Tuesday, November 18, 2014

'Daesh inakiuka Uislamu na ubinaadamu


Wanamgambo wa kikundi cha Daesh wakiwaua watu bila kuwa na makosa.

Serikali ya Morocco imeitaka jamii ya kimataifa kupambana vilivyo na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Ripoti iliyotolewa leo na Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco imesisitiza kuwa, vitendo vinavyofanywa na kundi hilo ni kinyume kabisa na misingi ya dini ya Kiislamu na ni kinyume na ubinaadamu.

Sanjari na kulaani mauaji ya Peter Kassig, aliyekuwa akishikiliwa na wanachama wa kundi hilo la kitakfiri linalofanya jinai kwa jina la Uislamu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco imetaka kuzidishwa juhudi katika mapambano dhidi ya kundi hilo. 

Jana kundi hilo lilisambamba mkanda wa video ulioonyesha kuuawa Peter Kassig. Peter alitekwa nyara na kundi hilo mwaka jana nchini Syria na kupelekwa kusikojulikana. 

Kwengineko Wizara ya Ulinzi nchini Iraq, imetangaza kupinga mpango wowote wa Marekani kwa kuingia kijeshi kwa ajili ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa wanachama wa Daesh. Khaled al-Obeidi, Waziri wa Ulinzi wa Iraq amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo ndilo litakaloukomboa mji huo bila kuhitajia msaada wa Marekani. 

Hayo yanajiri katika hali ambayo viongozi kadhaa wa Iraq, wametangaza upinzani wao juu ya mpango wa Marekani kutuma askari wake wengine kwa ajili ya kupambana na kundi hilo, wakisema kuwa hatua hiyo ni uvamizi mwengine wa Washington dhidi ya ardhi yao. 

Baadhi wamenukuliwa wakisema kuwa, operesheni za Marekani nchini Iraq dhidi ya Daesh, itakuwa na matokeo mabaya kwa taifa na watu wa Iraq.

Mujuru atuhumiwa kutaka kumuua Rais Mugabe


Joice Mujuru Makamu wa Rais wa Zimbabwe

Joice Mujuru Makamu wa Rais wa Zimbabwe anakabiliwa na tuhuma za kutaka kumuua Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo. Gazeti la Sunday Mail linalochapishwa Zimbabwe limeandika katika toleo la jana kwamba, 
Bi. Joice Mujuru pamoja na wasaidizi wake wawili wanahusishwa kwenye njama za kutaka kumuua Rais Mugabe aliyeiongoza nchi hiyo tokea ilipojipatia uhuru wake mwaka 1980. 
 
Hayo yanajiri katika hali ambayo, mirengo ya kisiasa ndani ya chama tawala cha ZANU PF inafanya juhudi ya kupata satua na ushawishi mkubwa kwa wanachama wa chama hicho, kabla ya kufanyika mkutano mkuu uliopangwa kuitishwa mwezi ujao. 

Bi Joice Mujuru amekuwa akishirikiana bega kwa bega na Rais Mugabe kwa kipindi kirefu, lakini katika miezi ya hivi karibuni amekuwa kwenye malumbano makali ya kisiasa na Grace Mugabe, mke wa Rais Robert Mugabe. 

Grace Mugabe amekuwa akimtuhumu Joice Mujuru Makamu wa Rais kwa kupanga njama za kumpindua Rais Mugabe. 

Vita vya kugombania madaraka ndani ya chama tawala vimeshadidi baada ya Grace Mugabe ambaye ni mkuu wa umoja wa vijana wa chama tawala, kupata uungaji mkono mkubwa kutoka kwa Emmerson Mnangwaga mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa ndani ya chama tawala cha ZANU PF. 

Tuesday, November 11, 2014

WAISLAM WA MADHEHEBU YA SHIA ITHNA ASHARIYYAH WAMEADHIMISHA MAOMBOLEZO YA IMAM HUSSEIN (A.S), TANDIKA BILAL , JIJINI DAR ES SALAAM.

Viongozi wa taasisi mbalimbali wakiwa katika Maandamano ya Maombolezo ya kifo cha mjukuu wa Mtume (s.a.w.w), yaliyofanyika leo katika Msikiti wa Bilal Tandika,jijini Dar es Salaam,Tanzania.
 
Imam Hussein AS akizungumza Makka alisema: "Ewe Allah! Unajua kile ambacho tunakifanya katika jamii si kwa sababu ya kupata mamlaka na utawala na wala si kwa ajili ya kupata utajiri. Sisi tunataka kuonyesha njia ya dini yako, tufanye marekebisho katika miji yako, waja wako waliodhulumiwa waishi katika utulivu na usalama na waweze kukutii Wewe pasina bughudha. Sisi tumeazimia kutekeleza yaliyofaradhishwa katika Uislamu, Suna ya Mtume SAW na sheria za Allah."

Imam Hussein AS alianzisha mapambano yake ili kutenganisha baina ya haki na batili. Alifahamu kuwa nguvu za utawala wa Yazid ulikuwa umejengeka katika misingi ya batili na iwapo ungeendelea hivyo, basi kungeshuhudiwa kuangamia kazi zote za mitume za kueneza uadilifu na ukweli. Kwa hivyo katika vikao vyake tafauti mtukufu huyo alifafanua na kuweka wazi haki na batili.

Maombolezo ya Kifo cha Imam Hussein (a.s), yamefanyika leo Tandika katika Msikiti wa Bilal, Maombolezo hayo yameudhuliwa na watu mbalimbali wakiwemo Wanawake kwa Waume.
Moja ya sababu nyingine za kudumu harakati adhimu ya Karbala ni uwazi wa mwamko huo. Imam Hussein AS wakati akianzisha mapambano yake makubwa, awali kabisa alibainisha utambulisho wa mapinduzi yake  kwa njia ya wazi kabisa. Aliwafahamisha watu kuwa mapamabano yake yalilenga kupinga dhulma na kuhuisha Uislamu sambamba na kuwaokoa watu kutoka katika shari ya utawala wa Yazid. Alibainisha hata mbinu za mapambano ambazo zilipaswa zitumike.

Kijana wa Hawza ya Bilal, akiongoza Masira kwa nyimbo za huzuni juu ya Imam Hussein (a.s).
Tokea kuumbwa Adam kulikuwepo mapambano baina ya haki na batili na vita vingi katika historia ya mwanaadamu vilijiri kwa ajili ya hayo mawili. Katika kipindi muhimu zaidi, Imam Hussein AS alijitokeza kama mbeba bendera ya haki alipokabiliana na Yazid ambaye alikuwa mbeba bendera ya batili. Ili kulinda haki na kuweka wazi njia yake hadi siku ya qiyama, Imam Hussein AS, familia yake pamoja na wafuasi wake watiifu; wote kwa pamoja walitoa maisha yao muhanga. Ashura ni kielelezo cha vita vya daima baina ya haki na batili na thamani bora dhidi ya upotofu.

Ashura ni tukio ambalo imepita miaka 1373 tokea kujiri kwake lakini si tu kuwa tukio hili la kihistoria linawavutia Waislamu bali pia wapenda uhuru kote duniani wamevutiwa na yaliyojiri katika jangwa la Karbala.
Katika kipindi chote cha historia, kumejiri matukio mengi ambayo akthari yamesahaulika. Lakini tukio la Karbala ni la aina yake kwani tokea kujiri kwake hadi sasa limekuwa likivutia hisia za wengi na kuleta nuru katika nyoyo zilizokuwa kizani.
Siku ya 10 ya mwezi Muharram mwaka 61 Hijria Qamariya, kilio cha Imam Hussein AS na wafuasi wake cha kutaka haki kimebakia na kudumu katika kurasa historia. Leo kilio cha Imam Hussein AS kimewafikia watu wenye kiu cha kusikia kilio cha haki. Tuko katika siku za kukumbuka kuuawa shahidi Mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS na wafuasi wake katika jangwa la Karbala.

Monday, November 3, 2014

kumlilia Imam Hussein (a.s) inaruhusiwa

Wanawake wakimlilia Imam Hussein (a.s) aktika siku za ASHURA.







Hapana shaka kwamba kuwalilia wafu Waumini ni jambo linalofaa katika Uislamu kutokana na dalili ya kitendo cha Mtume (s.a.w.w) kuhusu jambo hilo.

Siku Mtume (s.a.w.) alipozuru kaburi la mama yake Bibi Amina, alilia kiasi cha kuwaliza watu waliokuwa karibu yake, siku alipofariki ami yake na mlezi wake Bwana Abu Talib, siku alipouawa kishahidi ami yake Mtume Bwana Hamza katika vita ya Uhud 


Siku alipofariki Bwana Ibrahim ambaye ni mtoto wake mwenyewe Mtume (s.a.w.w). Mtume (s.a.w.w) alimlilia mwanawe huyu kiasi ambacho kilimfanya Bwana Abdurahman bin Auf amwambie Mtume (s.a.w.w): "Na wewe unalia Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu"? Bwana Mtume (s.a.w.w) akasema: "Ewe mwana wa Auf hiyo ni alama ya huruma".


Alipotimia Imam Husein umri wa miaka miwili Mtume alitoka kufanya safari na katika safari yake hiyo alisimama mahali fulani, basi aliamua kutoendelea na safari yake na mara macho yake yakawa yanabubujika machozi, akaulizwa sababu gani iliyomfanya alie. Mtume (s.a.w.) akasema: 


"Jibril ananieleza kuhusu ardhi iliyoko kando ya mto Furat iitwayo "KARBALA" mahala ambapo atauawa mwanangu Husein, sasa hivi ni kama nauona uwanja wa mapambano baina yake na adui zake, pia kama kwamba napaona mahala atapozikwa.


Kisha baadaye Bwana Mtume (s.a.w.) aliamua kurudi hali ya kuwa mwenye huzuni na majonzi, akapanda katika Mimbari na akatoa khutba huku Hasan na Husein (a.s.) wakiwa mikononi mwake.

Hawza Imam Jafari Swadiq wasafisha Barabara

Sheikh Hemed Jalala akiwapungia mkono wanannchiwa kigogo, jijini Dar es salaam, kulia kwake ni Sheikh Zuberi Kabwe

Sheikh Hemed Jalala akionesha mfano wa kufanya usafi katika maendeo ya barabarani, kigogo

Sheikh Hemed Jalala akiwa ana Wanaharaati wake maeneo ya kigogo wakikusanya uchafu

Sheikh Hemed Jalala akielekea katika eneo la usafi bunde baada ya mvua kunyesha

Sheikh Hemed Jalala akiongoza msafara kwenda kuanza usafi.







Hawza Imam Jafar Swadiq chini ya Sheikh Hemed Jalala katika kukukmbika kifo cha Mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambaye ni Imam Hussein (a.s) wamefanya shughuli mbali mbali za Kijamii kama Kuwatembelea Wafumgwa, ambapo walikwenda katika Mahabusu ya Watoto Upanga, Dar es salaam, Kusafisha Barabara na Kujitolea Damu katika Hospitali ya Muhimbili

Thursday, October 30, 2014

Hawza Imam Jaafar Swadiq yatembelea Mahabusu ya Watoto


Meneja wa Hawza ya Imam Jafar Swadiq Chini ya Sheikh Hemed Jalala, amewataka watu kutoa misaada ya hali na mali kwa watu wanaoishi Magerezani kwa kuzingatia wao ni Binaadam wanahitaji mahitaji kama watu walio huru.

Hayo yamesemwa leo na Sheikh Salim Mwamba wakati walipotembelea Mahabusu ya Watoto, Upanga Jijini Dar es salaam, wakikumbuka kifo cha Mjukuu wa Mtume Imam Hussein (a.s).

 “Sio kila aliye Gerezani ni mkosa,kwani wao wanahitaji huduma za kijamii kama chakula na mavazi kama watu walio huru” alisema sheikh Mwamba.

“Imam Hassan Askari na Nabii Yusuph walifungwa Gerezani na hali ya kuwa hawana makosa”ameongeza Sheikh Mwamba.

Sheikh Mwamba amewataka askari magereza kuwa na moyo wa ubinaadam, kwa kuwatendea Haki na Uadilifu wafungwa waliopo gerezani kwa kuwa ni watu kama wao na wanamahitaji kama yao.

Wanaharakati wa Imam Jafar Swadiq wanafanya shughuli mbalimbali za kijamii kama Kusafisha Makaburi, Kutembelea magereza, kusafisha barabara na kujitoea damu, kwa ajili ya kuadhimisha kifo cha Mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambaye ni Imam Hussein ibn Ali.


Imam Hussein (a.s) alizaliwa tarehe 15, mwezi wa Shaaban Mwaka 4 A.H na Fatma bint wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Amirul Muuminina Ally na aliuwawa tarehe 10 Muharram katika mji wa karbala nchini Iraq.