Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Mhe. Prof. Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi anayejenga
barabara ya Mwenge – Moroco KM 4, kuhakikisha inajengwa kwa ubora
uliokusudiwa na kukamilika kwa wakati ili kumaliza adha ya msongamano wa
magari katika eneo hilo.
Akikagua ujenzi wa barabara hiyo
Prof. Mbarawa amemtaka Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dar es
salaam kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na hatua kali
zinachukuliwa kwa watu wote watakaozembea na kuhujumu miradi ya
barabara.
“Kipaumbele chenu kiwe ubora na
kufanya kazi kwa haraka ili barabara hii ikamilike katika wakati
uliopangwa na hivyo kuondoa usumbufu kwa wananchi”, amesema Waziri Prof.
Mbarawa.
Akizungumza na wafanyakazi wa
TANROADS makao makuu Prof. Mbarawa amesema serikali haitawavumilia
watumishi wazembe wanaofanya kazi chini ya kiwango au kwa uzembe.
Amewataka TANROADS kuhakikisha
hakuna misururu mirefu katika vituo vya mizani zote nchini na kupambana
na rushwa katika ngazi zote ili kulinda fedha za serikali na kukuza
uchumi.
Akizungumza na watendaji wa Bodi
ya Mfuko wa Barabara (RFB) Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa
kutopeleka fedha za mfuko wa barabara kwa halmashauri zinazoshindwa
kujenga barabara bora na kuzitaka halmashauri zote kuhakikisha fedha
zinazopelekwa zinawiana na miradi inayojengwa.
“Bila miundombinu ya kisasa
hatuwezi kujenga uchumi tutumie fursa tuliopewa kuwatumikia watanzania
kwa moyo wa uzalendo ili kukuza uchumi wa nchi”, amesisitiza Waziri
Prof. Mbarawa.
Meneja wa Bodi ya Mfuko wa
Barabara (RFB) Bw Joseph Haule amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa
bodi hiyo inayohudumia barabara zenye urefu wa KM zaidi ya elfu 252
katika halmashauri 166 nchini imejidhatiti kuhakikisha fedha za mfuko wa
barabara zinatumika kwa kazi iliyokusudiwa ili kuimarisha sekta ya
uchukuzi na kukuza uchumi.
Katika hatua nyingine Prof.
Mbarawa ametembelea Bodi ya Wahandisi (ERB), Bodi ya Wabunifu Majengo na
Wakadiriaji Majenzi (AQRB) na Bodi ya Makandarasi (CRB) na kuagiza
kurahisisha mchakato wa usajili ili kuvutia wataalam wengi wa fani za
ujenzi kujisajili katika bodi hizo na kupunguza watendaji wasio na sifa.
“Sekta ya miundombinu ndio chanzo
cha mafanikio ya nchi yoyote duniani hivyo fanyeni kazi kwa weledi na
kuzingatia mabadiliko ya sayansi na teknolojia ili nchi ipige hatu za
haraka kimaendeleo”.
Naye katibu mkuu wa wizara ya
ujenzi, uchukuzi na mawasiliano sehemu ya ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga
amezungumzia umuhimu wa bodi hizo kujitangaza katika vyuo vikuu ili
kuvutia wanafunzi wengi kusoma fani za kihandisi na kuongeza idadi ya
wahandisi hapa nchini.
Amezitaka wakala na bodi
zinazohusika na ujenzi kuongeza ubunifu ili kutoa huduma bora na
kuiwezesha serikali kufikia malengo yake kwa wakati.
Waziri Prof. Mbarawa yuko katika
ziara ya kukagua miradi ya ujenzi na kutoa mwongozo wa namna ya
kuitekeleza kwa wakati ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO WIZARA YA UJENZI,UCHUKUZI NA MAWASILIANO
No comments:
Post a Comment