Saturday, January 26, 2019

Waislam AhlulSunna Waungane na Waislamu Shia Ithnasheriya ili kudumisha Umoja | Maulana Jalala

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akiotoa Khutba ya Swala ya Ijumaa, leo Masjid Ghadir Kigogo Post Dar es salaam, akizungumzia Je, Usuni na Uwahabi ni kitu Kimoja?

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania  Maulana Sheikh Hemed Jalala amewataka Masheikh na wanazuoni wa Ahlul Sunna Dar es salaam na Tanzania nzima kuungana na Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania ili waendee kuwa wamoja na kuweza kumshinda Adui anaofanya kazi ya kuwagawa.

 “Enyi Ndugu zangu, Wasomi, Masheikh na Wanazuoni wa AhlulSunna Tanzania kuweni macho, Waislamu Shia Ithnasheriya ndio wenzenu, na Mkitaka Usuni uwendelee, ninawaambia Masheikh wa Ahlul Sunna wa Dar es salaam na Tanzania nzima waungane na Mashia Ithnasheriya ndio ndugu zao na wabaki pamoja, na wakitaka wamshinde adui wa Usuni wawe pamoja na Mashia Ithnasheriya” Amewataka Maulana Sheikh Jalala.

Maulana Sheikh Hemed Jalala amesema hayo leo Khutba ya Swala ya Ijumaa, imeyoswaliwa wiki iliyopita, Masjid Ghadir Kigogo Post Dar es salaam, ambapo katika khutba hiyo alizungumzia Je, Usuni na Uwahabi ni Kitu Kimoja?.

Aidha Maulana Sheikh Jalala amewatahadharisha Wasoni, Masheikh na Wanazuoni wa Kiahalul Sunna kuwa macho na gurupu linalofanya kazi ya kuwagawa AhlulSunna na Shia Ithnasheriya kwa kutofuata maelekezo yao ambayo inaonekana ndio chanzo cha Matatizo mengi katika jamii ya Kiislamu.

“Nataka niwaeleze Ndugu zangu, Wasomi na Wanazuoni wa Ahlul Sunna katika nchi hii wakae wakitambua kwamba hilo gurupu linalowaambia Waislamu Shia Ithnasheriya sio wenzenu, msiwaalike kwenye Maulid zenu, msishirikiane nao, msiende kwenye misikiti yao, hao ndio sio wenzenu katika Ahlulsunna, na hao ndio waliowaletea matatizo mengi” Maulana Sheikh Jalala amesema

Hatahivyo Maulana Sheikh Jalala amewatoa hofu Watanzania kwa kusema kuwa Dini tukufu ya Uislamu asili unalingania watu kuwa wamoja, kupendana na kutokuunga mifarakano yoyote ambayo itapekekea migogoro yoyote katika jamii ya Kiislamu.

 “Watanzania Mungu amewaletea Uislamu ambao hauwagawi watu, unawatakeni muwe kitu kimoja, unawatakeni mpendane, vipi linakuja gurupu linaanza kuwagaweni huyu ni Shia Ithnasheriya na huyu ni Ahlul Sunna?,huyu ni Ibaadhi huyu ni Ghawarij?, mbona sivyo Uislamu ulivyo?,?” Amesisitiza Maulana Sheikh Jalala


Saturday, January 19, 2019

Waislamu watakiwa Kuitukuza na Kuienzi Qur’an | Sheikh Kasonso.

Khatbu wa Swala ya Ijumaa Sheikh Amir Kasonso akitoa Khutba Jana katika Masjis Bilal Temeke, Jijini Dar es salaam, akizungumzia Kuitukuza Qur'an.

Khtabu wa Swala ya Ijumaa Sheikh Amir Kasonso amewataka Waislamu kuipa kipaumbele kitabu Kitufu cha Qur’an katika kukitunza, kukienzi na kufuata yaliyomo ndani ya Qur’an ili kuweza kupata mahitajio yote ya mwanadamu katika Nyanja zote katika Maisha ya Kila Siku.

Sheikh Kasonso alisema hayo jana katika Khutba ya Swala ya Ijumaa , iliswaliwa Masjid Bilal Temeke, Jijini Dar es salaam, katika Khutba yake akizungumzaia Utukufu na Ubora wa Quran tukufu.

