Friday, August 14, 2015

Serikali yajenga vituo 22 vya kutolea huduma za makataba

Serikali imejenga vituo 22 vya kutolea huduma za makataba katika Mikoa mbalimbali hapa nchini ili kuimarisha mfumo wa kutoa elimu kwa wananchi.
Hayo yamesemwa  leo jijini Dar es salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mipango toka Bodi ya Huduma za makataba (BOHUMATA) Bw. Comfort  Komba wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Komba amesema kuwa huduma za maktaba zimefika katika Mikoa 22,Wilaya 19 na tarafa 2 ikilinganishwa na vituo 17 vilivyokuwa Mikoani na 15 katika Wilaya mwaka 2005.
“BOHUMATA imeshirikiana na Halmashauri za Wilaya za Ruangwa,Chunya,Masasi,Mbulu na Ngara katika kuanzisha na kuimarisha Maktaba Mpya katika Halmashauri hizo.” Alisisitiza Komba.
Aliongeza kuwa uanzishwaji wa maktaba  katika maeneo mbalimbali hapa nchini umesaidia kuongeza na kuhamasisha utamaduni wa kujisomea miongoni mwa wanajamii ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa kwa maktaba hizo .
Akitaja mafanikio mengine Komba amesema ni ongezeko la kiwango cha elimu,maarifa,taarifa na ujuzi miongoni mwa  wanajamii .
Pia Komba alitoa wito kwa watanzania na wasio watanzania kujenga utamaduni wa kutumia maktaba za umma kwa kuwa zipo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote.
Bodi ya Huduma za maktaba Tanzania (BOHUMATA)  ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 6 mwaka 1975 ikiwa na jukumu la kuanzisha,kusimamia,kuongoza,kuimarisha,kutunza na kuendeleza maktaba za umma ili kujipatia elimu,maarifa,taarifa,mbalimbali zitakazowasaidia katika kujiletea maendeleo.

Angalia Kikwete Akimzika Kisumo

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe mama Salma Kikwete wakitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza la Kada Mkongwe wa CCM  Marehemu Mzee Peter Kisumo wakati wa ibada ya mazishi iliyofanyika huko kijijini kwake Usangi- Mwanga Mkoani Kilimanjaro leo.

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimfariji Mama Hosiana Kisumo Mke wa Marehemu Peter Kisumo wakati wa mazishi yake huko Usangi Mwanga Mkoani Kilimanjaro.

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiweka udongo katika kaburi la Kada Mkongwe wa CCM Marehemu Peter Kisumo wakati wa mazishi yaliyofanyika nyumbani kwake Usangi- Mwanga Mkoani Kilimanjaro.

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisaini kitabu cha maombolezo kilichowekwa kanisani wakati wa mazishi ya kada mkongwe wa CCM Mzee Peter Kisumo yaliyofanyika kijijini kwake Usangi-Mwanga Mkoani Kilimnjaro.Chanzo:Fullshangwe

Monday, August 10, 2015

Profesa Lipumba Amuunga Mkono Zitto Kabwe

Wiki hii Chama Cha Wananchi (CUF) kilipata mtikisiko baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza uamuzi wa kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa chama hicho katika kipindi ambacho wengi hawakutegemea.
Uamuzi wa Profesa Lipumba uliitikisa pia ngome ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kuzingatia kuwa ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa wenyeviti wote wa vyama vinavyounda umoja huo.
Ukifuatilia kwa kina sababu alizozitoa Profesa Ibrahim Lipumba, ni pamoja na kuona kuwa Ukawa imepoteza muelekeo kwa kuwa imeshindwa kuzingatia tunu za taifa ikiwemo tunu ya uadilifu.
“Nimeshiriki katika vikao vingi vya Ukawa vilivyotufikisha hapa. Hata hivyo, dhamira na nafsi inanisuta kuwa katika maamuzi yetu ya Ukawa tumeshindwa kuenzi na kuzingatia Tunu za Taifa za utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi na uwajibikaji,” alisema Profesa Lipumba.
Maelezo ya Profesa Lipumba katika kipengele hicho yanaunga mkono kauli ya Kiongozi Mkuu wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe aliyesema kuwa vyama vingine vya upinzani havizingatii tunu ya uadilifu tofauti na chama chake ambacho kimeamua kuiweka tunu hiyo kwenye azimio lake la Tabora.
Zitto Kabwe aliyasema hayo alipokuwa anawahutubia wanachama wa chama hicho mjini Kigoma huku akiwapima mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa na Dk. John Magufuli na kudai kuwa hawana ubavu wa kupambana na ufisadi.
Ni kama Profesa Lipumba na Zitto Kabwe waliongea lugha moja katika vipindi tofauti katika kipengele hicho.
Ingawa Profesa Lipumba alishiriki katika kumsafisha Edward Lowassa na kumkaribisha Ukawa, alirudi kusema hadharani kuwa nafsi yake inamsuta hivyo ametafuta kile ambacho wazungu wanaita ‘peace of mind’.
Hata hivyo, muungano wa Ukawa una madhara chanya ya kidemokrasia katika taifa letu ambayo hata Zitto Kabwe alikiri kuyaona.
“Uchaguzi wa mwaka huu hata kama chama kimojawapo kitashinda hakiwezi kuunda serikali peke yake. Na kama kuna jambo ambalo tutalifanya wapinzani na wananchi wasitusamehe ni kushirikiana na CCM,” alisema Zitto Kabwe.Chanzo dar24

Sunday, August 9, 2015

Wanahabari Kemeeni Kukufurishana-Sheikh Jalala.

Kiongozi Mkuu wa Waislam, Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala,akiongea na Wanahabari punde baada ya kumaliza hotuba yake.
Kiongozi Mkuu wa Waislam Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania amwevitaka Vyombo vya Habari kusimamia vitu muhimu vyenye maslahi kwa Taifa pamoja na kutanua fikra na mitazamo kwa Jamii ambayo itapelekea maendeleo nchini.
“Wanahabari wanatakiwa kuwa chanzo cha kuleta mabadiliko mema katika jamii, pamoja na kuwaunganisha watanzania kuwa kitu kimoja katika Nyanja za Kiuchumi, Kijamii, Kidemokrasia, hususani nchi kuibakiza katika Amani” amesema Sheikh Jalala.
Shekhe  Jalala amekemea suala la Waislam na Watanzania  kuwa  na fikra za kukufurishana na  kunyosheana vidole vibaya pamoja na kuitana majina mabaya (makafiri)  kwani kufanya hivyo ni kuisambaratisha  jamii na matokeo yake ni kuleta  uvunjifu wa  amani.

Hayo  ameyasema leo katika semina maalumu ya Wanahabari yenye kauli mbiu “Wajibu wa Vyombo vya Habari katika Kuelimisha Jamii” iliyoandaliwa na Chuo Cha Kidini cha Imam Swadiq, Kilichopo Kigogo-Post, Dar e salaam.
 Amesema Kuwa diniya Kiislamu haina mahusiano na uvunjifu wa amani ,kwani uislamu aliofundishwa na Mtume pamoja na Mafunzo ndani ya qur’an ni Uislam ambao unaolingania amani, maelewano,ushirikiano kwa dini zote.
Shekhe Jalala ameitaka jamii ya kiislamu kuyaelewa na kusoma vizuri namna mtume alivyoishi ishi maka na madina kwani aliishi na washirikina na mayahudi kwa amani na salama hivyo hivyo alikaa nao vikao ili kulinda amani.
Hawa ni baadhi ya Wanahabari walioshiriki katika Semina ya Wajibu wa Vyombo vya Habari katika Kuelemisha Jamii.
 Hatahivyo amesema  kuwepo kwa bidii, jitihada na mikakati ya dhati  kwa viongozi wa dini wa Tanzania itakuwa ni kiashirio kizuri cha amani kwa kuweka vikao vya pamoja kwa mashekhe, maskoofu na wachungaji juu ya kulinda amani na si kukutana kwenye vikao vya posho.

Wanahabari Wanatakiwa Kuleta Mabadiliko nchini

Kiongozi Mkuu wa Kiroho wa Waislam, Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala akiongea na Wanahabari nje ya Ukumbi wa semina baada tu ya kumaliza Khotuba yake.
 
“Wanahabari wanatakiwa kuwa chanzo cha kuleta mabadiliko mema katika jamii, pamoja na kuwaunganisha watanzania kuwa kitu kimoja katika Nyanja za Kiuchumi, Kijamii, Kidemokrasia, hususani nchi kuibakiza katika Amani” amesema Sheikh Jalala.
 
Hayo  ameyasema leo katika semina maalumu ya Wanahabari yenye kauli mbiu “Wajibu wa Vyombo vya Habari katika Kuelimisha Jamii” iliyoandaliwa na Chuo Cha Kidini cha Imam Swadiq, Kilichopo Kigogo-Post, Dar e salaam.
.

 Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Bwana Chairs Kayoka akitoa khotuba yake inayowataka wanahabari kabla ya kuandika habari wafanye Uchunguzi.
 




Saturday, August 8, 2015

Abwao: UKAWA hawana nia nzuri; Watanzania msipeleke wafanyabiashara Ikulu

ALIYEKUWA mjumbe wa kamati kuu Taifa ya Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) na mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Bi Chiku Abwao amevitaka vyombo vya habari nchini kusaidia kuwaokoa watanzania juu ya kasi kubwa ya wafanyabiashara kung'ang'ania kwenda Ikulu kupitia vyama vilivyokuwa vikiunda umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) kuwa kinachoendelea ndani ya UKAWA ni hatari kwa ustawi wa Taifa na sasa limekuwa ni genge la wafanyabiashara.

Ambwao ambae alijiengua na CHADEMA hivi karibuni na kujiunga na chama cha ACT Wazalendo alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanahabari mkoani Iringa juu ya maandalizi ya mkutano mkubwa wa ACT Wazalendo utakaoongozwa na kiongozi mkuu wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe siku ya jumapili wiki hii.

Alisema pamoja na kuwa dhamila ya kukitoa chama cha mapinduzi ipo kupitia vyama makini kama chama chake cha ACT Wazalendo ila bado kuna njama mbaya zinazofanywa na vyama hivyo zilivyojipachika jina la UKAWA kutokana na kuonyesha kwao wazi wazi kuwa wapo kimaslahi zaidi na sio kwa ajili ya kulikomboa Taifa hili kwa kupinga ufisadi ila wapo kwa ajili ya kusafisha na kutetea vitendo vya ufisadi nchini jambo ambalo ni hatari na kuna kila sababu ya vyomba vya habari nchini kusaidia kuelimisha jamii ili kukwepa kuingizwa mkonge UKAWA wanaokumbatia ufisadi.

Alisema kuwa yeye ni miongoni mwa wanasiasa wazuri hapa nchini ambae kamwe hapendi siasa za maji taka za kukumbatia vitendo vya ufisadi bali yupo kuona anakemea na kupinga kwa nguvu zote vitendo vya ufisadi hapa nchini hivyo hakupendezwa kabisa na hatua ya CHADEMA kumpokea waziri mkuu mstaafu Edward Lowasa kuwa mgombea urais huku wakitambua wazi kuwa hana sifa ya kupinga ufisadi.

"Dhamira ya kukitoa chama tawala madarakani ipo lakini kwa hatua ambayo UKAWA wameonyesha ni kama wapo kwa ajili ya kushangilia vitendo vya ufisadi kutokana na kukumbatia wale ambao awali waliwaita kuwa ni mafisadi papa na leo wanatumia nguvu kubwa kuuaminisha umma kuwa ni wasafi... huu ni sawa na unafiki ambao UKAWA wameuonyesha na kamwe itakuwa ni vigumu watanzania kuamini haya kwa leo... huyu akiwa CCM tulipaza sauti kuwa ni fisadi leo amekuja upinzani tunauaminisha umma kuwa ni msafi... hapana hii si siasa ya ukombozi kwa mtanzania ila ni siasa ya kibiashara zaidi ambayo inafanyika UKAWA... nawaombeni sana wanahabari nchini msaidie kuliokoa Taifa hili mhakikishe kiongozi anayekwenda Ikulu awe mweye mwonekano wa kuliokoa Taifa hili si wa kwenda kutumia kivuli cha Ikulu kuboresha biashara zake," alisema Chiku.

Bi Chiku alisema Taifa hili kwa sasa limekwenda pabaya kwani limekwisha tekwa na wafanyabiashara na kuwa kwa upande wake haamini kama kweli kwa viongozi wa Chadema wanania nzuri na Taifa hili kwa jinsi ambavyo wanavyotangulia pesa mbele na kutaka kuwaingiza kwa nguvu kubwa wafanyabiashara Ikulu.

"Hawa CHADEMA awali walikuwa mstari wa mbele kukemea ufisadi ila leo wamegeuka na kukumbatia ufisadi na kuwa chama cha kuwasafisha mafisadi kwa kumpa nafasi ya kuwa mgombea urais LOwasa na kumuacha Dk Slaa ambae ni nembo ya siasa za Tanzania na nembo ya CHADEMA... Dk Slaa ni kiongozi msafi na muadilifu anayetambua kila mmoja wetu na kuwa dhamira ya kutaka kuongoza nchi yawezekana wanayo ila si dhamira nzuri kwa watanzania wanataka kutuuza watanzania kwani tutakwenda pabaya kuliko hapa tulipo."

Hata hivyo alisema kwa hali ya mambo yanavyokwenda ni wazi kuna wakati mgumu zaidi kuliko wakati wote ule uliopita kwani ni mwaka huu pekee ambao vyama vya upinzani vinakwenda katika uchaguzi mkuu kwa lengo tofauti kabisa la kuwapeleka wafanyabiashara na wachafu Ikulu tofauti na awali ambapo vyama vya upinzani kazi kubwa ilikuwa ni kupinga CCM kwa ufisadi ila leo watanzania wanashuhudia upinzani ukitetea ufisadi .

Bi Chiku aliwataka wananchi kuwa makini na mbinu chafu ya UKAWA kutaka kuliangamiza Taifa hili na kuchagua vyama makini na viongozi makini kutoka chama cha ACT-Wazalendo ambacho ndicho chama chenye sera na misingi imara ya kulikomboa Taifa hili kutoka mikononi mwa CCM.

Kwani alisema hata kinachotokea ndani ya UKAWA kwa sasa kwa viongozi kujiuzulu nafasi zao ni sehemu ya pigo kutoka kwa mwenyezi Mungu kwa kuona wale waliotumwa kuokoa wakikengeuka na kuwa waangamizaji wakuu wa Taifa hili na kuwa hamshangi aliyekuwa mwenyekiti wa CUF Prof Ibrahimu LIpumba na Dk Slaa kujiuzulu nafasi zao kwani kama wangebaki ni wazi heshima yao ingeshuka zaidi ya hapo na kuwa ndani ya UKAWA kuna viongozi wasiozidi wawili ambao wanafanya siasa kuwa biashara binafsi.Chanzo Wavuti

Friday, August 7, 2015

Sheikh Mkuu wa al Azhar: kuwakufurisha Waislamu wa madhehebu ya Shia ni kitendo kisichokubalika

Sheikh Mkuu wa al Azhar nchini Misri amesema, kuwakufurisha Waislamu wa madhehebu ya Shia kunakofanyika kupitia kanali za televisheni za satalaiti ni kitendo kisichokubalika na jambo hilo haliwezi kuhalalishwa au kutetewa kwa kutumia kitabu kitakatifu cha Qur’ani, Suna na mafundisho ya dini.
Sheikh Ahmad al Tayyib amesema Waislamu wa madhehebu ya Suni wanaswali nyuma ya maimamu wa madhehebu ya Shia na kuongeza kuwa: Baina ya Shia na Suni hakuna hitilafu kubwa zinazoufanya upande mmoja uukufurishe na kuutoa katika dini upande mwingine na kwamba kinachoshuhidiwa kwa sasa na kutumiwa vibaya na kwa malengo ya kisiasa baadhi ya hitilafu za kimitazamo. 
Sheikh al Tayyib amesema wadhifa mkuu wa al Azhar ya Misri ni kufanya jitihada za kuunganisha Umma wa Kiislamu licha ya hitilafu za kimitazamo zilizopo katika ulimwengu wa Kiislamu. Sheikh Mkuu wa al Azhar amesema yuko tayari kusafiri na kwenda eneo lolote lile duniani kwa ajili ya kuimarisha umoja wa Waislamu.
Kwa kutilia maanani hali ya sasa ya nchi za Waislamu, inaonekana kuwa umoja wa Waislamu ndiyo wenzo muhimu zaidi ya kuwawezesha kuvuka salama fitina na njama za ubeberu na maadui wa dini hiyo ya Mwenyezi Mungu. Wakitumia mbinu mbalimbali, maadui hao wa Uislamu wamelifanya suala la kuanzisha vita na mapigano kati ya Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni kuwa ndiyo ajenda yao kuu kama njia ya kugawa na kuzusha hitilafu katika Umma. Nyenzo zinazotumiwa na maadui hao kwa ajili ya kupenya baina ya Waislamu ni kutumia wasaliti waliopotoka kutoka madhehebu mbalimbali za Waislamu na kisha kuhubiri tafsiri zisizo sahihi za kisiasa.
Kufasiri na kuhubiri Uislamu wa Kimarekani ni njama ambayo lengo lake ni kuzusha mpasuko na hitilafu katika safu za Waislamu na kuzuia ulimwengu wa Kiislamu kuwa nguvu kubwa katika siasa za kimataifa. Maadui wa Umma wa Kiislamu wanadhamini maslahi yao haramu kwa kuzusha na kukuza hitilafu ndogondogo baina ya Shia na Suni. Kwa njia hiyo maadui wa Umma wanawashughulisha Waislamu na masuala yasiyokuwa na umuhimu na kuwaghafilisha na mauala ya asili ya muhimu sana hususan kadhia ya Quds tukufu. Maadui hao wanaupambanisha Uislamu halisi na sahihi unaosisitiza umoja na mshikamano na ule wa fikra mgando unaowakilisha ujahili na ukatili. Mfano wa uislamu mgando ni ule wa makundi ya kigaidi ya Daesh, al Qaida na Boko Haram ambayo yote yanaungwa mkono kwa njia moja au nyingine na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kama anavyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, katika maktaba na mfumo wa kifikra wa Imam Khomeini, Uislamu wa mashekhe vibaraka wa watawala, Uislamu wa Daesh, Uislamu usijali na unaokaa kimya mbele ya jinai zinazofanywa na Marekani na Israel na kunyoosha mkono wa udugu na urafiki kwa madola ya kibeberu unatokana na chanzo kimoja na hauwezi kukubalika.
Kwa msingi huo Waislamu wanapaswa kuwa macho na wasiruhusu maadui kutumia vibaya hitilafu zao za kimaoni na kimitazamo.