Friday, October 9, 2015

Wanajeshi wa Israel wawaua shahidi Wapalestina 6

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mapema leo wamewaua shahidi Wapalestina 6 katika Ukanda wa Gaza. Duru za hospitali zinasema kuwa, Hammoud Hisham, Ahmad al-Harbawi, Abed al-Wahidi na Hussam Dawla wamefariki dunia kutokana na majeraha mabaya ya risasi. Wanajeshi wa utawala haramu wa Israel wametumia risasi hai kuwatawanya waandamanaji katika eneo la Shejaiya huko Gaza ambapo mbali na kuwaua shahidi watu 6 pia wamewajeruhi wengine kadhaa. 
Wapalestina wanaandamana kupinga hujuma za Wazayuni dhidi ya msikiti mtakatifu wa Al-Aqsa. Kwa siku kadhaa sasa, Israel imekuwa ikiwavamia Wapalestina na kuwakamata ovyo huku ikiwazuia kuingia na kufanya ibada katika msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.    
Wanajeshi wa Kizayuni pia wamewavamia waandamanaji wa Kipalestina katika Nablus huko ukingo wa magharibi wa Mto Jordan na habari zinasema watu kadhaa wamejeruhiwa na wengine wengi kukamatwa.Chanzo irib

Tuesday, October 6, 2015

Swala Tanzania kuanza uchimbaji mafuta Kilombero

Kampuni ya mafuta na gesi ya Swala Tanzania plc  inapenda kutaarifu  kwamba  imechagua eneo kwa ajili ya uchimbaji wa kisima cha mafuta na utafutaji kwa mwaka  2016 ambao utafanyika kwenye eneo tarajiwa la Kito  kwenye leseni ya Kilosa- Kilombero.
 Akifafanua kuhusu kuanza kwa uchimbaji huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Swala, David Mestres Ridge alisema kuwa tafsiri ya marudio ya 2013 na 2014 ya takwimu za mirindimo zimesababisha  kuboreshwa kwa uelewa wa eneo tarajiwa  la Kito, huku akiongeza kuwa tathmini za mirindimo zilizopo zimebainisha kuwepo umbo la ziada kwenye ufa unaopakana na bonde  hilo la Kito lilopo upande wa magharibi mwa bonde la Kilombero.
“Tafsiri mpya za takwimu kwenye bonde la  Kito  zimeonesha kuongezeka kidogo kwa ukubwa muundo wa ramani iliyotengenezwa awali wakati mapitio ya awali ya muundo huo wa ziada  yameiwezesha kampuni  kukubaliana na hazina  iliyopo kwenye bonde la Kilombero.
 Ridge alisema, “Mapitio ya kiufundi kwa Bonde la Kilombero yanaonesha matarajio ya Kito  yatakuwa makubwa  na yametoa vidokezo vya matumaini vya kuwepo rasilimali muhimu ndani ya bonde hilo. Kampuni ya Swala ipo kwenye mchakato wa kumalizia  tathmini ya athari za mazingira (EIA) kwenye maeneo yaliyoteuliwa kwa ajili ya uchimbaji na pia kutafuta wakandarasi wa uchimbaji kwa ajili ya kisima cha utafutaji mafuta cha Kito kwa mwaka 2016.

                                                             Kuhusu Swala:

Swala ni kampuni iliyo chini ya kivuli cha Swala Energy Limited, kampuni ambayo kwa upande wake iko kwenye orodha ya soko la hisa la nchini Australia (ASX) na ikijulikana kwa kifupi kama "SWE". Swala inamiliki mali katika nchi za Afrika Mashariki zinazopitiwa na mfumo wa bonde la ufa na ina ardhi yenye eneo la zaidi ya kilomita za mraba 17,500. Swala inafanya kazi kwa juhudi na ina mpango wa maendeleo ya biashara ili kuendelea kukua hasa katika majimbo ya Afrika Mashariki yenye nishati ya hydrocarbon.

Sunday, October 4, 2015

SOMA KWA UNDANI HAPA ALICHOONGEA LIVE KINGUNGE MUDA HUU WAKATI ANAVUA RASMI UANACHAMA WA CCM.