“Sisi leo hii Waislamu tujiulize, Qur’an tunaitetemekea katika unyenyekevu na ule kuitukuza Qur’an je tunacho?, na kitendo cha kuienzi na kuyafuata yaliyomo ndani ya Qur’an tunayo? Huku ndiko kunyeyekea kunakotakikana” Alisema Sheikh Kasonso.

Aidha Sheikh Kasonso alionyesha hali ya kusikitisha kwa kuwa hali ya Waislamu wanaishi kinyume na mafundisho ya Kitabu chao kitukufu cha Qur’an na kufanya kila wanaloweza bila ya kuwa na chembe ya Hofu ya kuiogopa Qur’an.

 “Leo hii tunatembea Vingine na Qur’an yetu inatuambia vingine, Kila jambo katika Ulimwengu huu tunalipeleka vile ambavyo tunaona sisi liko sawa, lakini si vile Qur’an inataka, hii ni dalili yakwamba sisi sio wenyenyekevu, sisi hatuheshimu Qur’an, hatuiogopi Qur’an” alisisitiza Sheikh Kasonso.

Hatahivyo, Sheikh Kasonso amewataka wazazi kuweza kuthamini Kitabu kitufu cha Qur’an na kutokilinganisha na Vitabu vingine ambapo baadhi ya wazazi wameonekana wako tayari kumnunulia Daftari mtoto wake kuliko kumnunulia kitabu kitufu cha Qur’an.

“Leo hii mzazi hataile thamani ya kumnunulia mwanae Juzu la Tsh.300/= ni mtihani Mkubwa, angalie Qur’an inavyodhalilika, lakini aende akanunue daftari, atanunua hata Daftari 15 hadi 20, ikiwa Juzu Mzazi yuko tayari mwanae aende hivyohivyo, hii ni dalili Qur’an haidhaminiwi” Sheikh Kasonso alionyesha huzuni.

Friday, January 18, 2019

Waislamu watakiwa kuwa Wamoja katika Amani- Maulana Sheikh Jalala


Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akiongea katika Khutba ya Swala ya Ijumaa, leo Masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es salaam.
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala amewataka Waislamu wa Tanzania kuienzi amani, Umoja kwa kuacha tofauti ya Mitazamo yao pamoja na kujitenga na makundi yenye lengo la kuondoa Umoja na Mshikamano baina ya Waislamu na Watanzania.

Maulana Sheikh Jalala amesema hayo leo katika Khutba ya Swala ya Ijumaa ya wiki iliyopita, iliyoswaliwa Masjid Ghadir, Kigogo Post, Jijini Dar es salaam, huku akizungumzia Je, Uwahabi na Usuni ni Kitu Kimoja?.

“Katika zama hizi ni zama ambazo Waislamu wanahitajia kuwa kitu kimoja,kama kuna kipindi Waislamu wanatakikana waache tofauti zao,na mitizamo zao ni zama tulizokuwa nazo, ni zama ambayo Umoja, kuwa kitu kimoja, kuzungumza pamoja, kukaa meza moja, ni zama muhimu mno” Alisema Maulana Sheikh Jalala.


Aidha Maulana Sheikh Jalala anawakumbusha Waislamu wa Tazania kuwa asili ya Watanzania hata kabla ya Uhuru na baada ya Uhuru wameleleka katika Umoja, kupendana, kushirikiana, kuelewana, kusaidiana bali hawakuleleka katika kubaguana na kukufurishana.

 “Watanzania wameleleka kwenye Umoja, kupendana, kuelewana, kushirikiana, watanzania hawajaleleka kwenye kubaguana na kuchukiana Waislamu wa Tanzania Ahlul Sunna, Shia Ithnasheriya na Ibaadhi katika nchi hii walikuwa kitu kimoja hata kabla ya Uhuru wa nchi hii,na wala hawakujua kubaguana, wala kukufurishana” alisisitiza Maulana Sheikh Jalala


Hatahivyo Maulana Sheikh Jalala amewatahadharisha Waislamu na Watanzania kujitenga na makundi yote likiwemo kundi la Kiwahabi yenye malengo mabaya ya kuichafua Tanzania inayosifika nchi ya Amani na Maelewano.

