Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amewatuhumu majaji
wa mahakama za nchi hiyo kuwa wazembe kwa kuruhusu maandamano ya kupinga
serikali ambayo baadaye yaligeuka kuwa ya fujo na machafuko.
Mugabe alitoa matamshi hayo jana katika mkutano wa tawi la
vijana la chama tawala cha ZANU-PF, siku mbili kabla ya Mahakama Kuu
kusikiliza shauri la kupinga uamuzi uliotolewa wiki iliyopita wa kupiga
marufuku rasmi maandamano ya upinzani.
Serikali ya Zimbabwe ilichukua uamuzi wa kupiga marufuku kwa muda wa
wiki mbili maandamano yote katika mji mkuu Harare ambao umekuwa
ukishuhudia maandamano ya kulalamikia utendaji wa Rais Mugabe katika
kushughulikia matatizo ya uchumi, uhaba wa fedha na ukosefu wa ajira
nchini humo.
Kwa mujibu wa toleo la leo la gazeti la Sunday Mail, Rais Mugabe
aliuambia mkutano huo wa vijana wa chama chake tawala kuwa "hawezi
kuvumilia tena" na kwamba hatoruhusu maandamano ya fujo na machafuko
yaendelee kufanyika.
Kwa mujibu wa gazeti hilo Mugabe amesema mahakama, mfumo wa sheria na
majaji wa Zimbabwe wanapaswa kuwa watu wenye uelewa zaidi kuliko raia
wa kawaida na kwamba wasizembee katika maamuzi wanayotoa wakati
yanapowasilishwa maombi na watu wanaotaka kuandamana.
Kufuatia kauli hiyo ya Rais Mugabe, kiongozi wa chama cha
Kidemokrasia cha Wananchi, Tendai Biti na ambaye pia
ni mwanasheria aliyeongoza mpango wa kuwasilisha shauri la kupinga
marufuku ya maandamano iliyotangazwa hivi karibuni, amemtuhumu Mugabe
kuwa anatoa vitisho dhidi ya mahakama na kukiuka katiba.
Wakiongozwa na Biti, wanaharakati kadhaa wa kisiasa wamewasilisha
shauri katika Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo wa serikali wakisema kuwa
ni kinyume na Katiba. Shauri hilo linatazamiwa kusikilizwa hapo kesho.
No comments:
Post a Comment