Kingunge amevua rasmi uanachama wa CCM na amesema sababu ya kujitoa CCM ni kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho kwasasa na hatojiunga na chama kingine ila yuko upande wa mabadiliko
Kingunge- "Kila unapopita vijana,kinamama, na watanzania wote wanataka mabadiliko na mimi niko upande wa mabadiliko na yaje haraka"
Kingunge- "Wanabadilisha kibwagizwo toka kidumu 'chama cha mapinduzi' hadi 'kidumu chama tawala', hapo ni kung'ang'ania madaraka"
Kingunge- "Baada ya kukaa madarakani muda mrefu chama cha CCM hakiwezi kufanya jipya, chama kikikaa nusu karne hakina jipya tena"
Kingunge- "Mabadiliko ni muhimu kweli kweli, upate watu wengine wenye pumzi mpya, mnataka mbakie nyinyi tu, nyie pumzi imekwisha"
Kingunge -" Sisemi chama hiki cha zamani kisifanye kazi, kiwekwe kando kwa muda, CCM imeacha kujadili issues sijui wanajadili nini"
Kingunge- "Wanaotaka tuondoke hapa twende mbele lazima watu wapya waongoze, lazima fikra mpya ziongoze".
Kingunge- "Tumefika mahali pagumu sana, nguvu ya kupinga mabadiliko ni kubwa ila kwa utafiti wangu nguvu ya wanaotaka mabadiliko ni kubwa zaidi hivyo msiogope" amemalizia kwa kusema hayo

BREAKING NEWS Ndugu Kingunge Ngombale Mwiru ametangaza rasmi kujivua uanachama wa CCM

BREAKING NEWS: Mwanasiasa mkongwe ambaye ni kada maarufu wa chama cha CCM Ndugu Kingunge Ngombale Mwiru ametangaza rasmi kujivua uanachama wa chama hicho cha siasa na amesema sababu kubwa ni kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho kwa sasa.

Amesema hatojiunga na chama kingine cha siasa ila anaamini vijana, kinamama, na watanzania wanahitaji mabadiliko na yeye yuko upande wa mabadiliko. kwa habari zaidi tutaendelea kukujuza zaidi

Ujumbe wa Sheikh Hemed Jalala baada tu ya Kurejea kutoka katika Ibada ya Hijja, 16 Dhulhijja 1436, Sawa na 30/09/2015



Mmoja wa Viongozi Wakuu wa Kiroho wa Waislam, Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala, akiongea na Wanahabari juu ya Chanzo cha Vifo vya Mahujaji, punde tu baada ya kutoka Hijja
Bismillah Rahmani Rahim.
Asalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatu
Ujumbe wa Sheikh Hemed Jalala baada tu ya Kurejea kutoka katika Ibada ya Hijja, 16 Dhulhijja 1436, Sawa na 30/09/2015
Kwa kuwa kama mtanzania na mmoja katika viongozi wakuu wa kiroho wa waislam,dhehebu la shia Ithnasheriya Tanzania na kwa kuwa leo ndio tumefika katika miongoni mwa misafari inayotoka Hijja. 
Nadhania itakuwa vizuri zaidi na mimi nishiriki pamoja na watanzania wenzangu, ambao bila shaka wanashauku kubwa na wanahamu kubwa yakutaka kujua yaliyotokea katika ardhi takatifu.

Nipende kusema kwamba  tunamshukuru Mungu (swt) tumemaliza ibada hii ya hijja kwa usalama sisi kama watanzania, lakini jambo la kusikitisha na la kuliza kwamba hatukurudi sote salama ambao tuliokwenda kutekeleza hiyo ibada ya hijja, wako ndugu zetu ambao badala ya kuwapokea mahujaji wao,wamepokea habari za kusikitisha, habari za kilio na habari za msiba.
Napenda kwa kweli kuwapa pole wote watanzania ambao waliokumbwa na msiba huu kwa  nyumba zote ambazo watu wake wamefariki katika ardhi ya minna, mwenyezimungu (swt) watu hao awape shubira awape uvumilivu,na awalipe kila la kheri, vilevile kwa msiba huu uliowatokea, na ninaamini ni msiba wa Kitaifa na Kimataifa kwa watanzania wote.
Baada ya kusema hayo niseme kwakweli pamoja ya kwamba tumetekeleza ibada yetu hii ya hijja kwa salama,lakini naweza kusema kwa kweli kilichotokea  katika ibada ya mwaka huu ni jambo la kutisha  na ni jambo la kusikitisha na ni jambo ambalo kunyamaziwa kimya kwa kweli sio sawasawa na sio mahala pake.Idadi ya watu waliokufa ni wengi mno, na tukizungumza ripoti ya mwisho mwishoidadi  isiopungua zaidi ya Mahujaji 4000


