Tuesday, June 6, 2017

Makamu wa Rais afanya ziara serengeti na haya ndio ameyasema

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Mbuzi Mugumu Serengeti ikiwa sehemu ya kukamilisha ziara yake ambapo alitumia fursa hiyo kuwashukuru wakazi wa Serengeti na kuwapongeza kwa kutunza mazingira
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameuagiza uongozi wa wilaya ya Serengeti na wa mkoa Mara kukamilisha haraka awamu ya kwanza ya ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo ili kuondoa adha ya wananchi kusafiri kwenda mikoa ya jirani ya Arusha na Mwanza kwenda kupata huduma afya.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo leo 6-June-2017 kwenye mkutano wa hadhara mjini Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara mara baada ya kutembelea ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya  na kuweka jiwe la msingi.

Makamu wa Rais amesema kutokana na wilaya ya Serengeti kupata wegeni wengi kutoka nje ya nchi ambao wanaenda kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti  hivyo ni muhimu kwa viongozi wa wilaya na mkoa kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo kukamilisha ujenzi huo haraka ili wananchi waweze kupata huduma za afya za uhakika katika wilaya yao.

Makamu wa Rais amesema kukamilika kwa ujenzi huo wa awamu ya kwanza kutaondoa taabu kubwa wanayopata wananchi wa wilaya ya Serengeti katika kupata huduma ya afya karibu na maeneo yao.

Katika kuunga mkono jitihada hizo za ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Serengeti, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ameahidi kuchangia kiasi cha shilingi milioni Tano na amewaahidi wananchi wa wilaya ya Serengeti kuwa atakikisha fedha kutoka Serikalini ambazo zinatakiwa kupelekwa wilayani humo zinapelekwa haraka ili kukamilisha ujenzi huo.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan pia amewataka wananchi kote nchini kuunga mkono jitihada za Serikali za kupambana na rushwa na ufisadi ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa na manufaa kwa wananchi wote.

No comments: