri, kwanini haya yote? Haya yote ni kufunza maadili mema, siku ya Israa na Miiraj iwe ni siku ya kuwafunza watanzania  ya kuwaelekeza watanzania maadili mema, maadili mazuri, imefikia muda kuachana na kila jambo ambalo ni maadili mabaya, si mila za watanzania, si mila za waafrika, si mambo yao, na haya maadili leo ni mengi ambayo ni changamoto kubwa inayoikabili taifa na inayowakabili watanzania kwa ujumla.

Ishara ya nne: ni ishara ya Umoja wa dini zote, tukio la Israa na Miiraj pamoja na Bi’idha tunajifunza funzo la Umoja wa dini zote, Mtume Muhammad (s.a.w.w) baada ya kufika Masjid al Aqswa aliweza kuswali na Mitume wote (a.s) nay eye akatangulia mbele akawaswalisha , Mitume wote waliotumwa na Mungu 124,000 walikusanyika pale, wakaswali pamoja na Mtume Muhammad (s.a.w.w), wakaswali swala moja, wakaomba maombi mamoja,wakakaa kikao kimoja, wakatanguliwa na mtu mmoja.

Hii ni ishara na ni mafunzo ya kwamba Mitume (a.s) wote waliotumwa na Mungu, wote ujumbe wao ni mmoja, mafunzo yao ni mamoja, maelekezo yao ni mamoja. Kwahivyo yeyote hapa Tanzania, yoyote hapa Afrika, yoyote hapa Duniani atakae kuja na dini yake akafunza kinyume na umoja, akafunza kinyume na mshikamano, akafunza kinyume na Upendo, huyo amekwenda kinyume mafunzo ya Mitume (a.s) wote, na maimam wote, Vitabu vyote, na watu waliokusanyika pale katika msikiti mtakatifu wa al Aqswa na wakamuomba Mwenyezi Mungu na wakaswali swala moja wakiongozwa ni Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Ishara ya tano: ni ishara ya Umuhumu wa kuenzi Amani na maelewano,Nukta ya tano nay a Mwisho kitendo cha msafara wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuondoka mahala panapoitwa Masjid Harraam yaani Msikiti mtakatifu, nini maana ya msikiti mtakatifu? Msikiti mtakatifu maana yeke ni msikiti ambao huruhusiwi kumwaga damu, hauruhusiwi vita, hauruhusiwi mapambano, msafara ukaanzia katika msikiti huo moja kwa moja ukaja msikiti wa pili  Masjid al Aqswa, hii ni ishara ya nini? Ni ishara ya kwamba kilichopo Masjid Haraam ndio kilichopo Masjid al Aqswa,kama ulivyokuwa Masjid al Haraam Hairuhusiwi Vita,  hauruhusiwi kumwaga damu, hairuhusiwi mapambano.

Hivyo hivyo Masjid Aqswa hairuhusiwi vita vyoyote, hairuhusiwi kumwaga damu, hairuhusiwi mapambano yoyote, kama ilivyokuwa Al kaaba ni mahala pa kuenziwa amani, hivyohivyo masjid al Aqswa ni mahala pa kuenziwa amani,kama ilivyokuwa msafara uliondoka uliondoka kwenye msikiti na ukafikizia kwenye msikiti, msikiti ni mahala pa amani, msikiti ni mahala pa upendo, msikiti ni mahala pa kutokumwaga damu.

Tuko dhidi ya yoyote ambae anamwaga damu katika msikiti iwe ni masjid Haraam iwe ni Masjid al Aqswa, tuko dhidi ya yoyote ambae anatumia nguvu zake kumwaga damu, iwe ni msikiti ulioko Makka au ni Msikiti ulioko Jerusalem, yoyote ambae anavunja amani ya sehemu hizi mbili huyo sisi tuko dhidi yake na hatuko nae na yuko dhidi ya  amani ya dunia,yupo dhidi ya Upendo wa Dunia. Kwa hivyo msafara wa Israa, Miiraj na Bi’idha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni msafara wa unaofunza amani, ni msafara wa kuenzi amani, ni msafara wa kusomesha upendo na maelewano.

Mwisho: Ujumbe wetu katika siku hii ya Israa na Miiraj pamoja na Bi’idha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), ujumbe wetu mkubwa tunaouelekeza kwa watanzania ni Ujumbe wa umuhimu wa Elimu, kimefika kipindi ya kwamba itakuwa ni kosa la jinai watoto kubakia majumbani pasina kupelekwa Shuleni, hususani katika kipindi hiki ambacho  Elimu imekuwa ni Elimu ya Bure, nafasi za Shuleni zimekuwa nafasi pana, ujumbe mkubwa ni kuhakikisha watoto wetu wanasoma, kama tunataka maendeleo ya familia zetu lazima watoto wetu wasome, kama tunataka maendeleo ya taifa letu lazima watoto wetu wasome, kama tunaitaka dunia basi watoto wetu wasome, kama tunataka akhera watoto wetu wasome.

Mwenyezi Mungu nakuomba kwasababu ya tukio la Israa na Miiraj pamoja na Bi’idha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) Taifa hili ulipe amani, taifa hili ulipe utulivu, yoyote mwenyekuitakia matatizo na migogoro Tanzania , Mwenyezi Mungu huyo asiweze kufanikiwa.

Mwenyezi Mungu endelea kubakiza Upendo na Mshikamano kwa watanzania wote, endelea kuifanya Tanzania ni kisiwa na amani ni mahala pa watu wanakaa vizuri,na Mshikamano watu wasioelewa Vita wala kugombana , Asanteni sana, Miiraj njema, Israa njema na Bi’idha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) njema. Ndugu zangu Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kweny nyote.

Imetolewa na 
Maulana Sheikh Hemed Jalala
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania
Tare: Jumanne 02.04.2019 sawa na 26 Rajab 1440
Masjid Ghadir, Kigogo Dar es salaam

Thursday, March 21, 2019

Siku ya Baba Duniani kwa Kuzaliwa Imam Ali Ibn Abutwalib (a.s) | Maulana Sheikh Jalala

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akiongea na Waandishi wa Habari katika kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Ali (a.s) ambayo ndio siku ya Baba Duniani, kikao hicho kilifanya Jana Masjid Ghadir Kigogo Post Dar es salaam.

Bislamillah Rahmani Rahim
Ndugu zangu Waandishi na Watanzania Wenzangu
Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu Nyote.

Siku ya Baba Duniani kwa Kuzaliwa Imam Ali Ibn Abutwalib (a.s).

Siku hii ya leo ambayo kwa tarehe ya Kiislamu ni sawa na Tarehe 13 mwezi wa Rajab mwaka wa 1440, ambao ni sa /\wasawa na terehe 20, mwezi wa 3 mwaka 600 AD.Mwaka huo unakumbana na siku hii ya leo ambayo waislamu duniani, hususan Shia Ithnasheriya tunakumbuka siku ya kuzaliwa Imam au Kiongozi Ali (a.s) ambae ni Imam wa Kwanza na Kiongozi wa Kwanza baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuondoka duniani.

Mazazi ya Imam Ali (a.s) au Kiuongozi Ali (a.s) baada ya Mtume (s.a.w.w) ni muhimu kukumbukwa kwa mambo yafuatayo:

Jambo la kwanza, napenda tutambue huyu tunaemzungumza mahali alipozaliwa , alizaliwa ndani ya al kaaba, yaani kwa ibara nyingine nzuri ndani ya ile nyumba ambayo waislam wote duniani wanapofanya ibada zao iwe ni dua iwe ni swala, iwe ni ibada nyingine yoyote wanaelekea pale mahala panapoitwa al kaaba, pale ndipo alipozaliwa  muheshimiwa huyu anaeitwa Imam Ali (a.s).

Kitendo cha kuzaliwa mahala pale kinatupa sisi tutafakari baadhi ya mambo, kwanini amezaliwa pale?, nitazungumza nukta tano za yeye kuzaliwa pale.Nukta ya kwanza alizaliwa pale ambapo ni mahala pa Ibada ili iwe ni darasa kwetu sisi walimwengu, kwetu sisi wanadamu, kitu kinachoitwa Umuhimu wa Ibada, mahala pale alipozaliwa Imam Ali (a.s) ni mahala ambapo aliejenga mahala pale ni Nabii Ibrahimu (a.s).

Nabii Ibrahimu tunavyomuita sisi waislamu, tunamwita ni baba wa dini zote kwasababu Nabii Ibrahimu (a.s) ndio alimzaa Nabii Ismail (a.s) na Nabii Islamail ndicho kizazi cha Mtume Muhammad (s.aw.w), Nabii Ibrahimu ndio aliemzaa Nabii Isshaq/Isaka (a.s),Isaka ndio aliemzaa Nabii Yakub (a.s), Nabii Yakub (a.s) ndie alieitwa Israel kwahiyo ndio aliezaa Mitume wote wa Israel yaani Nabii Mussa (a.s), Nabii Issa / Yesu Kristo (a.s) na wengineo wote.

Kwahivyo alieijenga al kaaba ni Baba wa dini zote mahali hapo ndipo alizaliwa Imam Ali (a.s), Imam wa Kwanza baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ikiwa ni ishara ya umuhimu wa wanadamu wote kumuabudu mungu, binadamu wote kumtii Mungu, binadamu wote kumsikiliza Mungu, mara kwa mara nilikuwa nikisema Ibada sio kuswali tu, bali mwenyewe Mtume Muhammad (s.a.w.w) anatuambia ya kwamba ibada kubwa zaidi ni kumtumikia mwanadamu.

 kwa hivyo yoyote anaemtumikia mjane amefanya ibada kubwa sana, yeyote anaemjali yatima amefanya ibada kubwa sana, yeyote anaewajali watu wanaoishi katika mzingira magumu amefanya ibada kubwa sana, hayo yote hayafungamani na dini yoyote bali ni mbali yanayohusiana na dini zote za mbinguni.Siku hii ya kuzaliwa Imam Ali (a.s) Imam wa kwanza ni siku ya kuenzi Ibada, na bora ya Ibadan i kumtumikia mwanadamu.

Jambo la pili: ya kuzaliwa Imam Ali (a.s) ndani ya al kaaba linatupa darasa moja muhimu sana, linatupa darasa la umhimu wa kazi, Sayyidina Ali (a.s) Imam Ali (a.s) katika historia yake ikimsoma ni mtu alikuwa halali, ni mtu alikuwa mchapa kazi, ni mtu aliekuwa masaa 24 akifanya kazi, kwasababu alikuwa akiamini, mungu anatutaka tufanye kazi.

Na nabii Ibrahimu (a.s) baba wa dini zote alifanya kazi yeye na Nabii ismail,wakaijenga al kaaba wakaitengeneza ibada ya hijja, ambayo ibada yenyewe ni kazi, kwahivyo tendo la kuzaliwa Sayyidina Ali (a.s) au Imam Ali (a.s) tunakumbuka kuzaliwa kwake ndani ya al kaaba, moja ya darasa muhimu kwa sisi watanzania wote pasina kubagua dini zetu ni funzo la kufanya kazi, na kwamba kufanya kazi ndio kutatufanya tufikie mahala panapoitwa mahala muhimu na mahala pakubwa.

Jambo la tatu:Kitendo cha kuzaliwa Sayyidina Ali (a.s) kuzaliwa katika nyumba kubwa na nyumba muhimu, nyumba ya kwanza kuwekwa duniani, nyumba inayofunza uadilifu ni nyumba inayoitwa nyumba ya Mungu tunasoma darasa la Umuhimu wa Uadilifu, na ndio maana yeye mwenyewe Sayyidina Ali (a.s) ameitwa nani?, yeye mwenyewe ameitwa kwamba ni sauti ya uadilifu.

katika vitu alivyopigana navyo alipigana navyo Uadilifu,alipigana kuhakikisha watu wote wanapata haki zao, watu wote ni sawa, hakuna tabaka fulani hilo ni bora kuliko tabaka linguine, hakuna akina fulani wao wanahaki zaidi kuliko wengine, Kitendo cha Kuzaliwa Ali (a.s) ndani ya al kaaba nyumba ya Uadilifu ni dalili ya kwamba Sayyidina Ali (a.s) ni mwalimu wa waadilifu na kwamba sisi katika siku hii ya leo siku ya mazazi ya Imam Ali (a.s) tuuwenzi uadilifu na kuukumbuka uadilifu, na kwamba kubakia kwetu, kustawi kwetu ni kwasababu ya Uadilifu tutakao ufanya hapa duniani.

Jambo la nne: la muhimu la kuzungumzwa la kuzaliwa Sayyidina Ali (a.s) ndani ya al kaaba tunapata darasa gani? Tunapata darasa la Umoja, al kaaba nyumba ya kwanza iliyojengwa kumuabudu maungu, baada yake ndio ikajengwa nyumba ya Jerusalem, al kaaba iliyojengwa na Nabii Ibrahimu (a.s) baba wa dini zote, baba wa waislamu, baba wa wakristo, baba wa mayahudi ndie mjenzi wa nyumba ile.

 Kitendo cha kuzaliwa Sayyidina Ali (a.s) pale ndani ni darasa moja muhimu, darasa kwamba Imam Ali (a.s) ni bingwa wa kutengeneza Umoja, ni bingwa wa kuzifanya dini zote hizi zikae mahala pamoja, nakwamba tukae tukifikiria na tukae tukitambua ya kwamba waislamu, mayahudi, wakristo hawa wote baba yao ni mmoja.

Nae ni Yule mjenzi wa al kaaba na Yule mjenzi wa mahala pale patakatifu mahala pale ndipo alipozaliwa Imam wa kwanza wa waislamu Sayyidina Ali (a.s) au Khalifa wanne anavyojulikana kwa waislamu wengine. kwahivyo ni somo muhimu, ni somo kubwa la kuenzi umoja wetu wa wawatanzania, umoja wetu wa wanadini,waislam, wakristo na mayahudi, ndani ya ardhi yetu ya Tanzania.

Jambo la tano: Al kaaba mwenyezi mungu anasema ndani ya Quran “yoyote mwenyekufika al kaaba, amefika mahala pa amani” kwahivyo mungu ameweka nyumba maalumu akaiita ni nyumba ya kuenziwa amani, Sayyidina Ali (a.s) alizaliwa katika nyumba hiyo, amezaliwa katika nyumba ya kuienzi amani.

Hii ni ishara na ni dalili ya kwamba moja katika mambo muhimu ya kufanywa kukumbuka mazazi ya Imam Ali (a.s) Kiongozi huyu baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni kuenzi amani, ni kuenzi utulivu, ni kuenzi mshikamano, ni kuenzi upendo kati ya watanzania kama watanzania, kati ya waafrika kama waafrika,lakini vilevile kati ya wanadunia na kati ya wanaulimwengu wote.

Na kwamba nyumba ya kwanza iliyojengwa na nabii Ibrahimu (a.s) baba wa dini zote, baba wa wakristo, baba wa waislamu,baba wa mayahudi na akaziliwa Imam Ali (a.s) Kiongozi wa Waislamu ni dalili ya kwamba jambo la amani ndio jambo ambalo limeasisiwa mahala pako mpaka leo tunapaona watu wa dini zote, na kwa tukio hili napenda nigusie ya kwamba hii inaonyesha ya kwamba waislamu, si katika nadharia ya Uislamu, wala si katika nadharia ya kiyahudi, wala si katika nadharia ya wakristo kitu kinachoitwa kuvunja amani, kitu kinachoitwa Ugaidi, kitu kinachoitwa kutumia nguvu.

Kulaani: Kwa tukio hili la kuzaliwa Imam Ali (a.s) tunatoa msimamo wetu na tunatoa kauli yetu ya dhati kabisa ya kulaani kitendo cha kigaidi kilichofanyika katika nchi ya Newsland kilichopelekea mauaji ya waislamu wasiopungua takriban watu 50 ndani ya Msikitini, tumesema ni kitendo cha kigaidi, na hii ni dalili ya kwamba  ugaidi hauna dini, hauna Ukristo, hauna Uyahudi wala hauna Uislamu, na sisi tupo pamoja na yeyote ambae anaenzi watu wakae vizuri, anaenzi watu wake kwa upendo na watu wakae kwa usalama.

Wito: wito wetu katika siku hii ya kuzaliwa Imam Ali (a.s) au Kiongozi au Imam wa kwanza wa waislamu baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), wito wetu kwanza kwa viongozi wa dini waislamu na wakristo nchini, tunatoa wito wa kuwa wawe Viongozi wa dini na nia ya dhati ya kujenga umoja,mshikamano, ushirikiano na upendo kati yao kama alivyokuwa Sayyidina Ali (a.s), Imam Ali (a.s) katika Utawala wake moja ya mambo muhimu ukimsoma aliyoyajenga ilikuwa ni maelewano, upendo na mshikamano kati yao wao wenyewe kama viongozi wa dini.

Na hayo yatafikiwa na Viongozi wa dini kuwa na mambo yafuatayo, kwa ibara nyingine nzuri Viongozi wa dini watafikia mahala mahala wanamshikamano, wanaupendo, ushirikiano na umoja watakapokuwa na mambo matatu muhimu yakuyafanya, jambo la kwanza, wawe na tabia ya kutembeleana, jambo la pili wawe ya kukaa pamoja,jambo la tatu wawe na tabia kupeana zawadi, kwenye Krismasi, kwenye Eid, kwenye Maulid na matukio mengine.

Wito wetu wa pili, ili watanzania waishi kwa amani,kwa utulivu, kwa Upendo na kwa umoja lazima tuishi kama mitume wa mungu walivyoelekeza na kama Maimam , Viongozi akiwemo Sayyidina Ali (a.s) walivyoelekeza, lakini vilevile kama vitabu vya mbinguni Taurati, Injili, Zaburi na Qur’an vilivyoelekeza, vitabu vyote hivyo vimeelekeza Upendo,Mshikamano, Umoja na watu kukaa Vizuri.

Mwisho: Mwenyezi Mungu nakuomba katika siku hii ya kuzaliwa Imam Ali (a.s) Imam wa Kwanza baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), au Khalifa wan ne waislamu wengine, Mwenyezi Mungu nakuomba Tanzania uipe amani, Tanzania uipe Utulivu, Viongozi wetu Mwenyezi Mungu uendelee kuwapa Hekima,uwape busara, uwape muono wao wa kuwatumikia watanzania mpaka mwisho wa masiku yao.

Na sisi kama watanzania tuwe na tabia ya kuombea Mungu Viongozi wetu ili waweze kutuongoza katika njia iliyokuwa ya kisawasawa. Mungu aibariki Tanzania, Mungu awabariki Viongozi wetu wote tuliokuwanao wanaotuongoza, Asanteni sana Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu nyote.

Imetolewa na: 
Maulana Sheikh Hemed Jalala
Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania
Tare:20.03.2019/13 Mwezi wa Rajab, 1440.
Masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es salaam.


Wednesday, February 27, 2019

Kuzaliwa Fatma Bint Muhammad (a.s) ndio siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani-Maulana Sheikh Jalala.

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala (kushoto) akiongea na Waandishi wa Habari katika kukumbuka kuzaliwa kwa Mtoto wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Bi Fatma bint Muhammad (a.s), kuwa ndio Siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani, Jana Masjid Ghadir, Kigogo Post Jijini Dar es salaam

Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu Nyote.
Siku hii ya leo ambayo kwa tarekh ya Kiislamu tunaita ni Mwezi 9,ni siku ambayo wanazuoni wa Kiislamu wameitangaza kuwa ni Siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani, sababu kubwa ya Tangazo hilo nikutokana na kuzaliwa Bint ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambae Bint huyu na Mama huyu na dada huyu ananafasi kubwa katika Dini ya Uislamu.

Mama huyu ambae tunakumbuka mazazi yake ambae Maulamaa wameitangaza kuwa ni siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani daraja lake mama huyu katika Uislamu ni kama vile daraja la Maryam bint Imran, Mama yake Nabii Issa (a.s). Lakini kwanini kukumbukwa mama huyu lakini vilevile kwani kutangzwa ni siku ya Mwanake wa Kiislamu Duniani.

 Sababu kubwa ni daraja la mwanamke na nafasi ya mwanamke katika jamii na katika Uislamu.Uislamu unamuangalia Mwanamke katika mambo yafuatayo, kwanza Uislamu unamuangalia Mwanamke kwamba ni mwanadamu wa Kawaida kama vile Mwanamume.kwa ibara nyingine nzuri Uislamu hautofautishi kati ya jinsia ya Kiume na jinsia ya Kike.

Na tunaamini kakika Uislamu ya kwamba jinsia hizi mbili zote zipo sawasawa, jinsia ya Kike na Jinsia ya Kiume. Kwahiyo siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani ni siku ya kufuta maneno yanayowezwa kusemwa ya kwamba mwanamume ni bora kuliko mwanamke, hapana ni jinsia mbili ambazo zipo sawasawa kama ni mapungufu basi yapo kwa wanaume na yapo vilevile kwa wanawake.

Jambo la pili ni jambo la haki, mwanamume anahaki kwenye mambo mengi na mambo kadhaa haki hizo vilevile zipo kwa mwanamke, kwa mfano mwanamke anayohaki ya kufanya kazi? Je katika Uislamu mwanamke anayohaki  ya kufanya kazi? Jawabu ndio. Haki hiyo vilevile anayo mwanamke katika Uislamu.

Mwanamume anayohaki ya kuendesha gari, Je mwanamke anaruhusiwa kuendesha gari? Ndio mwanamke vilevile anayohaki ya kuendesha gari katika uislamu. Mwanamume anayohaki ya Elimu, mwanamume anayohaki ya Kusoma mpaka kufikia ngazi za juu, je haki hiyo mwanamke anayo katika uislamu? Ndio mwanamke vilevile anayohaki ya kusoma na kusomeshwa mpaka ngazi za juu.

Katika siku hii ya kumkumbuka mwanamke duniani, katika sikun hii ya kumkumbuka mwanamke wa Kiislamu Duniani moja ya jambo la kuliangazia ni jambo la Elimu ya kwamba wazazi watambue kama walivyokuwa na haki kumsomesha kijana wa kiume na mototo wa kiume vilevile ni haki yao kumsomesha binti wa kike na kijana wa kike na kumsomesha hakuna kiziwizi maalumu ikiwa na maana asomeshwa mpaka ngazi Fulani kasha basi.

Kulikuwa na fikra ambazo zinapatikana kwenye baadhi ya maandiko ambayo maandiko hayo tunayasema ni maandiko ya Kimakosa kwa mfano kuna baadhi ya fikra zinaona Mwanamke ndie aliefanya makosa alipokuwa kule Peponi na ikawa ndio sababu ya kufukuzwa adam na hawa kwamba sababu ilikuwa ni mwanamke.

 Hapana dini ya Uislamu inaangalia yakwamba makosa yaliyofanya ndani ya pepo hayana mahusiano na Mwanamke na kwamba mwanamke ni kiumbe kama vile viumbe wengine wa kawaida. Mwanamume anayokarama anayoheshima, je heshima hii ipo kwa mwanamke?

Mwenyezi Mungu ndani ya Quran anaitaja waziwazi hawa wanaadamu wote wanakarma wanaheshima, kama vilevile mwanamume anatakikana aheshimiwe na vilevile mwanamke anatakikana aheshimiwe, kama vile mwanamume anadaraja kubwa mbele za mwenyezi Mungu kwasababu ni kumbe ambacho kinaroho ya Mungu, daraja hili vilevile analo mwanamke kwasababu nae ni kumbe cha mwenyezi Mungu.

Tunapojaribu kuisoma Quran na kuiangalia Quran iliyowazungumza wanawake na daraja iliyowapa, tutaona ya kwamba daraja hilo halina tofauti na daraja la mwanaume, kwa mfano Quran imewataja wanawake ambao ni wanawake watakatifu kama ilivyowataja wanaume, Quran imemtaja Maryam (a.s) ambae ni mama yake Nabii Issa (a.s) yakwamba ni mwanamke mtakatifu.

Kama ambavyo imemtaja Fatma Zahraa (a.s) ambae leo tunakumbuka mazazi yake katika aya tofauti, kama ambavyo imemtaja mlezi wa Nabii Mussa (a.s) au Mke wa Firaun, Quran imemtaja mwanamke kwa kiwango hicho na kwa daraja hilo na kwa heshima hiyo kama vile ambavyo imemtaja mwanaume kwa heshima na kwa daraja tofauti alilokuwanalo.

 Je, mwanamke anamiliki? Katika Uislamu, mwanamke anayohaki ya kufanya kazi na kumuliki kama anavyomiliki mwanamume? Mwenyezi Mungu anatangaza waziwazi ya kwamba kama alivyokuwa mwanamume anayohaki ya kumiliki vilevile mwanamke anayohaki ya kumiliki, mwanamke anayohaki ya kurithi? Ndio mwanamke hata baada ya kuolewa vilevile anayohaki ya kurithi kama alivyokuwa mwanamume anayohaki ya kurithi.

Kwa ufupi yote tuliyoyasema ni katika kuzungumza daraja na nafsi ya mwanamke katika dini ya Uislamu katika siku hii ambayo tunakumbuka mazazi ya bint ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) bi Fatma bint Muhammad (a.s), katika siku amabyo wanachuoni wameitangaza hii ni siku ya mwanamke duniani.

Kwamba mwanamke ni kiumbe kama kiumbe kingine cha kawaida, jinsia zao ziko sawa, mapungufu kama yapo yapo kwa mwanaume na yapo kwa mwanamke, wana haki sawa kama mwanamume anahaki na vilevile mwanamke anahaki sawa.

Asanteni sana, Hongereni kwa siku hii nzito ya kuzaliwa ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) bi Fatma Zahra bint Muhammad (a.s) na siku ya Mwanamke Duniani.
Imetolewa na 
Maulana Sheikh Hemed Jalala 
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania.     Tare : 26.02.2019, Masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es salaam.

Thursday, February 21, 2019

Dkt. Harrison Mwakyembe awa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya Miaka 40 ya Mapinduzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jijini Dar es salaam.

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Mhe. Muosa Farhang (katikati) akisoma Risala kwa Mgeni Rasmi Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia), katika maadhimisho ya mika 40 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, iliyofanyika Nyumbani kwa Balozi wa Iran nchini, 11.02.2019,Jijini Dar es salaam, Tanzania.

Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akipokea Zawadi kutoka kwa Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Mhe. Muosa Farhand.

Baadhi ya Wageni ambao ni Mabalozi wa Nchi mbalimbali nchini wakihudhiria maadhimisho hayo.


Baadhi ya Wageni waalikwa ambao ni baadhi ya Viongozi wa Dini mbalimbali na katika madhehebu mbalimbali wakishirki katika maadhimisho hayo.



Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Mhe. Muosa Farhand (kushoto) akitambulisha kitabu cha Shiraz na Baluchi mbele ya Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia), kitabu ambacho kinaonyesha Mahusiano ya kihistoria katika ya Tiafa la Tanzania na Taifa la Iran.

Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akiongea katika maadhimisho ya miaka 40 ya Mapinduzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jijini Dar es salaam.






Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Mhe. Muosa Farhand akimshika mkono Makamu Raisi Msafu wa awamu ya nne Dokta Bilal akishiriki katika Maadhimisho hayo.