Na hawa wamepotea na tunaposema wamepotea la siwezi kusema ninaudhibitisho kuwa wamekufa ,lakini wamepotea wapi? Tunapozungumza Minna ni mtaa na vilevile tunazungumza sio kama watu wamefunikwa na kifusi, hapana, bali ni watu walio kufa njiani, kwahivyo tumewakosa watu hawa, watu 4000 ni watu wengi mno,hakuna taifa ambalo halijaguswa na msiba  huu
Je,kutokea jambo hili katika zama hizi ni mahala pake? Ukiliangalia tukio la kumpiga shetani siku ya Eid, vikuta hivi ni vikuta vikubwa wapo watu wanapiga chini na wengine juu na baada ya kupiga watu wanatoka na hawarudi, lakini kwanini hili limetokea. Hili limetokea kwa sababu hizi njia kuu zilifungwa, njia ambzo ndio kuu zilifungwa, kwani njia hizi kuu zingiwa wazi, lisingetokea tukio lolote.
Na ndio maana tunaona kwamba sehemu za kupiga shetani kutoka zimepanuliwa haijawahi kutokea tukio la vifo katika sehemu hizo, kwahivyo kilichotokea ni kwamba sehemu hizi zilifungwa mahujaji pamoja na wingi wao wakatakiwa wapite katika njia ambazo sio njia pana hapa wakakusanyika wanaokuja kumpiga shetani na wanaorudi kutoka kumpiga shetani, pakatokea maafa ya kusikitisha.
Sisi na nikiwemo mimi kama Imam wa Msikiti wa Ghadir, Kigogo-Post, na Mmoja wa Viongozi wa Wakuu wa Waislama, Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania kwa kweli ninaibebesha Serekali ya Saudia Arabia kwa Uzembe uliotendeka na uliofanyika katika tukio hili. Serikali ya Kifalme ya Saudia Arabia inabeba dhima hii kubwa, kwanini inabeba,inabeba kwa sababu kwanza zipo barabara kubwa ambazo hazipungui mita 30,

kwa nini mahujaji wasiruhusiwe kupita barabara hizo, hili la kwanza , la pili na hili ni muhimu vilevile la kuliangalia kwa makini sehemu takatifu zimezungukwa na Kamera , hivi hizi kamera hazikuona watu wanokufa,kwani  kila baada ya dakika 3 walikuwa wanakufa watu wasiopungua watano.

Kwa hiyo mimi naamini na ni msimamo wangu kwamba serikali ya Saudia Arabia inabeba jukumu lote la kutokea vifo vya mahujaji hawa, kama inavyobeba jukumu la kizembe la kwanza lililotokea katika ardhi ya makka lililotokea katika msikiti, masjid Haram, swala la Winchi,hili linabeba serikali na Serikali yenyewe imekubali kwamba ni kosa imefanya.

Lakufanya ni nini? Kama watanzania mimi ningeiomba serikali na viongozi wa nchi watambue ya kwamba tunapokwenda hijja hatwendi kufa, tunakwnda kutekeleza moja ya nguzo za Kiislam, kwahiyo hatwendi kule kufa, hiyo ieleweke,na kama kuna watu wanaitikadi hiyo, itikadi hiyo sio sawasawa.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni lazima iungane na nchi ambazo zinaidadi kubwa ya Mahujaji inayowapeleka serikali iungane nao katika kuhakikisha kwamba wanashirikishwa katika upangaji wa Ibada ya Hijja. Kushiriki katika kupanga Ibada ya hijja haina maana tumeingilia mamlaka ya Serikali ya Saudia Arabia ,haina maana hiyo.kwa sababu Ibada ya hijja ni Ibada ya Waislam wote. Ili nayo ione na ikinaike, Je, inayohaki kuwapeleka watanzania katika ibada hiyo wakaenda na wakurudi salama. Hili ni jambo la kwanza serikali inaweza kulifanya.

Jambo la pili ambalo linaweza kufanyika ni zile nchi za Kiislam (OIC) ni umoja wa Nchi za Kiislam,umoja huu usimamie, kwa sababu taratibu zote zinaonesha kwamba serikali ya Saudia Arabia imefeli katika kupanga Ibada ya hija ndio yakatokea mauaji haya ya Kimbari.kwa hivyo umoja wa nchi za Kiislam zilisimamie Ibada hii ili iende salama.

Na kwa kuwa hija ni Ibada ya Usalama, ibada ya maelewano ni Ibada ya Amani na muanzilishi mkuu wa ibada hii ni Nabii Ibrahim (a.s), Nabii Ibrahim ni Nabii wa watu wote , ni Nabii wa Waislam, ni Nabii wa Wakristo, Ibrahim(a.s) alimzaa Ishaq (a.s) ni mtume anaekubalika kwa ndugu zetu Wakristo na Ismail (a.s) ni mtume anaekubalika kwa Waislam na Wakristo.

Niseme kwamba Ibada hii sisi mahujaji tunauombea mungu Uchaguzi ambao ndio tupo karibuni kuingia. Tunaiombea sisi kama Mahujaji mimi na wenzangu tumeorudi katika msafara huu kwamba Mungu aibakishe amani na utulivu na maelewano nchi hii katika kipindi hiki kigumu ambacho tunaingia, Niliwahi kuongea na ninaendelea kuongea yakwamba miongoni mwa Vigezo vikubwa vya kura zetu tumpe nani,

Tumpe Yule mtu ambaye anawataka watanzania kuwa kitu kimoja , anawataka watanzania wawe ndugu, yeyote ambae mantiki yake , fikra zake ni kuwagawanya Waislam na Wakristo kuwagawanya watu wenye dini tofauti ambao wanaokaa vizuri, huyu ndugu zangu Watanzania hatuna haki ya kumpa kura zetu. Mungu aibariki Tanzania, Mungu aupitishe Uchaguzi huu uwe Huru, Uwe Salalama na Tanzania ibakie kuwa nchi ya amani, Utulivu, Maelewano na Busara.    
                                                          Asanteni Sana
                                                          Wabillah Tawfiq

Mchungaji Christopher Mtikila afariki dunia leo alfajiri

Mwanasiasa mashuhuri nchini na Mwenyekiti wa Chama Cha DP Mch.Christopher Mtikila amefariki dunia na watu wengine watatu kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea katika kijiji cha Msolwa kilichopo Chalinze mkoani Pwani asubuhi ya leo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jafari Mohamed, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa “Taarifa za mwanzo” zinasema Mtikila amefariki majira ya saa 11:45 asubuhi ya leo katika kijiji cha Msolwa, Chalinze.

Amesema gari alilokuwa amepanda Mtikila lilikuwa linatoka mkoani Morogoro kwenda Dar es Salaam, ndani ya gari hilo kulikuwa na watu wanne ambapo wengine watatu wamejeruhiwa vibaya na kupelekwa katika Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha Pwani
Kwa habari zaidi endelea kufuatilia habari zetu tutakujuza hivi punde

Thursday, October 1, 2015

Maafa ya Mahujaji sio Mpango wa Mungu (swt)

Mmoja wa viongozi wakuu wa kiroho wa waislamu, Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala amesema maafa yaliyotokea Hijja sio mpango wa Mungu bali yamesababibshwa na serikali ya Saudi-Arabia
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dares salaam baada ya kurejea kutoka Hijja alfajiri ya leo Sheikh Jalala amebainisha kuwa serikali ya Saudia inapaswa kukiri kuhusika na maafa hayo kwakuwa kulikuwa na usimamizi mmbovu uliopelekea maafa hayo

Akibainisha sababu za serikali ya Saudia kubeba mzigo wa lawama Jalala amesema kitendo cha kufunga barabara mbili zenye ukubwa wa mita 30 zinazo elekea eneo la jamarati na kuwaacha mahujaji kutumia barabara ndogo ndio chanzo kikubwa cha maafa ya mahujaji wakati wakitekeleza ibada ya kumpiga mawe shetani.

Hata hivyo ameongeza kuwa licha ya eneo kuwa na kamera kila kona lakini mahujaji waliokuwa wakipoteza maisha kila baada ya dakika tano hawakuweza kuokolewa na hata kitengo cha msaada wa kwanza hakikutimiza majukumu yake kikamilifu jambo ambalo lilipelekea idadi ya vifo vingi

Aidha sheikh Jalala amesema  jambo hilo ni la kusikitisha na kwamba haitakuwa busara kulikalia kimya kwakuwa idadi ya watu waliopoteza maisha na ambao mpaka sasa hawajulikani walipo ni kubwa saana na kwamba serikali ya Tanzania inapaswa kuliingilia kati kwa kuwa watu walienda maka kuhiji na sio kupoteza maisha.

Katika ibada ya Hijja mwaka huu zaidi ya mahujaji 700 wameripotiwa kupoteza maisha katika mkanyagano tofauti na hijja zingine.