Tuesday, December 13, 2016

"Vyama vingine wakitaka kufanya vikao hapa Ikulu waombe ila tutataka kujua ajenda zao." Magufuli

Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akihutubia katika kika cha chama hicho leo jijini Dar es salaam
"Sioni aibu ya kuwakaribisha wanaCCM hapa Ikulu maana bila ninyi nisingefika hapa, hapa ni mahali pa watanzania wote'."
"Nitapenda chama changu CCM kizingatie kanuni za uchaguzi ikwemo kanuni ya kiongozi kuwa na nafasi moja tu ya uongozi."
"Nitapenda kuwa na jumuiya za chama zinazozingatia matakwa ya chama."

"Hii haitakuwa mara ya mwisho tutakapoamua hakuna mtu atakayenipangia nifanyie mkutano wapi."
"Hatutaki kuwa na chama legelege cha watu walalamikaji, sisi ndio tumepewa ridhaa na wananchi kuongoza."
"Napenda tuwe na chama kinachoongozwa na wanachama na sio chama kuongozwa na mtu chama ni mali ya wanachama na sio mtu."

"Nitapenda kuwa na jumuiya za chama zinazozingatia matakwa ya chama."
"Napenda tuwe na chama kinachoongozwa na wanachama na sio chama kuongozwa na mtu chama ni mali ya wanachama."
"Tunataka kununua meli mbili, moja ziwa Tanganyika na nyingine ziwa Victoria."

"Tunataka chama chetu kijitegemee kiuchumi, ni aibu kutegemea fedha za ruzuku na watu binafsi ili kujiendesha."
"Rasimali nyingi hatunufaiki nazo kutokana na mikataba isiyo na tija, usimamizi mbovu na ubadhirifu."
"Wapo wananchama wachache ambao ukisaliti chama chetu hasa kipindi cha uchaguzi na wengine kuendeleza makundi."

"Katika awamu hii hatutamsamehe mtu yeyote wa kutafuta uongozi kwa njia ya rushwa."
"Naziagiza jumuiya zote kuhakikisha kanuni zao zinaendana na katiba ya C.C.M......"

"CCM itaongeza idadi ya Wanachama, kupambana dhidi ya Rushwa, kujitegemea Kiuchumi, kukomesha makundi ndani ya Chama, kujiimarisha ngazi ya chini ya Wanachama".
"Napenda kuona sasa mtu mmoja akishika cheo kimoja ndani ya C.C.M badala ya vyeo vingi kama ilivyo sasa"

"CCM kuzingatia Kanuni zake za uchaguzi, Kanuni za Jumuiya ziendane na Katiba ya Chama, CCM kuongozwa na wanachama badala ya chama kuongozwa na Mwanachama".
"Nitapenda sana chini ya uongozi wangu, vikao vya maamuzi huku juu viwe na watu wachache."

"Nawaomba wajumbe mabadiliko yatakayoletwa kwenu myachambue, myapitie na kisha kuyapitisha kwa maslahi ya chama chetu CCM maana sisi Kamati Kuu tumeshayapitisha sio kwa vyeo vyetu bali maslahi ya chama chetu."

Dk.John P. Magufuli
Mwenyekiti CCM Taifa.

Ufunguzi Kikao cha NEC 13/12/2016

“Tusheherekee Maulid ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwa kupambika na Huruma yake” Sheikh Jalala

                                   
Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala akisisitiza jambo katika Kikao na Waandishi wa Habari katika Kuadhimisha siku ya Kuzaliwa (Maulid) ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) jijini Dar es salaam.
                               TAARIFA KWA UMMA
Ndugu zangu Waislam wenzangu Asalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatu,Amani ya Mwenyezimungu iwe kwenu wote. Napenda kwanza niwape hongera kwa waisla wote watanzania kwa tukio hili la kukumbuka kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), napenda niwape Hongera kwa sababu ya tukio hili kubwa la kuzaliwa kiongozi huyu.

Kama ambayo nawapa hongera Watanzania wote Waislam na wasiokuwa waislam kwa kushirikiana na watanzania wenzao katika tukio hili la Maulid, katika tukio hili la kuzaliwa Mtume wa Huruma, Mtume wa Upendo, mtume wa Mapenzi, Mtume wa Maelewano, Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Katika siku hii ya Maulid na katika kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume huyu napenda kuzungumza jambo moja ambalo ni nzito na la muhimu, na sisi kama watanzania wote kwa ujumla Waislam na wasiokuwa waislam tunalihitajia tukio hilo, au tunayahitajia maelezo hayo yanayohusiana na Mtume wetu Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Tukio hili napenda nimesome Mtume kwenye upande wa kazi moja kubwa ambayo sisi kama watanzania tunahitajia nayo ni kazi ya Kuwaunganisha watu,Moja ya kazi kubwa muhimu ambayo mtume huyu tunaemkumbuka Maulid na kuzaliwa kwake leo,moja ya kazi kubwa nyeti na muhimu aliyoifanya ilikuwa ni kuwaunganisha watu.
 
Hawa ni baadhi ya waandishi wa habari upande wa Television wakiwa makini kumsikiliza Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) yeye sambamba na mitume wengine wote waliopita,moja ya kazi yao kubwa ilikuwa ni “Tauhidil Kalima” ni Tauhidil Umma” ilikuwa ni kuwaunganisha watu, kwanzia Mtume Adam (a.s) mpaka kufikia Mtume Ibrahim (a.s), mpaka kufikia Mtume Mussa (a.s), Mpaka kufikia Mtume Issa / Yeu(a.s) na hatimae kufikia kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), hao wote moja ya mafunzo yao muhimu na makubwa ilikuwa ni kuwafanya watu wawe kitu kimoja.

Hakuna Mtume aliekuja kuja kufundisha mafundisho ya kuwatenga watu, hakuna mtume wa Mungu aliyekuja kuwafunza watu kutengana, bali watu wote walikuja kuwaunganisha watu kuwa kitu kimoja.Siku hii ambayo leo tunakumbuka Mazazi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) naamimi ya kwamba darasa hili la Umoja aliyoifunza Mtume Muhammad (s.a.w.w), aliyoifunza Nabii Issa / Yesu (a.s), naamini darasa hili muhimu  Watanzania wanalihitajia leo kuivaa na kuiunga Mkono kwa hali na mali.

Dini zote zilizotoka kwa Mungu, Vitabu vyote vilivyotoka kwa Mungu,ikiwemo Taurati,ikiwemo Injiir, ikiwemo Zabour na ikiwemo Qur’an takatifu, vitabu vyote hiyo ukijaribu kivisoma kwa umakini vyote vimekuja kumuunganisha  Mwanadamu na wala sio kumgawanya Mwanadamu, Kama Mitume walifanya kazi za kuwaunganisha watu na vitabu vya mungu ukivisoma vyote vinakazi ya kuwaunganisha watu.

Hatuna kitabu cha Mungu kinachowagawanya watu,hatuna kitabu cha mungu kinachowabagua watu, hatuna kitabu cha mungu kinachowatenga watu, kwahivyo dini zote zilizotoka kwa mungu zote zimelingania kuwafanya watu kuwa kitu kimoja, 

zote zinawataka watu wasikilizane na waelewane, na mimi naamini na mtakubaliana na mimi watanzania wenzangu ya kwamba Moja ya mafunzo muhimu leo hii yanayotakikana kwa watanzania wote pamoja na tofauti za dini zao, wawe Waislam, wawe Wakristo, wawe Mayahudi na wawe wenye dini zingine zinazojulikana, naamini yakwamba mafunzo haya wanayahitajia Watanzania.

Na ninaamini vilevile taifa hili kwa darasa hili na somo hili linalofunzwa katika siku hii ya kumbukumbu ya kuzaliwa Muhammad (s.a.w.w) vilevile naamini Watanzania pamoja na Taifa kwa ujumla linahitajia.Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) ameishi sehemu mbili huyu amabe tunamkumbuka leo hii kualiwa kwake, Bwana huyu ameishi katika mji wa Makka, ameishi vilevile katika mji wa Madina. 


Katika Mji wa Makka katika kazi alizozifanya nataka kuonyesha vipi Mtume alipokuwa Makka alijitahidi kuwaunganisha watu na si kuwagawanya.

Watu wa Makka au Wakazi wa Makka walikuwa na Dini tofauti, walikuwepo Wakristo, walikuwepo Mayahudi, walikuwepo wanaoabudu Masanam wanaoabudu Hubal, Lata Manata walikuwa ni waungu wao wakiwaabudu, lakini angalia Mtume Muhammad (s.a.w.w) alivyoishi na watu wa Makka, aliishi na watu wa makka mpaka wenyewe wakawa wanasema “Hatujawahi kukuona wewe ukiongopa katika jambo” huu ni ushuhuda au ushahidi unaotolewa na watu sio Waislam ndani ya ardhi ya Makka.

Hii ni kuonesha ya kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) moja ya masomo yake muhimu yalikuwa ni kuwaunganisha watu, yaani kuunganisha Umma, yaani ni kuwafanya watu kuwa kitu kimoja na ilikuwa nikuwafanya watu waelewane, wasikilizane na wala sio kwenda kinyume na hivyo.

Wanamuambia Mtume (s.a.w.w) hatujawahi kukusikia wewe Ukiongopa,Historia inatuambia Mtume huyu tunaekumbuka leo kuzaliwa kwake, alikuwa akijulikana kwa siku mbili muhimu, sifa ya ukweli na sifa ya uaminifu, Sifa ya Ukweli na Uminifu Mtume (s.a.w.w) ndani ya nchi ya Makka aliitwa na Waislam na wasiokuwa Waislam, sio waislam tu walimpa sifa hiyo.

Waislam na wasiokuwa waislam kwanini, kwasababu Mtume (s.a.w.w) katika Mafunzo yake ya Makka ilikuwa Watu wa Makka wawe kitu kimoja, ilikuwa jamii ya Makka iwe wamoja, naamini masomo haya, mafundisho haya na mahubiri haya leo hii sisi katika taifa hili la Tanzania tunayahitajia kwa kiasi kikubwa.

Katika kuunganisha jamii ya Makka, watu wa Makka waislam na wasiokuwa waislam amana zao, fedha zao, vitu vyao vilikuwa vikiwekwa nyumbani kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), kwa Ibara iliyokuwa nzuri nyumba ya Mtume ndio ilikuwa Benki ya Watu wa Makka, naamini ya kwamba ilikuwa umoja wa hali ya juu.

Umoja uliompelekea mtu anaeabudu sanam, mtu anaemuamini Nabii Issa / Yesu (a.s) kwamba ndio Mtume wake, mtu anaeamini Nabii Mussa (a.s) ndio Mtume wake na Taurati na Injiir ndio vitabu vyao lakini amana zake anaziweka nyumbani kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika kuwaunganisha watu kuwafanya kuwa Kitu kimoja alijitahidi kupambana na utumwa na kujaribu kuondoa utumwa  kwa hali na mali katika jamii, alijitahidi kuwaondoa wanaoitwa Watumwa, akajaribu kufunza mafunzo ambayo yataondoa Utumwa katika jamii ili watu wawe kitu kimoja.
Mtume akafunza kwamba kunyanganya  ni jambo halifai ambapo kwa kipindi hicho lilikuwa ni jambo la kawaida, utapeli ni jambo halifai, akafunza rushwa haifai, akafunza uharibifu haufai yote yalikuwa ni mafunzo yake, kwanini kwasababu yanalenga kuifanya umma, kuifanya jamii kuwa kitu kimoja.

Mtume Muhammad (s.a.w.w) akajitahidi jambo moja muhimu naamini leo linahitajika mmno kujaribu kunyanyua heshima na hadhi ya Mwanamke, Mwanamke alikuwa akionekana ni mtu wa daraja la pili,mtume akainyanyua hadhi ya mwanamke, mtume akafundisha hakuna Mfumo Dume ndani ya Uislam, mtume akafunza yakwamba mwanamke anayohaki ya kurithi kama vile anavyorithi mwanaume, mtume akafunza yakwamba mwanamke ni mmoja katika wanafamilia.


Mtume Muhammad (s.a.w.w) akafunza kuwa mwanamke anayohaki sawa kama vile mwanamume, mtume akafunza kuwa mwanamke anayohaki ya kumiliki kama vile anavyomiliki mwanaume, Mtume akafunza mwanamke anayohaki yakushiriki katika maamuzi, anayohaki ya kushiriki katika kupiga kura, anayohaki ya kuendesha gari lake. 

Haya ndio yalikuwa mafunzo ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika kuonesha na katika kuunganisha jamii.Na nizungumze jambo nzuri zaidi Mtume Muhammad (s.a.w.w) walikuwepo baadhi ya wanawake wakimtembelea akinyanyuka kwa sababu ya kwaheshimu wanawake hao, kwahivyo naamini ya kwamba mafunzo haya ya kuwaunganisha watu ya kuwafanya watu kuwa kitu kiomja na dhana ya mwanamke kama alivyoifundisha Mtume , naamimi ya kwamba ni funzo muhimu watanzania wote wanalihitajia.

Vilevile jambo nzuri la kupendeza Mtume Muhammad (s.a.w.w) akajaribu kutengeneza na sio tu kuunganisha watu Mtume alivuka zaidi ya hivyo, Mtume alivuka na akatengeneza udugu, yaani Mtume alitengeneza Umoja hakuishia hapo na akaingia kutengeneza udugu ikawa huyu ni ndugu wa huyu, Yule ni ndugu wa Yule yote kwa nini ni kuakikisha jamii yote inakuwa kitu kimoja.

Mtume Muhammad (s.a.w.w) alipohama kwenda madina, alipofika madina akaendelea na kazi hiyo hiyo akajitahidi kuunganisha katika ya watu waliohama kutoka makka kwenda madina, akajitahidi kuwaunganisha hawa wawe kitu kimoja, Mtume Muhammad (s.a.w.w) alijitahidi kuunganisha kati ya Makabila mawili yaliyokuwepo madina, kabila la AUS NA AZRAJ akayaunganisha makabila hayo na kuhakikisha yanakuwa kitu kimoja, 

si hivyo tu Mtume alipofika Madina akatengeneza umoja wa watu wa Madina, umoja huo ulikuwa unawakusanya Wakristo, unawakusanya Mayahudi na unawakusanya Waislam.

Mtume Muhammad (s.a.w.w) akatengeneza kamati ya amani ya kuwalinda watu wa Madina Waislam na Wasiokuwa Waislam, kamati ya kuwalinda Waislam, Wakristo, Mayahudi walioko katika ardhi ya Madina, Mtume Muhammad (s.a.w.w) akakaa meza moja na watu hawa anaotofautiana nao Kidini, Kifikra na Kimtazamo.

Kwa umuhimu wa kikao kile cha Amani na Maelewano na umoja kwa watu wa Madina ningependa kunukuu beti kama mbili au tatu katika vitabu vya kihistoria bakubaliano yanaandikwa kwa kusemwa “Haya ni makubaliano kutoka kwa Muhammad (s.a.w.w) Mtume wa Mungu baina ya Waumini na Waislam, kwa ibara nzuri Mtume (s.a.w.w) anawaita Mayahudi, anawaita Wakristo anawaita kwa jina la WAUMINI, 

kwahivyo makubaliano yake anasema ni kati ya Waumini na Waislam mpaka mwisho wa makubaliano.leo naamini mafunzo haya tunayahitajia, kwamba kumbe sisi tunaoamini Qu’an na wenzetu wanaoamini Injiir na wanaoamini Taurati na Zabuuri Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambae leo tunakumbuka kuzaliwa kwake hawa anawaita WauminiAnasema tena 

“ Na hakika Mayahudi wa Bani Aufu, hawa mayahudi na wanaowafuata mayahudi yani Wakristo na wengineo hawa wote ni waumii ni umma mmoja ni jamii moja, wao wanadini yao na waislam wana dini yao, kama kuna mtu alifundisha kuheshimiana katika dini, kuheshimu dini za watu basi Mtume Muhammad (s.a.w.w) atakuwa mtu wa kwanza na atakuwa anaongoza,

Mtume pia anasema “Kati ya mayahudi na wakristo wote walioko madina wao akishambuliwa Mwislam lazima wanyanyuke kumsaidia mwislam na mwislam watakapompata yahudi, watakapompata Mkristo anashambuliwa wao ni lazima na wao wanyanyuke wamsaidie Mkristo,” huyu ndio Mtume tunaemkumbuka leo hii,mtume wa huruma, mtume wa maelewano.

Mtume anasema tena “ yeyote atakaeishi hapa Madina  awe Mwislam awe Mkristo awe Myahudi yupo katika amani haya ndio makubaliano ya Mtume ambae tunakumbuka kuzaliwa kwake na tunamsheherekea Mtume aliefunza  hivi.aliewaunganisha watu hivi,
Nikimalizia nisema neon moja nzuri kwamba mafunzo yake yote Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika maisha yake yote yalikuwa yamegubikwa kwenye huruma,mtume alikuwa mtume wa huruma,


 akiwaonea huruma watu wa aina zote, kwa hivyo siku hii ya kuzaliwa mtume na siku hii ya Maulidi ya Mtume (s.a.w.w).Moja ya Mafunzo makubwa ya kujifunza ni sisi kama watanzania kupambika na huruma ya Mtume (s.a.w.w), yule unaetofautiana nae Kidini, Kirai na Kifikra umuonee huruma sio uwe na roho mbaya dhidi yake, yule ambae unamuona hayuko katika dini yangu yupo katika dini nyingine, wewe wajibu wako kwa kumfuata Mtume ni kumuonea huruma.

Mtume Muhammad (s.a.w.w) hakufunza ukatili, Mtume hakufunza chinjachinja, mtume hakufunza kukunja uso, mtume hakufunza roho mbaya, yoyote anaekuambia mtume amefunza roho mbaya, mtume amefunza chinjachinja, mtume amefunza kukunja uso, huyo bado hajamuelewa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Mwenyezimungu anasmea katika Qur’an kumuambia Mtume Muhammad (s.a.w.w)

 “wewe umekubalika kwa sababu ya huruma uliyokuwa nayo” ndio maana Waislam, Mayahudi na Wakristo walikuwa wakihifadhi amana zao nyumbani kwa Mtume.Katika mafunzo aliyofunza Mtume yalikuwa ni Mapenzi, ni mahaba , ni upendo, maelewano, masikilizano, kumpenda jirani yako ndicho mtume alichofunza, Mtume alifunza waislam kupendana wenyewe kwa wenyewe, Mtume alifunza Waislam kupendana na Wasiokuwa Waislam,

 mtume alifunza kuwapenda mafakiri, alifunza kuwapenda masikini, alifunza kuwapenda wajane, alifunza kuwapenda mayatima
Alifunza kuwapenda watu wanaoishi katika mazingira magumu, alifunza kuwapenda kila watu wenye aina yoyote ya matatizo, hayo ndio yalikuwa mafundisho yake katika maisha yake, Mtume alifunza kusaidiana, Mtume alifunza ukarimu, Mtume alifunza kuvumiliana hata kwa mtu mnaetofautina Kidini na kifikra.

Mtume anawaambia anawaambia waabudu Masanam “Nyie mnadini yenu,na mimi nina dini yangu” ndivyo mtume alivyofunza akatufundisha ya kwamba “Hakuna kulazimishwa mtu katika dini” yaani hakuna kumlazimisha mtu kuifuata dini, jambo la kufuata dini ni jambo la kukinaika na kuridhia kwa mtu mwenyewe binafsi, mafunzo haya leo yanahitajika.Mtume alifunza kuishi kwa usalama, kuishi pasina mivutano, kuishi pasina misuguano, haya ndio yalikuwa mafunzo yake. 

Mwisho ni wito wetu kwa Watanzania kwa siku hii ya kuzaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Kama mafunzo ya mtume yalikuwa ni huruma, siku hii ya kuzaliwa mtume tunatoa wito kwa watanzania wawe na tabia ya kuhurumiana, matajiri wawahurumie masikini, wenye nacho wawahurumie wasiokuwa nacho, wenye elimu wawahurumie wasiokuwa na elimu, wenye uwezo wawaahurumie wasiokuwa na uwezo.

Katika siku hii ya Maulidi moja ya ujumbe muhimu tuubebe ni upendo na maelewano aliyoyafunza Mtume Muhammad (s.a.w.w) tuondoke na somo la maelewano kama watanzania, tupendane,hakuna sababu ya sisi kubaguana kwa sababu mitume wetu wote walikuja kufunza maelewano, mitume wetu wote walikuja kufunza kusikilizana, mitume wetu wote walikuja kufunza kuvumiliana, mitume wetu wote walikuja kufunza mtu aipende nchi yake, mtu kuwapenda watu wake, 

kupenda nchi yako ni katika imani.Hayo ndio mafunzo yaliyofunzwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w) na ninaamini ndio mafunzo  yaliyofunzwa na Nabii Issa / Yesu (a.s) na ndio mafunzo ya Nabii Mussa / Mosses (a.s), na ndio mafunzo ya Yohana na ndio mafunzo ya Mitume wote wa Mwenyezimungu (swt), katika siku hii ya Maulid turudi katika mambo hayo.

Mwisho niseme dini za mungu zimekuja kufunza amani, zimekuja kufunza utulivu, “Wewe mungu wewe ni amani” mungu mwenye anaeabudiwa na Waislam, anaeabudiwa na Wakristo, anaeabudiwa na Mayahudi, anaeabudiwa na Majusi mungu huyo anaitwa amani, “na wewe mungu kwako inatoka amani na kwako vilevile inarudi amani, “Mungu tufanye hapa Tanzania, na duniani kote tunaishi kwa amani.

Mitume wote wa Mwenyezimungu wamekuja kufunza amani, na Mungu tunakuwanae ni Mungu wa Amani, si Mungu wa Vita, si Mungu wa mivutano bali ni Mungu wa Amani na Masikilizano, Mungu tunakuomba utupe amani ya nchi yetu, Tanzania uzidi kuiboresha na kuifanya ni kisiwa cha amani na kisiwa cha masikilizano, uzidikuwafanya watanzania hawajui kubaguana kwa sababu ya dini zao, wabakie ni ndugu, 

wanasikilizana,wanaelewana, Mwenyezimungu tunakuomba vilevile Viongozi wan chi yetu, Utawala tuliokuwa nao Mungu uwape Hekima,busara, Utulivu waweze nao wawe ni chachu kuendeleza amani  tuliyokuwanayo, na watuongoze kwa busara na utulivu mpaka mwenyezimungu utakapoturudisha kwako.

Asanteni sana na hongereni Watanzania wote kwa kuzaliwa Kiongozi wa watu wote wa huruma, upendo na maelewano Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Imetolewa Na:
Kiongozi Mkuu wa Waislam Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala
10-12-2016, Jumamosi.

Monday, December 12, 2016

Ayatullah Larijani: Kulindwa umoja ni jukumu la kidini na kiakili la Waislamu

Mkuu wa Vyombo vya Mahakama nchini Iran amesisitiza juu ya kufanyika juhudi kadiri inavyowezekana kwa ajili ya kulinda umoja na mshikamano baina ya Waislamu na kusimama kidete mbele ya mabeberu.

Ayatullah Sadeq Amoli Larijani amesema hayo leo katika kikao cha maafisa wa ngazi za juu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama na kusisitiza kwamba, hii leo Ulimwengu wa Kiislamu unahitajia umoja na mshikamano zaidi kuliko wakati wowote ule hivyo kuna haja ya watu wote kufanya juhudi kwa ajili ya kulinda umoja huo.

Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama nchini Iran amesema kuwa, kuzusha mifarakano ni sera za maadui wa Uislamu na kubainisha kwamba, miamala ya madola ya Kiistikbari inaonyesha kuwa, iko tayari kufanya chochote kwa ajili ya kuzusha mifarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu na siku zote madola hayo yamo mbioni kudhoofisha Waislamu sambamba na kupenya na kuwa satuwa katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Ayatullah Sadeq Amoli Larijani ameongeza kuwa, njia pekee ya kukabiliana na siasa hizo za kikoloni ni kuongezwa kiwango cha ufahamu na kumtambua adui baina ya Waislamu.
 
Amesema, kuwalingania watu umoja ni jukumu la watu wote wenye vipaji, maulama na wasomi wa Ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa, jinai za maadui wa Uislamu nchini Yemen, Iraq, Syria, Afghanistan na kwingineko ni ishara kwamba, uistikbari wa dunia unataka kuangamiza kizazi cha mwanadamu.

Sunday, December 4, 2016

“Waelezeni watu Uislam wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni Uislam wa Huruma” Sheikh Jalala

Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala akisisitiza jambo juu ya Uislam wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuwa ni Uislamwa Huruma.
TAARIFA KWA UMMA WA KIISLAM
Sikuambii Huruma ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwa Waumini wa Kiislam mpaka akafikia mahala akasema “Yoyote mwenye kukiri Mungu ni Mmoja, mtu huyo ataingia peponi”hii ndio huruma ya Mtume (s.a.w.w) na Uislam aliotuletea.

Sasa ndugu yangu wewe unapata wapi fatua, unapata wapi Rai, unapata wapi Aya na Hadith za kumuambia mwenzako huyo ni Mtu wa Motoni wakati anasema Lailaha ilallah (Hakuna Mola apasaekuabudiwa ila Allah) Fatwa hiyo umeipata wapi?

Ni kwa mantiki gani unaetoa fatua ya kuuwawa Yule ambae unaetofautiana nae na yeye anasema Lailaha ilallah (Hakuna Mola apasaekuabudiwa ila Allah) Fatwa hiyo umeipata wapi?

Unapata ujasiri upi wa kuchukua mkono wako ukamuua mtu anaesema Lailaha ilallah (Hakuna Mola apasaekuabudiwa ila Allah)ujasiri  huo umeupata wapi?

Unatoa kwenye Qur’an gani fatua ya kuvaa bomo kwenda kulipua ndani ya Msikiti watu wanaosema Lailaha ilallah (Hakuna Mola apasaekuabudiwa ila Allah) Fatwa hiyo umeipata wapi?

Uislam wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) bado haujulikani, Mnayo kazi ya kuwaeleza watu Uislam wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuwa ni Uislam wa Huruma.

Imetolewa na
Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala.
Ijumaa, 02-12-2016.





Thursday, December 1, 2016

"Yoyote ambae anafikra ya kwamba Uislam ni dini ambayo haina huruma huyo atakuwa hajautambua Uislam",-Sheikh Jalala.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
MAADHIMISHO KIFO CHA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W) MWEZI 28, SAFAR 1438.

Napenda kuanza na mazungumzo yangu katika Qur’an Mungu ansema “Hatujakutuma ewe Muhammad (s.a.w.w) ila ni huruma kwa viumbe wote” siku hii ya leo ya mwezi 28,mfungo tano kwa kalenda ya Hijiria ndio siku ambayo Kiongozi wa watu wote duniani, kiongozi wa Waislam Mtume  wetu Muhammad (s.a.w.w) ndio ameaga dunia.

Weusi huu mnaouona, matembezi haya ya amani mnayoyaona yote ni kwasababu ya kukumbuka kifo cha mtukufu na mtakatifu Mtume Muhammad (s.a.w.w), Lakini lakujiuliza kubwa ni kwanini mtu huyu tumkumbuke katika kifo chake, zaidi ya miaka 1400 iliyopita. 

Sababu kubwa ya kukumbuka kifo cha Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuna sababu nyingi mmno, lakini niseme sababu mbili tatu kwa harakaharaka, Sababu ya kwanza kama anavyosema Mwenyezimungu katika Qur’an kwamba “Wewe tumekutuma ukawe ni huruma kwa watu wote” sio huruma kwa Waislam, 

Sasa unapomuangalia Mtume Muhammad (s.a.w.w) wakati bado yupo hai, akiwa yuko katika mji wa makka na baada ya kuwa madina, tulimpata mtume alikuwa na huruma kwa watu wote, mtume alikuwa huruma kwa wasiokuwa waislam, mtume alikuwa na huruma kwa waislam, mtume alikuwa huruma kwa wtu waliokuwa wanaabudu masanamu, kwa watu waliokuwa wanaabudu lata, wanaabudu manata na wanaabudu hubal,
Kiongozi Mkuu wa Waislam Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala akiongea na Waandishi wa Habari katika Matembezi ya Amani ya Kuadhimisha Kumbukumbu ya Kifo cha Mtume Muhammad (s.a.w.w) Kigogo Round About, Leo Jijini Dar es salaam.Ambayo yalianzia Ilala Boma hai Uwanja wa Pipo Kigogo.

 hawa walikuwa ni waungu wakiabudiwa na warabu, lakini mtume aliishi vizuri na alikuwa ni huruma kwa watu hao, mpaka amana za watu hao aliziweka katika  nyumba yake,
Mtume alipokuwepo maka na madina vilevule alikuwa na huruma kwa Ahlulkitab / Wakristo, yaani alikuwa ni huruma kwa Wakristo, alikuwa na huruma kwa mayahudi na alikuwa ni huruma kwa watu wenye dini zote.

Naamimi ya kwamba huruma hii aliyokuwa nayo Mtume Muhammad (s.a.w.w) kabla hajaondoka duniani, naamini ya kwamba Watanzania na walimwengu huruma hii wanaihitajia.
Leo hii tunapotembea matembezi haya ya amani kwa ajili ya kukumbuka Mtume Muhammad (s.a.w.w) kifo chake, kubwa la kulienzi ni hili la Huruma ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) inahitajika na ni muhimu, 

Naamini yakwamba Watanzania wote wanahitajia huruma aliyokuwa nayo mtume, huruma ambayo haikumfanya Mtume asiwapende wasiokuwa waislam.

Huruma ambayo ilimfanya mtume akae meza moja na Wakristo katika ardhi ya madina, Huruma ambayo ilimfanya Mtume akae meza moja na Mayahudi, huruma ambayo ilimfanya Mtume akae na Wakristo / Ahlulkitabu.

Naamini yakwamba leo hii Waislam watanzania Masheikh na Maimam na Maustadhi wanayonafazi kubwa yakumuenzi Mtume katika kukaa kwao na Wachungaji, wao na Maaskofu, wao na Mapari, wao na wenzi wao ambao wanatofautiana nao kidini, Naamini ya kwamba Matembezi haya yawe ni chachu yakuwafanya watanzania wote waiige huruma ya Mtume,

 ambayo huruma hiyo ilikuwa haimbagui mtu, huruma hii leo hii inahitajika mahala pakubwa.Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikuwa ni huruma kwa watu wote kwanini kwasababu alikuwa na huruma na watu.

Jambo la pili Mtume ambae tunamkumbuka leo hii, ni mtume alieng’ang’ania na alieenzi Umoja kabla ya mtume hajaondoka makka alitengeneza umoja kati ya maswahaba wake, na alipoondoka makka kwenda madina vile vile akatengeneza umoja kati ya wakazi wa madina (Answar) na kati ya watu waliotoka Makka(Muhajirun).

Akatengeneza Umoja kati ya makabila mawili yaliyokuwa yanavutana kabila la Ausi na Azraj, akatengeneza umoja wa Kidini ndani ya ardhi ya madina,naamimi ya kwamba leo hii, uwepo wa umoja wa Kidini ndani ya ardhi ya Tanzania,kipindi hiki ambacho huruma imekosekana , 

kipindi ambaho kuvumiliana kumekosekana, naamimi ya kwamba mafunzo haya Mtume Muhammad (s.a.w.w) yanahitajika leo hii kwa Watanzania na watu wote bila ya kuwabagua waislam wala wakristo wote wanahitajia umoja huu, wanahitajia kuishi huku kwa pamoja ameyoyafunza Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Nimalizie kwa kusema yoyote ambae anafikra ya kwamba Uislam ni dini ambayo haina huruma huyo atakuwa hajautambua  Uislam, yoyote ambae anafikiria ya kwamba Mtume alikuwa ni mtu wa Misimamo ya kutisha ambayo hawezi kukaa na watu hayo hajamtambua Mtume. 

“Kwasababu ya huruma uliyokuwa nayo ewe Muhammad (s.a.w.w) watu wote wameweza kukukubali, umeweza kukaa na Wakristo, umeweza kukaa na Mayahudi,umeweza kukaa na Mapagani na umeweza kukaa na watu wa aina zote”

Jambo la Mwisho Mtume Muhammad (s.a.w.w) kama alivyoenzi Umoja, ulienzi utulivu, alienzi maelewano na alienzi amani, na ninaamini yakwamba Tanzania leo hii inayohaja kubwa yakuenzi Utulivu, yakuenzi Amani, yakuenzi Mshikamano watu kukaa pamoja, tofauti zetu za kifikra na za kimtazamo zisitufanye kutokuwa wamoja.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki wanadini wote walioko Tanzania, wabariki Viongozi wa Dini wahubiri Upendo, Maelewano, Mshikamano pamoja na Amani katika nchi hii,Vilevile Viongozi wetu na Serikali ambayo inatusimamia katika mambo yetu. 

Imetolewa na:
Kiongozi Mkuu wa Waislam Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala
30-11-2016,Jumatano.