“Malengo la kundi hilo la Kiwahabi ni kutaka kuwagawa na kuwataka kuwafanya kuwa ni makundi tofauti ambayo mwisho wa yote ni kugombana na kuifanya Tanzania sio mahala pa amani, maelewano na mshikamano”aliongeza Maulana Sheikh Jalala

Saturday, January 12, 2019

Sera ya Kiwahabi ni Sera ya Kuwagawa Waislamu-Maulana Jalala

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akitoa Khutba ya Swala ya Ijumaa, Masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es salaam.

Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala amesema kuwa katika jambo la kusikitisha na kuhuzunisha leo katika Ulimwengu wa Kiislamu ni kundi la Kiwahabi kufanya bidii na mikakati ya hali na mali, mikakati ambayo ni ya kuwagawa Waislamu, kuhakikisha Waislamu hawezekani wakawa kitu kimoja.

Maulana Sheikh Jalala alisema hayo jana  katika Khutba ya Swala ya Ijumaa, iliyoswaliwa Masjid Ghadir, Kigogo Post, Dar es salaam,akizungumzia Je, Uwahabi na Usuni ni Kitu Kimoja?, na kusema kuwa Kundi la Kiwahabi limefanikwa kuingia katika Jamii ya Waislamu Ahlul Sunna na kujiita wao ni Ahlul Sunna.

Maulana Sheikh Jalala alisema kuwa Mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Swalafun Swaleh yanaharamisha Kumkufurisha Mtu anaetoa Shahada Mbili hatakama mnatofautiana rai, lakini jambo la kushangaza kundi la Kiwahabi wanakufurisha Mtu anaetoa Shahada Mbili kwa kuwa wanatofautiananae rai.

“Watu walikuwa wamoja, Waislamu walikuwa ni Kitu kimoja, kutoka Mtume Muhammad (s.a.w.w), Moja ya jambo ambalo ukilisoma katika historia ya kipindi hicho cha watu ambao ni Salafun Swaleh, moja ya kitu walichokuwa wanapambana nacho na hawakikubali ni jambo la kumkufurisha mtu anaetamka Shahada Mbili, ila Kundi la Kiwahabi linakufurishana” alisema Maulana Sheikh Jalala.

Maulana Sheikh Hemed Jalala aliongeza kuwa kundi la Kiwahabi ndio kundi cha kwanza kuzuka duniani lililokuja kumkufurisha mtu wa Qibla, na kuhalalisha Umwagaji wa Damu yake na Unyaganyi wa Mali zake na kusema kuwa hayo sio Mafundisho ya Ahlul Sunna.

 “Kundi la Kiwahabi lilipokuja, lilipodhihiri, lilipozuka Duniani ndio Kikundi cha kwanza lililokuja kumkufurisha Mtu wa Qibla, yani Mtu anaesema Ashahadu allaa illaah ilallah waashahadu anna Muhammad Rasulullah, kwa kuwa hakubaliani na fikra zao huyo ni Kafiri, na damu yake ni halali na mali yake ni hali” aliongeza Maulana Sheikh Jalala.

Hatahivyo Maulana Sheikh Jalala alisisitiza kuwa Jamii ya Kiislamu haina misamiati ya kukufurishana wala kuitana Mushriki kwa watu wanaotoa Shahada Mbili, kwasababu wanatofautiana rai na mtazamo na kusema kuwa hayo sio Mafundisho ya Ahlul Sunna.

“Jamii ya Waislamu haijazoea, haijasikia wala haijalelewa katika Misamiati hii huyu ni kafiri, huyu ni Mshirikina, haipo kwenye kamusi ya Kiislamu, kwa waislamu wenyewe kwa wenyewe kutuhumiana na Shirki, kwa kosa gani? Kwa kosa la kutoafautiana rai na mtazamo ambapo sio Mafunzo na Maelekezo ya Maimam wanne wa Ahlul Sunna”alisisitiza Maulana Jalala.


Toeni Nafsi zenu katika Mambo ya Mwezi Mungu.

Kahtibu wa Swala ya Ijumaa, Sheikh Ramadhani Kwezi, Jana Masjid Bilal Temeke, Dar es salaam.

Khatbu wa Swala ya Ijumaa Sheikh Ramadhani Kwezi amewataka Waislamu watanzania kujitolea nafsi zao kwa hali na mali katika kuhakikisha kuueneza na kuulinda Mila na Desturi na mafundisho ya Dini tukufu ya Uislamu.

