Wednesday, August 19, 2015

UTAFITI WA AFYA YA UZAZI NA MTOTO NA MALARIA KUANZA RASMI TAREHE 21 AGOSTI, 2015

 
Mgeni rasmi, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Dkt. Ahmed Makuwani kutoka Wizara ya Afya na Usitawi wa Jamii akiwahutubia Wasimamizi, Wahariri na Wadadisi wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015 wakati wa hafla fupi ya kufunga mafunzo ya utafiti huo iliyofanyika leo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Wito umetolewa kwa viongozi wote wa Serikali katika Ngazi zote na wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa Wasimamizi, Wahariri na Wadadisi wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria utakaoanza rasmi tarehe 21 Agosti, 2015.
 
 Wito huo uletolewa leo na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Ahmed Makuwani wakati wa hafla fupi ya kufunga mafunzo ya utafiti huo iliyofanyika wilayani Moshi, Kilimanjaro.
 
“Ninawaomba Wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Wadadisi, Wasimamizi na Wahaririwatakaoshiriki zoezi la kukusanya Takwimu za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria wa mwaka 2015 ili kupata taarifa muhimu na sahihi kwa ajili ya kupanga Mipango na Sera endelevu za Sekta ya Afya katika nchi yetu, amesema Makuwani”.
 
Dkt. Makuwani amesema kuwa taarifa zitakazokusanywa kwa wananchi kwa ajili ya  utafiti huo zitakuwa ni siri na zitatumika kwa shughuli za Kitakwimu tu na wala hazina uhusiano wowote na Uchaguzi mkuu wa Mwaka huu.
 
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akielezea umuhimu waUtafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015 wakati wa hafla fupi ya kufunga mafunzo ya utafiti huo iliyofanyika leo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema utafiti huu wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria wa mwaka 2015  unalenga kukusanya taarifa nyingi za sekta ya afya zinazotumika katika kutathmini malengo mbalimbali na pia kusaidia katika kupanga mikakati mipya.
 
Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa mara nyingine tena inafanya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria wa mwaka 2015 ambao kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2010. Utafiti huu utaanza rasmi tarehe 21 Agosti, 2015 kwa nchi nzima na utamalizika mwishoni mwa Mwezi Februari 2016.source.Fullshagwe

No comments: