Tuesday, February 21, 2017

Afisa mwandamizi wa Marekani atimuliwa kwa kumkosoa Trump

Craig Deare, afisa mwandamizi katika serikali ya Marekani ametimuliwa kwa kukosoa sera za Rais Donald Trump wa nchi hiyo.
Deare, ambaye ni afisa mwandamizi wa Baraza la Usalama wa Taifa ameachishwa kazi baada ya kukosoa sera za Trump na washauri wake wa karibu.
Afisa huyo mwandamizi wa serikali ya Washington ambaye aliteuliwa mwezi uliopita kuongoza kitengo cha baraza hilo katika eneo la Hemisphere ya Magharibi alisindikizwa na maafisa wa usalama kutoka jengo la ofisi aliyokuwa akifanya kazi mjini Washington.

Afisa mmoja mwandamizi wa Ikulu ya White House amethibitisha kuwa Deare si mfanyakazi tena wa Baraza la Usalama wa Taifa na kwamba amerejea kwenye shughuli yake ya hapo kabla katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Ulinzi.

Afisa huyo amethibitisha ripoti hiyo kwa sharti la kutotajwa jina lake pasina kutoa maelezo zaidi.

Hata hivyo baadhi ya maafisa wa serikali ya sasa na ya zamani ya Marekani wamesema, Craig Deare amefukuzwa kufuatia matamshi aliyotoa siku ya Alkhamisi iliyopita katika kikao cha faragha kilichofanyika kwenye kituo cha tanuri fikra cha Wilson kilichoko mjini Washington.


Rais Donald Trump wa Marekani
Kwa mujibu wa mmoja wa watu waliohudhuria kikao hicho, Deare aliishambulia vikao serikali ya Trump kutokana na sera zake kuhusiana na eneo la Amerika ya Latini  hususan kwa kuanzisha mikwaruzano na serikali ya Mexico.

Katika wiki ya kwanza mara baada ya kuingia madarakani, Rais wa Marekani alisaini dikrii ya ujenzi wa ukuta katika mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Mexico, ikiwa ni kutekeleza ahadi aliyotoa wakati wa kampeni za uchaguzi. Hatua hiyo ilimfanya Rais Enrique Pena Nieto wa Mexico avunje safari yake ya kuelekea Marekani aliyokuwa amepanga kuifanya mwishoni mwa mwezi Januari.

Imeripotiwa kuwa Deare alionyesha waziwazi kukasirishwa na kukatwa mijadala yote ya sera kuhusiana na Mexico na kueleza kwamba washauri wa karibu wa Trump akiwemo mkuu wake wa stratijia Steve Bannon na mkwe wa Rais huyo Jared Kushner hawakuwasiliana na kurugenzi ya Baraza la Usalama wa Taifa wakati serikali ilipokuwa ikiandaa sera

Kiongozi Muadhamu asisitiza ulazima wa walimwengu kuzingatia suala la Palestina

Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Duniani amesema suala la Palestina ni la kuhuzunisha mno linalomuumiza kila mtetezi wa uhuru, haki na uadilifu duniani.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo hivi punde katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa sita wa kimataifa wa kuunga mkono Intifadha ya Palestina unaofanyika hapa mjini Tehran ambapo mbali na kuwakaribisha wageni wote waalikwa amesisitiza kuwa historia ya Palestina na kuvamiwa na kukaliwa kwake kidhalimu kwa mabavu, kufanywa wakimbizi mamilioni ya watu pamoja na muqawama wa kishujaa wa taifa hilo shujaa kumeshuhudia hali ya faraja na misukosuko mingi.

Kiongozi  Muadhamu (wa pili kushoto) mara baada ya kuwasili kwenye ukumbi wa mkutano
Kiongozi Muadhamu amebainisha kuwa upembuzi makini katika historia unaonyesha kuwa hakuna kipindi chochote cha historia, wala hakuna taifa lolote duniani lililowahi kukabiliwa na mateso, machungu na hatua za kidhalimu kama taifa la Palestina ambapo kutokana na njama iliyopangwa nje ya eneo lake nchi hiyo ikavamiwa na kukaliwa kwa mabavu kikamilifu, watu wake wakatimuliwa katika majumba yao na badala yao likatafutwa kundi moja la watu kutoka huku na kule duniani na kupelekwa huko; 

uwepo halisi wa watu wa eneo hilo ukapuuzwa na badala yake uwepo bandia na wa kubuni ukawekwa mahala pake; hata hivyo, huu pia ni ukurasa mwingine mchafu wa historia ambao kama zilivyo kurasa nyingine chafu utafungwa tu kwa idhini na msaada wa Mwenyezi Mungu mtukufu.

Maelezo kamili ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu itakujieni katika matangazo yetu yajayo

Wednesday, February 15, 2017

Udharura wa kuundwa kamati ya kutafuta ukweli kuhusu jinai za kivita za Saudi Arabia

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen kwa mara nyingine tena sambamba na kumtaka Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kufanya safari nchini Yemen ili ashuhudie kwa karibu hali ya nchi hiyo ameitaka taasisi hiyo ya kimataifa iunde kamati huru ya kutafuta ukweli.

Hisham Sharaf Abdullah amesisitiza kuwa, ripoti iliyotolewa na ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na matukio ya wiki mbili zilizopita katika mji wa Mokha huko Yemen imefumbia macho jinai zilizofanywa na muungano wa nchi za Kiarabu dhidi ya raia katika mji huo. 

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesisitiza kuwa, ni vyema ofisi hiyo ijihusishe zaidi na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa unaofanywa na ndege za kijeshi za muungano wa Kiarabu ambazo kila siku  zimekuwa zikifanya mashambulio 300 katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo huku zikitumia silaha zilizopigwa marufuku ambazo unazipata kutoka Uingereza, Marekani na Canada; hatua ambazo zimenyamaziwa kimya na jamii ya kimataifa ambao haionyeshi radiamali yoyote ile.
Ndege za kivita za Saudia zinazofanya mashambulio ya anga kila uchao Yemen
Tangu kuanza vita nchini Yemen, viongozi wa Yemen na walimwengu wamekuwa wakimtaka mara kwa mara mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu afanye safari nchini Yemen ili akajionee uhalisia wa mambo kuhusiana na ukiukwaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na Saudi Arabia. 

Hata hivyo hadi sasa takwa hilo halijatekelezwa. Ripoti za hivi karibuni kuhusiana na jinai za utawala wa Aal Saud huo Yemen zimewafanya walimwengu wafahamu mambo ya kutisha yaliyofanywa na Saudia kutokana na kutumia kwake mabomu yaliyopigwa marufuku ya fosforasi na vishada dhidi ya wananchi wa Yemen.

Kwa hakika kile ambacho kimeandaa uwanja na mazingira ya Saudia kuendelea kutenda jinai nchini Yemen na kuwaua wananchi madhulumu wa nchi hiyo ni upuuzaji wa maafisa wa Umoja wa Mataifa na kutouchukulia hatua utawala wa Aal Saud. 

Kwa mfano, Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa aliitoa Saudia katika orodha ya nchi zinazokiuka haki za watoto, hatua ambayo ilikuwa na nafasi muhimu katika kuupa kiburi utawala wa Saudia cha kuendeleza jinai zake huko Yemen.
Watoto wengi nchini Yemen wanataabika kwa njaa
Utendaji huo mbovu wa Umoja wa Mataifa unaonyesha ni kwa kiwango gani taasisi hiyo ya kimataifa imeathiriwa na uingiliaji wa madola makubwa ya Magharibi pamoja na pesa za mafuta za watawala wa nchi za Kiarabu. 

Nukta nyingine muhimu ni kwamba, wakati Saudia imetenda jinai kubwa nchini Yemen ambazo ni mfano hai na wa wazi wa jinai za pande tatu zilizoainishwa katika Hati ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, yaani jinai dhidi ya binadamu, jinai dhidi ya amani na jinai za kivita, kwa uungaji mkono na madola ya Magharibi imechaguliwa tena kuwa mwanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na hata kuwahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya wataalamu wa umoja huo!

Umoja wa Mataifa unaojulikana kuwa eti mlinzi wa amani na usalama wa dunia, katika kutekeleza majukumu yake, badala ya kuwahami wananchi wa Yemen, umeathiriwa na lobi za Wasaudia na kubadilisha msimamo kwa kupuuza uvamizi na jinai za Saudia huko nchini Yemen. Hali ya kuwa mmoja wa wadau muhimu wa kushughulikia mizozo ya kivita kimataifa ni Umoja wa Mataifa na asasi zinazofungamana na umoja huo. Umoja wa Mataifa katika fremu ya nguzo zake kuu yaani Baraza Kuu na Baraza la Usalama una jukumu la kufuatilia mizozo ya utumiaji silaha kimataifa.
Mabomu ya vishada yanayotumiwa na Saudia dhidi ya wananchi wa Yemen
Baadhi ya nguzo zisizo kuu za Umoja wa Mataifa zina majukumu ikiwemo kuwafikishia misaada wakimbizi, watoto, wanawake na waathiriwa wa vita; na baadhi ya nguzo nyingine zina jukumu la kutafuta ukweli na kuandaa ripoti kuhusuiana na ukiukaji wa haki za binadamu katika mapigano hayo, ambapo katika hili pia Umoja wa Mataifa haujawa na utendaji mzuri, si katika kuwafikishia misaada wananchi wa Yemen wala kuakisi jinai za Saudia dhidi ya wananchi hao.

Hatua pekee ambayo imechukuliwa na Umoja wa Mataifa kuhusiana na Yemen ni ile ambayo haikuwa na taathira yoyote ya Ismail Ould Cheikh Ahmed mwakilishi wa UN katika masuala ya Yemen ya kuitisha mazungumzo ya kitaifa. Mazungumzo hayo nayo hayajawa na natija yoyote katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo kutokana na mwakilishi huyo kutokuwa na nia safi kwa upande mmoja na hatua za ukwamishaji mambo za Saudia na mamluki wake kwa upande wa pili.

Watawala wa Aal Saud kwa kufahamu vyema kigugumizi na hatua za kusitasita za Umoja wa Mataifa na kutokuweko irada ya kweli ya maafisa wa umoja huo katika kukabiliana na jinai za Saudia, wamekuwa wakiendelea na jinai zao nchini Yemen bila ya wasiwasi wowote.

Maelfu ya wananchi waandamana Mexico dhidi ya Trump

Maelfu ya wananchi wa Mexico wamefanya maandamano makubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Mexico City wakitaka kuheshimiwa nchi yao na wahajiri wa nchi hiyo. Maandamano hayo yamefanyika kufuatia matamshi ya chuki na uhasama ya Rais Donald Trump wa Marekani na serikali yake dhidi ya wahajiri na Wamexico.

Ripoti zinasema kuwa wafanya maandamano hao ambao jana walikusanyika kwa wingi katika mji mkuu wa Mexico huku wakiwa wamebeba bendera za nchi hiyo, wametangaza kupinga mipango ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kutaka kujenga ukuta wa mpakani na kuendelea kuwafukuza wahajiri wa Mexico huko Marekani.
Maandamano ya wananchi wa Mexico dhidi ya Rais wa Marekani
Jumapili iliyopita pia maaandamano mengine kama hayo yalishuhudiwa katika miji mbalimbali ya Mexico katika kupinga siasa za Marekani dhidi ya nchi hiyo. Wafanya maandamano hao walisema kuwa wao wakiwa ni raia wa Mexico wanapasa kuitolea mwito serikali itekeleze majukumu yake na kuwalinda raia na mamlaka ya kitaifa mbele ya mashambulizi ya serikali ya Marekani. 

Tuesday, February 14, 2017

Imam wa msikiti wa Al-Aqsa: Hatutotekeleza sheria ya marufuku ya Adhana

Sheikh Ikrima Sabri, Khatibu na Imam wa msikiti wa Al-Aqsa amesema sheria ya kupiga marufuku sauti ya adhana katika misikiti ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni ya kidhalimu na kusisitiza kwa kusema: Sitatekeleza uamuzi huo.

Mufti wa Quds na Khatibu wa msikiti wa Al-Aqsa ameongeza kuwa hatua za aina hiyo za maghasibu wa Kizayuni si za kisheria na ni uingiliaji unaofanywa na Wazayuni katika masuala ya kidini ya Waislamu.

Huku akisisitiza kwamba hatua ya utawala wa Kizayuni kuhusiana na suala hilo ni uingiliaji mipaka ya Waislamu, Sheikh Sabri ameongeza kuwa adhana ni katika alama za Kiislamu na hakuna mtu mwenye haki ya kuingilia suala hilo kwa sababu au kisingizio chochote kile.

Mufti wa Quds na Imam wa Msikiti wa Al-Aqsa ameonya kuwa serikali ya mrengo wa kulia ya utawala wa Kizayuni wa Israel ndiyo itakayobeba dhima ya mivutano na mtafaruku wowote utakaosababishwa na uamuzi huo.
Msikiti mtukufu wa Al-Aqsa
Kamati ya mawaziri ya utungaji sheria ya utawala wa Kizayuni siku ya Jumapili ilipitisha rasimu iliyofanyiwa marekebisho ya sheria ya "marufuku ya kutangaza adhana" katika mji wa Baitul Muqaddas na kuiwasilisha kwenye bunge la utawala huo Knesset.

Kwa mujibu wa duru za habari, bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel, linatazamiwa kuupigia kura muswada huo kesho Jumatano ili uwe sheria.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, utumiaji vipaza sauti katika maeneo ya ibada na usomaji adhana utakuwa marufuku kuanzia saa tano usiku hadi saa moja asubuhi.

Katika miongo ya karibuni utawala wa Kizayuni umekuwa ukifanya kila njama za kubadilisha utambulisho wa Kiislamu wa mji wa Baitul Muqaddas; ambapo hatua ya karibuni kabisa ni hiyo ya kupiga marufuku kusomwa adhana kwenye misikiti ya mji huo

Monday, January 30, 2017

WATANZANIA WAOMBWA KUMUUNGA MKONO RAIS DK.JOHN MAGUFULI

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda (katikati), akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kuuaga mwaka wa 2016 na kuukaribisha mwaka 2017 Dar es Salaam jana. Kulia ni Msajili Msaidizi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Sisty Nyahoza na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ADA na Waziri wa Nchi asiye na Wizara Maalum, Zanzibar.
Na Dotto Mwaibale

WATANZANIA wameombwa kumuunga mkono Rais Dk.John Magufuli kwa jitohada zake anazozifanya za kupongoza nchi.

Mwito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini John Shibuda wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kuuaga mwaka wa 2016 na kuukaribisha mwaka 2017 Dar es Salaam jana.

Alisema Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikifanyakazi kubwa ya kudhibiti mirija ya unyonyaji wa pato la Taifa kupitia watumishi hewa, wanafunzi hewa, kaya masikini bandia na kupitia wahujumu uchumi wa matumizi mabaya ya dhamana za Taifa mambo ambayo yalikuwa yakipigiwa kelele na vyama vya upinzani.

"Binafsi nawaomba watanzania bila ya kujali itikadi za vyama vyao kumuunga mkono Rais wetu Dk.John Magufuli na wasaidizi wake Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na wengine wote kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuongoza Taifa letu la Tanzania" alisema Shibuda.

Alisema anaupongeza utumishi wa Serikali ya awamu ya tano kwa uzinduzi wa urejeshaji wa uwajibikaji wa watumishi wote kwani hivi sasa watumishi wengi wanatabia za miiko ya utiifu kwa umma.

Akizungumzia Zanzibar alisema uchaguzi umekwisha pita na Rais wa nchi hiyo ni Dk. Ali Mohammed Shein ambaye anatakiwa kuongoza nchi hiyo na wenzake waliochaguliwa ili kuiletea maendeleo Zanzibar hivyo siasa za mihemuko ziachwe.

Shibuda alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wazanzibar hasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ushindi walioupata Jimbo la Dimani na kuwaomba walioshindwa wasivunjike moyo kuvunjika jembe siyo mwisho wa uhunzi kwani hata timu kubwa hufungwa na timu ndogo.

Akizungumzia katazo la vyama vya siasa kutofanya mikutano hadi mwaka 2020 alisema majibu ya suala hilo yatatolewa baadae baada ya kulifanyia kazi jambo hilo. 

Katika hatua nyingine Shibuda alisema Baraza la Vyama vya Siasa litakuwa mshirika rafiki wa wadau wote wa siasa na kusimamia maslahi mapana ya jamii na Taifa yanayosimamiwa na Serikali na kuungwa mkono na Bunge mfano Azimio la EPA.

Shibuda alitoa ushauri kwa vyama vyote vya upinzani kuzingatia umakini wa mabadiliko ya Tabia nchi ya mfumo wa uwajibikaji wa Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.

Ufilipino yaitaka Marekani iache kuingiza silaha zake nchini humo

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amesema Marekani inahatarisha usalama wa eneo kwa kuendelea kurundika silaha zake katika nchi hiyo.

Rais Duterte ameituhumu Washington kuwa inatengeneza vituo vya kudumu vya kuhifadhi silaha zake katika mikoa mitatu ya nchi hiyo. Rais wa Ufilipino amesema: "Ninatoa ilani kwa vikosi vya jeshi la Marekani, sitoruhusu muendelee kuhifadhi silaha zenu katika ardhi yetu, hata hatufahamu kama makombora ya nyuklia yanaingizwa nchini na US au la."

Amebainisha kuwa, hatua hiyo ya Marekani ya kuingiza mashehena ya silaha nchini humo inakiuka moja kwa moja makubaliano ya ushirikiano wa kiulinzi kati ya nchi mbili hizo.
Wanajeshi wa Marekani nchini Ufilipino
Ufilipino ilisaini makubaliano ya ulinzi na Marekani ambayo yamedumu kwa zaidi ya muongo mmoja sasa mbali na makubaliano mengine mapya yaliyosainiwa baina ya pande mbili mwaka 2014.

Oktoba mwaka jana, Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino alitangaza kuwa anataka ndani ya kipindi cha miaka miwili ijayo vikosi vya jeshi la Marekani viwe vimekwisha ondoka katika ardhi ya nchi yake; na kama italazimu anataka pia kuvunja mkataba wa ulinzi na muitifaki huyo wa muda mrefu wa Manila.