Sheikh Kwezi alisema hayo jana katika Khutba ya Swala ya Ijumaa, iliyoswaliwa Masjid Bilal Temeke, Jijini Dar es salaam, akizungumzia Mazazi ya Bibi Zainabu bint Ali (a.s) na kusema Bibi Zainab aliitoa Nafsi yake katika Kulinda Dini tukufu ya Uislamu.

Sheikh Kwezi alisema kuwa Uislamu umewakataza Waislamu kufanya Matendo, Vitendo na mambo yote ambayo ni mabaya hayana maslahi katika Jamii, hayana maslahi kwa mtu mmja mmoja, na mambo amabyo yanavuruga na kusambaratisha Umma wa Kiislamu.

“Matendo,Vitendo na mambo mbalimbali au shughuli mbalimbali ambazo ni mbaya hazina maslahi kwa Umma,hazina mashalahi kwa mtu mmoja mmoja wala kwa jamii,bali ni mambo ambayo yanavuruga na kusambaratisha Umma wa Kiislamu Tumekatazwa” alisema Sheikh Kwezi.

Aidha Sheikh Kwezi amewataka Waislamu na Watanzania kuhakikisha wanafanya Uadilifu, Ihsani na Kutoa Sadaka na kutokuwadhulumu watu na kusema kuwa kufanya hivyo ni kufuata mafundisho na maamrisho ya Mwenyezi Mungu ambae ni muumba wa Vitu vyote Ulimwenguni.

Mwenyezi Mungu anasema “Hakika Mwenyezi Mungu anatuamrusha tuishi kwa Uadilifu yaani kila mtu apewe anachostahiki, kwa Ihsani yaani Matendo mema, kufanyiana wenyewe kwa wenyewe mambo mazuri, kuwasaidia mayatima,Wajane na wenyeshida na kutoa kwa watu wa karibu”

Hatahivyo Sheikh Kwezi amewataka Waislamu na Watanzania kumuiga na kumfuta Bibi Zainabu (a.s) katika Ushujaa na Ujasiri na kusimama imara katika kuhakikisha haki inatengeka, Uadilifu unafanyika, Dhulma haitakiwa, Mambo mabaya hayatakiwi, na maonevu hayatakiwi.

Bibi Zainabu (a.s) ni Mmoja katika Mashujaa wa Karbala, aliesimama Imara katika ardhi ya Karbala nchini Iraq,Bibi zainabu ni mmoja kati ya wale amabo wanadaraja kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu (swt), Bibi Zainabu Baba yake ni  Sayyidna Ali Ibn Abutwalib (a.s) na Mama yake ni Fatuma Bint Muhammad (a.s). Bibi Zainabu alizaliwa tarehe 5 Jumadal al Awal mwaka wa 5 AH sawa na tarehe 2, Oktoba mwaka wa 625 AD.


Wednesday, January 2, 2019

Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania (T.I.C), yafanya Semina Elekezi, 29-30 / 12 / 2018.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania (T.I.C) Sheikh Issa Rwechungura akiongea na Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini, Baraza la Ulamaa, Kamati Tendaji na Uongozi wa Taifa, katika Semina Elekezi,iliyojikita katika mambo ya Sheria na Uongozi, iliyoratibiwa na Jumuiya hiyo,ambayo ilifanyika 29-30/12/2018, Makao Makuu ya Jumuiya, Kigogo Post Dar es salaam.Hao ni Viongozi wa wapya wa muhula wa tatu waliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika mwezi wa 4. 2018.

Mkufunzi katika Semina Elekezi iliyoratibiwa na Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania (T.I.C) katika Kipengele cha Management (UONGOZI), Kigogo Post Dar es salaam

Picha ya Pamoja ya Baadhi ya Wajumbe wa Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania (T.I.C) katika ngazi ya Bodi ya Wadhamini, Baraza la Ulamaa, Kamati Tendaji Taifa, na Uongozi wa Taifa, katika Viwanja vya Kigogo Post Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, Jijini Dar es salaam.
Mjumbe wa Kamati Tendaji Taifa wa Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Mh.Abdulkarimu Shamte akinukuu mambo Muhimu, katika Semina Elekezi, kutoka kwa Mkufunzi wa Mambo ya Sheria, Kigogo Post Dar es salaam.



Mjumbe wa Kamati Tendaji Taifa wa Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania (T.I.C) Sheikhat Fatuma Mwiru akinukuu baadhi ya Nukta Muhimu katika Semina Elekezi, iliyofanyika Kigogo Post Dar es salaam.

Mjumbe wa Baraza la Ulamaa wa Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania (T.I.C) Sheikh Ammar Chega, akinukuu baadhi ya Nukta Muhimu katika Seminia Elekezi, Kigogo Post Dar es salaam.


Mjumbe wa Baraza la Ulamaa ambae ni Muakilishi kutoka Visiwani Zanzibar, akichangia katika Semina Elekezi, iliyofanyika 29-30/12/2018, Kigogo Post Dar es salaam.

Wednesday, December 26, 2018

“Amani iwe juu yangu siku niliyozaliwa, siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa” Quran 19 aya 33.Maneno ya Nabii Issa (a.s) au Yesu Kristo

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala (kushoto) akimkabidhi Kadi ya Krismas Askofu Banza Suleimani kwa Niabaa ya Wakristo wote Tanzania na Duniani, jana katika Kikao na Waandishi wa Habari cha Kutoa Salamu za Krismas na Mwaka Mpya, Kigogo Post Jijini Dar es salaam.

Bismillah Rahmani Rahimu
“Amani iwe juu yangu siku niliyozaliwa, siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa” Quran 19 aya 33.Maneno ya Nabii Issa (a.s) au Yesu Kristo

Watanzania wenzangu Waislamu na Wakristo, Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu nyote.

Katika siku hii ya leo sisi kama Waislamu wa Madhehebu ya Shia Ithnasheriya Tanzania tunapenda kutoa Mkono wa Kheri , Mkono wa Baraka, Mkono wa Fanaka kwa watanzania wote wakristo na wale wasiokuwa wakristo kwa mnasaba huu na kwa eid hii kubwa ya kuzaliwa Yesu Kristo au Issa       Ibn Mariam.

Tunatoa Mkono huu wa Kheri, Mkono huu wa Baraka uliojaa Mahaba, uliojaa Upendo, uliojaa Ushirikiano, uliojaa uzawa, uliojaa Utanzania, uliojaa kupenda nchi yetu kama watanzania sote tunaokusanywa na jina la Tanzania nan chi ya Tanzania, Namuomba Mungu wakristo wote wa Tanzania, Waafrika na Duniani Waisheherekee Eid hii kubwa ya Mazazi ya Yesu Kristo kwa kuzidi Upendo , kwa kuzidi Maelewano na kuzidi Mshikamano.

Napenda katika tukio hili wa Eid hii ya Krismas, Furaha hii ya Krismas kwa ndugu zetu wakristo wa Tanzania na wengine, napenda ninakili Quran takatifu katika sura ya 19 aya ya 33, Quran 19 aya 33 Mwenyezi Mungu anazungumzia Mazazi ya Nabii Issa (a.s) au Mazazi ya Yesu Kristo anasema Maneno yafuatayo “Maneno haya anayatamka  Yesu Kristo au Issa ibn Mariam (a.s) ndani ya Quran Surat Mariam aya ya 33 anasema Yesu au Issa.

“Na amani iwe kwangu Mimi siku niliyozaliwa na siku nitakayo Kufa na siku nitakayofufuliwa nikiwa hai” Maneno haya ameyatamka Nabii Issa (a.s) au Yesu Kristo wakati amezaliwa bado ni Mtoto Mdogo, Mayahudi wanamtilia Shaka Mariya Bikira au  Mariamu ,kwamba Vipi umempata Mtoto kabla ya kuolewa? Anadhibitisha Yesu Kristo au Issa (a.s) yakwamba Amani iwe juu yangu siku hii ya leo na siku nitakapo kufa na siku nitakapo fufuliwa.

Maneno haya yanatufunza nini? Na huu ndio ujumbe Muhimu wa Krismas yetu hii ya mwaka 2018 na 2019, kwamba Yesu Kristo na Mitume wengine wote, Yesu Kristo au Issa (a.s) anazaliwa, anachozaliwa nacho anasema nimezaliwa  kuenzi amani ndio kitu cha kwanza ametoka nacho, kwahiyo huu ni Ujumbe Mkubwa unaozungumzwa ndani ya Quran katika siku hii ya mazazi ya Yesu Kristo au Issa (a.s), mafunzo ya kuenzi amani, lakini kuenzi amani katika Nyanja gani?

