Monday, January 30, 2017

5 wauawa kwa risasi kwenye hujuma dhidi ya msikiti Quebec, Canada

Kwa akali watu watano wameuawa katika hujuma ya kikatili dhidi ya msikiti mmoja katika mji wa Quebec nchini Canada usiku wa kuamkia leo.

Mohamed Yangui, Rais wa Kituo cha Kiutamaduni cha Kiislamu mjini Quebec amesema waumini watano wa Kiislamu waliuawa walipokuwa wakisali Sala ya Ishaa jana usiku, baada ya wavamizi kuvamia msikiti huo na kuwamiminia risasi ovyo. Ameongeza kuwa, watu kadhaa wana majeraha ya risasi kufutia hujuma hiyo ya kinyama.

Polisi katika eneo hilo inadai kuwa imewakamata washukiwa wawili wa hujuma hiyo na kwamba yumkini mmoja amefanikiwa kutoroka.
Nje ya msikiti mjini Quebec, Canada
Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amelaani shambulizi hilo dhidi ya msikiti na kulitaja kama hujuma ya kigaidi dhidi ya Waislamu. 

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Trudeau amesema: "Tunalaani hujuma hiyo dhidi ya pahala pa kutekelezea ibada na kimbilio la waumini, kitendo hiki ni cha kioga na serikali inatoa mkono wa pole kwa wahanga wa hujuma hii, na tuko tayari kutoa msaada wa aina yoyote kwa familia za wahanga hawa."

Kituo cha Kiutamaduni cha Kiislamu mjini Quebec kimekuwa kikilengwa na watu wenye misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu mara kwa mara. Mwezi Juni mwaka jana wakati wa Ramadhani, watu wenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu waliacha kichwa cha nguruwe katika mlango wa msikiti huo.

Aidha mwaka 2015, msikiti mmoja katika jimbo la Ontario nchini Canada uliteketezwa moto na watu wenye misimamo ya kurufutu ada wanaouchukia Uislamu.

Rouhani: Iran sio nchi yenye hofu na chuki kwa wageni

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itatumia muamala na uhusiano wake mzuri na nchi zingine kwa maslahi na manufaa ya taifa hili.

Akizungumza katika kaburi la Imam Khomeini, Muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 38 ya Mapinduzi ya Kiislamu, Rais Rouhani amesema: "Wananchi wa Iran sio watu wenye chuki na hofu kwa wageni, sisi ni Waislamu na wananchi wa kimapinduzi."

Dakta Rouhani amebainisha kuwa, njia ya Imam Khomeini MA, ni njia ya kuelekea kwenye kilele cha uhuru wa kweli huku akisisitizia umuhimu wa kufuata njia hiyo.
Mosalla mjini Tehran
Kadhalika Rais Rouhani ametoa mkono wa pole kwa familia za mashahidi wa kikosi cha zimamoto waliopoteza maisha  katika tukio la kuungua na kuporomoka jengo la kibiashara la Plasco jijini Tehran hivi karibuni, ambao wanazikwa hii leo.

Shughuli za kuaga miili ya wazima moto hao 16 zinafanyika katika Msikiti wa Mosalla hapa Tehran, kabla ya kwenda kuzikwa katika maziara ya Behesht-e-Zahra.

Imam wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran Ayatullah Mohammad Emami Kashani anatazamiwa kuongoza suala ya maiti ya mashahidi hao. Jengo la kibiashara la Plasco mjini Tehran liliungua moto na kisha kuporomoka Januari 19, ambapo makumi ya watu walipoteza maisha.  

Friday, January 20, 2017

Waziri wa habari,utamaduni,Sanaa na Michezo Mh Nape Nnauye amemshukru Mwanariadha Simbu kuja na Medani

Kinara wa Standard Chartered Mumbai Marathon  ambaye pia ni Balozi wa Kampuni ya Multicjoice Tanzania wakwanza kulia Mr. Alphonce Simbu
Na: Amina Kibwana

Kinara wa Standard Chartered Mumbai Marathon  ambaye pia ni Balozi wa Kampuni ya Multicjoice Tanzania Alphonce Simbu amewasili jijini dar es salaam na kueleza yaliyojiri katika mbio hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa habari,utamaduni,Sanaa na Michezo Mh Nape Nnauye ametoa shukurani zake kwa Multichoice Tanzania ambao ni  wafadhili wa mwanaridha huyo kwa msaada waliompatia pamoja na  pongezi za dhati kwa mwanaridha huyo kuchukua ushindi katika mashindano hayo ambayo yalikuwa na washindani kutoka nchi tofautitofauti, 
"Ninawashukuru sana dstv kwa kujitolea kwao pale wanapoona kunafaa kwani mafanikio ya Simbu yamepatikana kwa kupitia msaada huo na kuufanya mchezo huu kurudi tena kwa kasi nchini kulinganisha na awali."
Naye Katibu Mkuu  wa chama cha riadha Nchini Willelm Gidabuday amesema kuwa waliamchagua Alphonce kwa kuamini kuwa nanweza na atafanya vizuri katika mchezo huo na kuweza kuiwakilisha vizuri Nchi yetu kutokana na kuweza kufanya vizuri katika mashindano yaliopita.
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Multichoice Tanzania Ronald  Shelukindo amesema kuwa wanaendelea kumdhamini Simbu na kwamba wanatarajia kuwa atafanya vema katika michuano ijayo ya London Marathon ya mwezi April na yale ya Dunia ya mwezi Agosti na kutuwakilisha tena kama alivyofanya huko mumbai nchini India.
"Tunaendela kumdhamini Simbu na tunashirikiana kwa karibu na meneja wake na kocha ili kuhakikisha kijana anajinoa vizuri kwa ajili ya mashindabo yanayomkabili." amesema Ronald.
Kwa upande wake Mwanaridha huyo amewasifu waandishi wa habari kwa kazi walioifanya ya kutoa taarifa kwa umma kuhusu yaliyojiri huko Mumbai wakati wa mashindano hayo pamoja na Ufadhili alioupata kutoka Kampuni ya Multichoice Tanzania kwa kwa kumuwezesha kufanya maandalizi mazuri yenye kiwango kinachohitajika.

 Simbu amesema kuwa katika mashindano hayo ushindani ulikuwa mkubwa sana kwani wengi wa wanariadha walioshiriki walikuwa ni wazoefu na wenye sifa za kushiriki mashindano makubwa ya kimataifa.
 
Hata hivyo ameimba serikali kukusanya wachezaji wengi katika mchezo huo kama wanavyofanya nchi nyingine kwani kwenye 10 bora kulikiwa na wakenya 7 ,waethiopia 2 na Mtanzania alikuwa peke yake, hii inaleta ugumu sana kwenye mashindano kwani kwa kawaida mkiwa wengi kuna mbinu za kusaidiana ilimradi kuhakikisha anashinda mtu aliyekuwa katika tumi yenu". amesema Simbu.

Ujumbe wa Kiongozi wa Kiislamu kwa Jumuiya ya Wanachuo Ulaya

Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Duniani Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.
Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Duniani Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametuma ujumbe kwa jumuiya za Kiislamu za wanafunzi wa vyuo vikuu barani Ulaya na kusema: "Ni jukumu la kila mtu kupeperusha bendera ya Uislamu halisi katika vita visivyo na usawa vya makabiliano na mrengo wa kufru na uistikbari."

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei,  katika ujumbe wake huo uliotolewa Ijumaa hii, amesema: "Ni matarajio yangu kuwa mbali na kuwa mtajijenga kielimu, kidini na kiakhlaqi, muwe pia ni wenye taathira katika mazingira yenu na muongoze watu zaidi wafuate njia ya Mwenyezi Mungu kwa maneno na vitendo vyenu vyema."

Ayatullah Khamenei ameashiria kuwa, 'ujana na uanachuo' ni nukta zenye nguvu ambazo humsaidia mwanadamu kufikia malengo yake ya juu' na kuongeza kuwa, 'mbali na kuwa muna sifa hizo mbili, pia mna sifa nyingine yenye taathira nayo ni kupitia jumuiya za Kiislamu.'

Kiongozi  amesisitiza kuwa, kila moja anapaswa kunufaika na baraka za chemchemu ya maarifa sahihi ya Kiislamu na kuwa katika njia nyofu ya Mwenyezi Mungu.

Thursday, January 19, 2017

Muft wa Tanzania awa Mgeni Rasmi kwenye Maulid ya Mtume (s.a.w.w) iliyoandaliwa na Bilal Muslim Mission of Tanzania

Viongozi wa Kiislam kutoka Madhehebu mbalimbali wakiwa katika Sherehe ya Maulid ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), iliyofanyika katika Msikiti wa Udoe, Dar es salaam, jana. Wapili kutoka kulia ni Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi na Watatu kushoto ni Kiongozi Mkuu wa Tabligh wa Bilal Muslim Mission of Tanzania Sayyid Arif Ali Naqvi.  
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi amewataka Waislam kuwa wamoja ili kuweza kupambana na changamoto mbalimbali zinazoukabili umma wa Kiislam.

Sheikh Zuberi amesema hayo jana kwenye Sherehe ya Maulid ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), iliyoandaliwa na Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania kutoka Taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania.

Katika Maulid hiyo Viongozi mbalimbali hususan kutoka Baraza kuu la Waislam Tanzania Wajumbe wa baraza hilo na Masheikh wa baraza hilo wa  Mkoa wa Dar es salamm walihudhuria.
 

 Ujio wa Mufti Zubery kushiriki katika sherehe za Maulidi ya Mtume tena kwa dhehebu ambalo awali ilikuwa ni vigumu kuhudhuria inaelezwa ni ishara tosha kuwa Kiongozi huyo amedhamiria kuondoa ubagauzi uliopo kati ya kundi moja na lingine ambayo yote yanasema yanamfuata Mtume Muhammad.




Tuesday, January 10, 2017

Viongozi mbali mbali duniani waomboleza kifo cha Ayatullah Rafsanjani

Huku shughuli za kumzika Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu hapa nchini, Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani, shakhsia na viongozi mbali mbali wameendelea kutoa salamu zao za rambirambi kufuatia kifo cha mwanachuoni huyo.

Miongoni mwa shakhsia waliotuma salamu zao za rambirambi kwa familia, jamaa, na marafiki wa marehemu Rafsanjani pamoja na serikali na taifa la Iran kwa ujumla ni Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast na mwenzake wa Cuba, Raúl Castro. 
Rais wa Kodivaa
Wengine wa hivi punde kutuma salamu zao za pole ni Rais Bashar al-Assad wa Syria, Karen Karapetyan, Waziri MKuu wa Armenia, Mfalme Abdullah II wa Jordan na Rais wa eneo la Kurdistan nchini Iraq Masoud Barzani.

Katika ujumbe wake uliotumwa kwa Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria amesema, taifa na serikali ya Algeria inatoa mkono wa pole kwa taifa na serikali ya Iran kutokana na kifo cha Ayatullah Rafsanjani. 

Awali pia Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alituma salamu zake za rambirambi na kusema: "Afrika Kusini inamshukuru Rais (Mstaafu) Rafsanjani kwa moyo wake wa kujitolea kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kisiasa na nchi za Afrika ikiwemo Afrika Kusini hususan wakati alipokuwa Rais wa Iran"
Josh Earnest, Katibu wa Masuala ya Vyombo vya Habari ya Ikulu ya Marekani White House
Hali kadhalika Josh Earnest, Katibu wa Masuala ya Vyombo vya Habari ya Ikulu ya Marekani White House ametuma rambirambi zake akimtaja Rafsanjani kama shakhsia wa aina yake katika historia ya Iran.
Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani alifariki dunia juzi usiku akiwa na umri wa miaka 82, baada ya kukumbwa na mshtuko wa moyo.

Kiongozi Muadhamu aongoza Swala ya maiti ya Ayatullah Rafsanjani

Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Duniani, Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei ameongoza Swala ya maiti ya marehemu Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani, rais wa zamani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Umati mkubwa ukiongozwa na viongozi wa ngazi za juu wa serikali na wanazuoni wameshiriki Swala hiyo, iliyoswaliwa katika Chuo Kikuu cha Tehran.

Takriban viongozi wote wa ngazi za juu wa Iran akiwemo Rais Hassan Rouhani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Ali Larijani na Mkuu wa Vyombo vya Mahakama Ayatullah Sadeq Amoli Larijani. 

Kiongozi Muadhamu na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Iran wakimuombea dua marhum Rafsanjani
Shughuli ya kusindikiza mwili wa marehemu Ayatullah Rafsanjani inaanza saa nne asubuhi ikiongozwa na Rais Hassan Rouhani, mawaziri wa serikali na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi wakifuatiwa na wananchi katika Husainiya ya Jamaran. Mwili wa marehemu Ayatullah Rafsanjani utazikwa kandokando ya kaburi la mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini katika eneo al Behest Zahraa katika viunga vya mjini Tehran.

Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani aliyekuwa Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran alifariki dunia Jumapili usiku kutokana na matatizo ya moyo