Ni katika Nyanja tano Muhimu  lazima kuenziwa amani, Nyanja ya kwanza lazima kuenziwa amani kwenye Nyanja na kiwango cha mtu mmoja mmoja, lazima kila Mwanadamu aishi kwa amani kama alivyoitangaza Issa (a.s) au Yesu Kristo siku anayozaliwa , amani iwe kwangu siku nilipozaliwa , siku nitakapo kufa na siku nitakapo fufuliwa , maisha yangu yote ni maisha yanayogubikwa na amani na mitume wote maisha yao yaligubikwa na amani mpaka siku yao ya mwisho.

Kwahiyo ni lazima tuenzi amani kwa kiwango cha mtu mmoja mmoja, mtu anapofanya kazi anapotekeleza wajibu wake huyo amekaa kwa amani, Mtu anapomuabudu Mungu, Jumapili akaenda Kanisani, Ijumaa akaenda Msikitini huyo anaishi kwa amani, mtu anaekaa Vizuri na Jiraani na wenzake huyo anaishi kwa amani.

Pili kuishi kwa amani kwa kiwango cha familia, familia yoyote inayopendana , baba anaependana na watoto wake, anaependana na mkewe, hiyo ni familia inayoishi kwa amani. Familia yoyote inayowafundisha watoto inayowapeleka watoto shule wasome ,wajifunze, ni familiya inayoishi kwa amani. Familiya inayoishi katika kulinda ada,kulinda taratibu za Kiafrika, za Kikabila, ,mambo mazauri tuliyokuwa nayo ya kiafrika kuyaenzi huku ni kuenzi amani.

Jambo la tatu ni amani kwa ustawi wa Kijamii, Jamii amabyo haitumii madawa ya Kulevya, jamii ambayo haina mambo ya Ushoja, jamii iliyosalimika na mambo ya mahusiano machafu na mabaya, hiyo ni jamii inaishi kwa amani.kwa hiyo jamii iliyosalimika na hayo ni jamii inayoishi kwa amani.

Kwahivyo siku hii ya Mzazi ya Issa (a.s) au Yesu Kristo ametangaza kwamba yeye amezaliwa kwa amani, ameishi kwa amani na atakufa kwa amani Tuienzi amani tutakuwa tumemuenzi Issa  (a.s) , tukienzi amani tutakuwa tumemuenzi Yesu Kristo.

Jambo la Nne ni kuilinda amani au ni kuitazama amani kwenye kiwango cha Kitaifa, Taifa linaloenzi amani ni taifa la aina gani? Ni Taifa linalojitahidi kufuta Ujinga kwa wtu wake, taifa linaloishi kwa amani ni taifa linalojitahidi kufuta maradhi katika jamii yake, taifa linalohimiza watu wake wafanye kazi kwa bidii, taifa ambalo linawatumikia watu wake, hilo ni taifa linaloenzi amani na linaloishi kwa amani.

Mwisho ni kuenzi amani kwa mustawa wa Kimataifa, yoyote yale ambayo yameathiri mataifa mengine, yamesababisha uvunjifu wa amani uwepo katika mataifa mengine, kuenzi amani kimataifa nikujitahidi yale yote mabaya yasifike katika ardhi ya Tanzania. “Amani iwe juu yangu siku niliyozaliwa, siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa” Quran 19 aya 33.
Huu ni Ujumbe wa Yesu Kristo au Yesu (a.s) ndani ya Quran siku aliyozaliwa , ni Mtu wa Amani ni mpenda amani, ni mpenda watu nan i mpenda jamii na hayo ndio maisha ya Mitume wote akiwemo Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Nawatakieni Krismas Njema, nawatakieni watanzania wanaoienzi amani, wanaopenda amani, wanaokaa Vizuri, wanaoelewana na wanaoshikamana, asanteni sana na Mungu awabariki katika Krismas yenye Baraka na kheri tele, Mungu ibariki Tanzania.
                                                                                                                                                                          Imetolewa na:                                                                                    Maulana Sheikh Hemed Jalala                                                   Kiongozi Mkuu wa Waislamu Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania