Thursday, September 12, 2019

“Imam Hussein (a.s) alitoka ili Jamii iwe Salama”Sheikh Jalala

Kiongozi wa Waislamu Shia Ithnasheriya Maulana Sheikh Hemed Jalala (wapili kushoto) akiongoza msafara wa Vijana kuelekea katika eneo la Zoezi la Usafi, katika kata ya Kigogo Mkwajuni Dar es salaam.

Kiongozi wa Waislamu Shia Ithnasheriya Maulana Sheikh Hemed Jalala amesema kuwa malengo ya Imam Hussein (a.s) ni kuifanya jamii iwe salama, na katika hali ya usafi wa Mazingira kwani kufanya hivyo ni kutekeleza Mafunzo ya Dini.

“Tunaamini ya kwamba Moja ya Malengo ya Imama Hussein (a.s) Mtoto na Mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kutoka na kuelekea katika ardhi ya karbala ni kufanya jamii iwe salama ni kufanya jamii iwe safi ni kufanya jamii iwe katika mazingira mazuri, na sisi tunaamini ya kwamba jambo la Usafi ni jambo kubwa na ni jambo muhimu, tunaamini ya kwamba Uasfi ni katika Imani Usafi ni katika dini” Maulana Sheikh Jalala

Kiongozi wa Waislamu Shia Ithnasheriya Maulana Sheikh Hemed Jalala akiongea na Waandishi wa Habari punde tu baada yta kuanza zoezi la Usafi.
Sheikh Jalala alisema hayo jana katika zoezi la Usafi ulifanyika katika kata ya Kigogo Jijini Dar es salaam kwa lengo la kukumbuka Kifo cha Imam Hussein (a.s) Mtoto na Mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w).

“Kutoka kwetu na Kufanya Usafi ni kwa ajili ya kuhakikisha yakwamba tumemuunga mkono Imam Hussein (a.s) katika jambo lake la kutengeneza jamii ,tunaamini yakwamba Usafi ni chachu ya kuleta afya bora, tunaamini yakwamba usafi ni sababu ya watu kukaa katika mazingira mazuri, watu wanaokaa katika mazingira mazuri watakaa kwa usalama, wanaweza kuwa na elimu bora”

Aidha Sheikh Jalala amesema miongoni mwa sbabu ya kutoka na kufanya usafi na kuiunga Mkono Serikali ya Mkoa wa Dar es salaam ambayo yanaenda sambamba na Mafundisho aliyotoka Imam Hussein (a.s) kuyatetea yarudi katika Jamii iliyomzunguka.

Serikali yetu na Mkoa wetu wa Dar es salaam kwa kupitia Mkuu wa Mkoa  huwa ikipiga kelele marakwa mara kuhusiana na jambo la usafi mpaka ikaweka siku maalumu ya usafi, tumetoka pia kumuunga mkono mkuu wa Mkoa kwamba tupo nay eye katika jambo la usafi katika siku hii ya kumkumbuka Imam Hussein (a.s) Mjukuu na Mtoto wa Mtume Muhammad (s.a.w.w)”

Mjumbe wa Serikali ya Mitaa wa Kigogo Mkwajuni Mhe. Ibrahim Gogo akiongea na Vyombo vya Habari punde tu baada ya kushiriki katika zoezi la Usafi.
Kwaupande wake Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kigogo Mkwajuni Mh. Ibrahimu Gogo amefurahishwa na kitendo cha Waislamu Shia Ithnasheriya kufanya Usafi katika eneo lao kwa kuadhimisha Siku ya Kifo cha Imam Hussein (a.s).

“Sisi kama Watendaji, sisi kama watu wenye dhamana kusimamia hii serikali katika mtaa wetu, tumeona tuungane nao, tuwe nao pamoja kwasababu wanafanya jambo la Kijamii ni jambo kubwa, licha ya kuwa wanaadhimisha Kifo cha Imam Hussein (a.s) wameona tushirikiane katika kusafika maeneo ya mtaa wetu” Mhe. Gogo.


Friday, June 7, 2019

Watanzania watakiwa kuwa Wakweli na Watii baada ya Mwezi wa Ramadhani | Maulana Sheikh Jalala

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akiongea na Waandishi wa Habari punde tu baada ya Swala ya Eid al Fitir, katika Viwanja vya Pipo Kigogo Dar es salaam.

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala amewataka Watanzania kuwa wakweli, watii, wasikivu, wapenda amani na wenye kupendana na kuelewana ikiwa ni mwendelezo wa athari iliyopatiana katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Baada ya kumalizika Mwezi wa Ramadhani tuwe Watanzania Wakweli, tuwe watanzania wenye Utii, tuwe ni watanzania wenye usikivu, tuwe ni watanzania wenye kupendana, tuwe ni watanzania wenye kuelewana, hayo yote ni maelekezo yaliyoko ndani ya Qur’an”

Maulana Sheikh Jalala amesema hayo wakati akiuongea na waandishi wa Habari katika kutoa Salamu za kheri na fanaka baada ya Swala ya Eid al Fitiri, iliyoswaliwa katika Viwanja vya Pipo Kigogo jijini Dar es salaam.

Aidha Maulana Sheikh Jalala amesema kuwa Tumeona ndani ya ardhi yetu ya Tanzania ndugu zetu wakristo wakiandaa futari wakiwaalika waislamu, wakikaa meza moja wachungaji, Maaskofu na Masheikh pamoja na Waislamu wengine hii ni dalili nzuri yakuonyesha upendo na Mshikamano. Kama tulikuwa tunakaa waislamu na wakristu tukifuturu pamoja katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, haya ni malezi yanatakikiana yaendelee baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani”

Mjumbe wa Baraza la Ulamaa wa Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania (T.I.C) Sheikh Mulaba Swalehe akiongea na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam 
Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza la Ulamaa wa Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania (T.I.C) Sheikh Mulaba Swalehe amesema kuwa lengo la Mwezi wa Ramadhani ni watu kuwa Wachamungu utakaopelekea Binadamu kuishi kwa amani na Salama katika Ulimwengu.

“Leo tunamshukuru Mungu kwa kukamilisha mwezi wa Ramadhani ambao ulikuwa ni mwezi lengo lake kubwa ni  kufikia Uchamungu, ni wajibu wa kila mmoja kuweza kumsaidia ndugu yake na kumpenda ndugu yake, kwani kwa hali hii ili tuweze kuishi kwa amani na salama katika dunia hii.
Mwisho Maulana Sheikh Jalala amesema kuwa anamuomba Mwenzimungu (swt) upendo tuliokuwanao katika Mwezi wa Ramadhani, Mahusiano mazuri tuliokuwanayo katika mwezi wa Ramadhani kama watanzania, mahusiano haya yazidi kuboreka, yazidi kuendelea, utulivu na amani tuliouonyesha ndani ya Mwezi wa Ramadhani amani hii na utulivu huu namuomba mwenyezi mungu uendelee katika ardhi ya Tanzania katika masiku mengine, Eid njema.
Waumini wa Dini ya Kiislamu wakijumuika pamoja na Waislamu wengine duniani katika kushiriki Swala ya Eid al Fitir, katika Viwanja vya Pipo Kigogo Dar es salaam. 

Waumini wa Dini ya Kiislamu wakiomba dua katika swala ya Eid al Fitir, iliyoswaliwa katika Viwanja vya Pipo jijini Dar es salaam


Thursday, June 6, 2019

Natamani Amani ya Tanzania iwepo Palestina na nchi zinginezo | Maulana Sheikh Jalala

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akiongea na Waandishi wa Habari katika Matembezi ya Amani ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds, yaliyoanzia Ilala Boma na kufikizia katika Viwanja vya Pipo Kigogo Dar es salaam.

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala amewataka watanzania wasikubali kuridhika na Amani walionayo nchini bali na hatimae  wahakikishe amani ya Tanzania inakuwepo katika nchi zinazopakana na  Tanzania ikiwepo nchi ya Palestina.

“Amani lazima tuienzi, na tusikubali tukaiacha hapa hapa Amani hii, lazima tuipeleke kwa wenzetu, lazima tuwaonyeshe wenzetu, lazima tuwaombee Mungu wenzetu wapalestina na sehemu zinginezo wawe na utulivu kama tulionao. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Palestina, zibariki nchi zote ambazo hazina utulivu na uzipe amani” Maulana Sheikh Jalala.

Maulana Sheikh Jalala amesema hayo wakati wa Matembezi ya Amani ya kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Quds, yaliyoanzia katika Viwanja Ilala Boma na kufikizia Viwanja vya Pipo Kigogo Dar es salaam pamoja na kuhudhuriwa na Waislamu, Wakristo na Wapenda Amani Tanzania na Ulimwenguni.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mshikamano wa Tanzania na Palestina Mhe. Abdallah Othmani akiongea na Waandishi wa Habari Kigogo Dar es salaam.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Mshikamano wa Tanzania na Palestina Mhe. Abdallah Othmani ameitaka Serikali kuwa Tuinaimba Serikali yetu izidi kupaza sauti juu ya swala la Palestina, wapalestina wametoa mchango mkubwa katika afrika, tusiaache wakiwa, turejee katika maneno ya baba wetu wa Taifa alivyokuwa na msimamo wake juu ya swala ya Palestina, tuhakikishe ndugu zetu wapalestina, tunawaunga mkono kwa hali na mali.

“Hatuna chuki na Waisraeli ni Binadamu kama sisi, ila siasa zile za kupora ardhi, siasa za uvunjifu wa amani wa haki za Binadamu, hilo ndilo tatizo tunalolisitikia, kwahivyo tunamuomba Raisi wetu apaze sauti juu ya jambo hili, ili kuwatizama wapalestina katika jicho la huruma na wao” amesema Mhe. Othmani.
Waumini wa Kiume wa Dini ya Kiislamu wakifanya Matembezi ya Amani ya Kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds, Jijini Dar es salaam

Waumini wa Kike wa Dini ya Kiislamu wakifanya Matembezi ya Amani ya Kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds, Jijini Dar es salaam

Imam Khomein (r.a) ni Bingwa wa Uislamu na ni Bingwa wa Amani | Sheikh Jalala

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala  akiongea na Maimamu, Maustadhi na Masheikh katika Semina ya kumbukizi ya Kifo cha Imam Khomein, Masjid Ghadir 02.06.2019,Kigogo Post Dar es salaam

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala amesema kuwa Imam Khomein (r.a) aliuelewa Uislamu kwamba inawezekana ukaishi katika dunia tuliokuwa nayo maisha yako yote kuwa ni Maisha ya Kiislamu na ukaishi na jamii isiyokuwa ya Kiislamu ikakupenda na ikakusikiliza.

Maulana Sheikh Jalala amesema hayo katika Semina ya Kumbukizi ya Kifo cha Imam Khomein (r.a), Semina ambayo iliwakusanya Maustadhi, Masheikh na Maimam, iliyofanyika Masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es salaam.

Maulana Sheikh Jalala amesema kuwa ukijaribu kuisoma historia na Mwenendo wa  Imam Khomein (r.a) na mahusiano yake na watu utaona kuwa ni Bingwa wa Uislamu na Bingwa wa Amani kwani hakuna siku alilingania Ushia, wala Umadhehebu, wala kundi fulani bali alilingania Laailah ilallah, Muhammadun Rasulullah.

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Mhe. Mousa Farhang akiongea na Maustadhi, Masheikh na Maimam katika Semina ya Kifo cha Imam Khomein.
Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Mhe. Mousa Farhang amesema kuwa Kumbukumbu ya Imam Khomein (r.a) hakumbukwi kwa ukubwa wake bali inakumbukwa Fikra na Mitazamo yake nay ale aliyoyafanya akiwa hai, ili kuyaendeleza kwa Vizazi vijavyo.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Mhe. Abbas Farmand akiongea katika Semina ya kumbukizi ya Kifo cha Imam Khomein.
Aidha nae Mkurugenzi wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Mhe. Abbas Farmand amesema kuwa Maisha ya Imam Khomein (r.a) unaweza kuyaangalia katika sehemu mbalimbali ya Kielimu, Kisayansi, Kijamii na Kisiasa, katika Maswala ya Kifamilia utaona hana mfano.
Masheikh, Maimam na Maustadhi waliohudhira katika Semina ya Kumbukizi ya Kifo cha Imam Khomein, Dar es salaam.

Saturday, May 18, 2019

Wajane watakiwa kuwa Wajasiliamali na kuchangamkia Fursa


Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akizungumza na Wajane takriban 350 wa kata ya Kigogo katika Futari ya pamoja  wakati wa kuadhimisha kumbukumbu ya Kifo cha Bi Khadija (a.s) Mke wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), iliyoandaliwa na Kitengo cha Kinamama wa Chuo cha Imam Swadiq (a.s), iliyofanyika Masjid Ghadir Kigogo Post Dar es salaam. 

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala amewataka Wajane kujishugulisha kwa kufanya Biashara mbalimbali za kujiletea maendeleo na kutokata tama ya maisha kwasababu wanae kiigizo ambaye ni Bi Khadija Mke wa Mtume Muhammad (s.a.w.w).

 “Kitendo cha Bibi Khadija (a.s) kujishughulisha kufanya Biashara, kuwa Mjasiliamali, kufanya harakati za uzalishaji ni dalili tosha na ni kiigizwa tosha cha kwamba Mwanamke Mjane, kumbe anaweza kuwa mjasiliamali, kumbe anaweza kujifanyia Biashara zake ndogondogo, na kuendesha Maisha yake na watoto alioachiwa na mwenzake” alisema Sheikh Jalala

Akizungumza Jana na Wajane takriban 350 wa kata ya Kigogo katika Futari ya pamoja  wakati wa kuadhimisha kumbukumbu ya Kifo cha Bi Khadija (a.s) Mke wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), iliyoandaliwa na Kitengo cha Kinamama wa Chuo cha Imam Swadiq, iliyofanyika Masjid Ghadir Kigogo Post Dar es salaam.

Aidha Sheikh Jalala amewataka Viongozi wa Dini kutumia Misikiti na Makanisa kuwa ni sehemu ya kuwakusanya wajane na Watanzania bila kujali dini zao kufanya hivyo ni kujenga Amani, Upendo, Umoja na Mshikamano, Misikiti na Makanisa isitumike kuwagawa Wajane na Watanzania.

“Leo hii wamekusanyika wajane pasina kubagua dini zao, wajane waislamu wako hapa, wajane wakristo wako hapa, ni somo nzuri na la kupendeza kwamba Misikiti yetu, Makanisa yetu yawe ni Sehemu ya kuwakusanya Waislamu, yawe ni sehemu ya kuwakusanya Wakristo na waka Misikiti yetu na Makanisa yetu yasiwe ni nyumba ya kuwagawa watanzania wetu” Alisisitiza Sheikh Jalala

Mkurugenzi wa Mtendaji wa Sadeline Heath Care Trust Mhe Sara Emmanuel  akizungumza na Wajane takriban 350 wa kata ya Kigogo katika Futari ya pamoja.
Nae Mkurugenzi wa Mtendaji wa Sadeline Heath Care Trust Mhe Sara Emmanuel amewataka Wajane kujiandisha na kuwa wanachama  kwenye Chama cha Wajane Tanzania (TAWIA) kwani  kuna fursa nyingi, ukishakuwa mwanachama kule Miradi mingi ambayo Serikali inatoa inapita kule na fursa nyingi zinapita kule” Alisema Sara Emmanuel

Mwenyekiti wa Chama cha Wajane Tanzania (TAWIA) Mhe. Mariam Aswile na wajane wenzake katika futari ya pamoja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wajane Tanzania (TAWIA) Mhe. Mariam Aswile amewatka wajane kutolala na kuhuzinika badala yake wamtumikie Mungu, kujitoa na kuchichangaya na wajane wenzie ili kutafuta fursa mbalimbali ambazo zitasaidia Ujane kuwa mwepesi katika maisha ya kila siku.

 “Napenda kusema kwamba, Wajane kama tumevyosikia somo la Ujasiliamali kwamba tusilale, tukakaa, tukaendelea kuhuzunika, ila tunapidi  kumtumikia Mungu, kujitoa na kujichanganya kama leo tumevyojichanganya mambo yetu yatakuwa ni Rahisi zaidi, hata huo Ujane utakuwa ni Mwepesi” Alisema Aswile.
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jumuiya ya Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania (T.I.C) Sheikhat Fatma Mwiru (kulia) ambae pia ni Mwanaharakati Kitengo cha Kinamama cha Hawzat Imam Swadiq (a.s) akiwa katika Semina pamoja na futari ya Wajane kwa kumbukumbu ya Kifo cha Bi Khadija (a.s).

Afisa Mtendaji wa Kata ya Kigogo Mkwajuni Mhe. Raphael Mchomvu akiongea na Wajane (hawapo pichani ) katika futari ya pamoja ikiwa ni kumnukumbu ya Kifo cha Bi Khadija (a.s) Mke wa Mtume Muhammad (s.a.w.w),.

Sunday, April 21, 2019

Tunapokumbuka Mazazi ya Imam Mahdi (a.s), tunakumbuka Mambo 5 ya Utawala Bora | 20.04.2019 | Sheikh Jalala


                               
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala, akiongea na Waandishi wa Habari Jana Masjid Ghadir Kigogo Post Dar es salaam katika kutoa Salamu na Kheri za Shererehe na kumbukumbu ya mazazi ya Imam 12 ambae ni Imam Mahdi (a.s).
Bismillah Rahman Rahimu 

           Ndugu zangu Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu nyote.
Tunapokumbuka Mazazi ya Imam Mahdi (a.s), tunakumbuka Utawala Bora.
Napenda nianze kikao change hiki kwa maneno ya Mwenyezi Mungu (swt) yaliyopo katika Qur’an takatifu Suratul Raad aya ya 7, Mwenyezi Mungu anasema mwisho wa hii aya : “na hakika hapana vingine wewe Muhammad (s.a.w.w) ni mwenye kuhofisha na kila watu wanakiongozi wao”

Katika aya hii inakwenda sambamba na tukio la leo la mwezi 15 shabani siku ambayo waislamu duniani na hususan Waislam Shia Ithnasheriya wanasheherekea na kukumbuka mazazi ya kuzaliwa Imam wa 12 ambae ndie muokozi atakaekuja kuwaokoa na kuwaongoza walimwengu.

Katika tukio hili la kuzaliwa Imam wa 12 , kwanza napenda kutoa mkono wa hongera na Baraka na fanaka kwa waislamu wote duniani kwa mazazi ya Imam Mahdi (a.j.t.s), lakini pia napenda kutoa mkono wa heri fanaka na Baraka kwa watanzania wenzangu wote, pia kwa wanazuoni na maulamaa wote duniani na marajiin wetu hususani Kionngozi wa Vyuo vya Kidini Duniani Sayyid Sistani, pia natoa mkono wa Hongera na kheri iliyojaa fanaka kwa Kiongozi wetu na Naibu wa Imam wa 12, Kiongozi wa Waislam Duniani Imam Khamenei.

Katika tukio hili la kukumbuka kuzaliwa Imam wa 12 Imam Mahd (a.s) napenda kuzungumza yakwamba wamekubaliana waislamu wote yakwamba atadhihiri zama za mwisho Kiongozi anaeitwa Mahdi (a.s) na kwa hili wamekubaliana vilevile dini zote, Wakristo, Mayahudi, Mabudha na dini za Kimisri za zamani, kwamba Dunia haiwezi kumalizika lazima atakuja kudhihiri Mtu ambae ndie atakaeihakikishia duniani imekuwa mahala pa Amani, mahala pa Upendo na mahala pa mshikamano.

Kwahiyo itikadi ya kudhihiri muokozi hii ni itikadi ya dini zote, je muokozi huyo ni nani?, sisi waislamu tunasema muokozi huyo ni Imam Mahdi (a.s) na sisi Waislamu Shia Ithnasheriya btunasema kwamba ndio huyuhuyu aliezaliwa siku kama ya leo ya mwezi 15 shabani, ambayo tunaiitwa kwa lugha nyingine siku ya kugawa riziki ambayo waislamu wote hukesha Misikitini na kuomba dua maalumu.

Lakini kubwa lakuzungumzwa ni malengo ya Imam huyu,na jambo analotaka kulifanya ni jambo gani?.  Hadith zinasema bwana huyu atakapodhihiri ataijaza dunia uadilifu, ataijaza dunia haki, ataijaza dunia amani. Kwahivyo niseme yakwamba Imam Mahdi (a.s) atakapodhihiri atakachokileta ataleta Utawala Bora, atakacholeta ataleta Utawala anaostahiki mtawala au watawala wawe.

Utawala huo atakaokuja nao Imam Mahdi (a.s) atakuwa ni mtawala ambae dunia ameijaza uadilifu, ameitajaza amani, ameijaza haki. Katika utwala bora wa Imam Mahdi (a.s) ni utawala utakao kuwa vitu vitano vifuatavyo: 


Jambo la kwanza: Ubaguzi, Bwana huyu atakapodhihiri atapambana na kuondoa Ubaguzi, atapambana kuhakikisha ubaguzi haupo, nah ii ni moja katika siri ya Utawala Bora.Aina zote za Ubaguzi atazisambaratisha, Ubaguzi wa mweupe na mweusi kwake kutakuwa hakuna katika utawala wake kwamba mweupe ni bora mweusi si bora au mweusi ni bora mweupe sio bora hilo litakuwa hakuna.

Ubaguzi wa Ukabila, kabila fulani ndio kabila bora kabila fulani sio kabila bora kwenye utawala wake bora, ubaguzi huo hautakuwepo.kuwabagua watu kwa dini zao huyu ni mwislam, huyu ni mkristo, huyu ni Yahudi, ubaguzi huo utakuwa haupo.ataondoa ubaguzi hata ndani ya madhehebu hakutokuwepo huyu ni bohora, huyu ni Mwiithnasheriya, huyu ni Mwiismailia, huyu ni sunni, huyu ni Shia, huyu ni Ibaadhi, huyu ni shafii, huyu ni kadiria, aina hizo za ubaguzi kwenye utawala wake bora zitakuwa hazipo.

Kwahivyo leo tunapokumbuka mazazi ya Imam Mahdi (a.s) tunakumbuka Utawala Bora atakaouleta bwana huyo. Sihivyo tu Utawala wake hautakuwa na Ubaguzi wa Mitaa, wilaya na Mikoa kwamba kuna mkoa fulani ni bora zaidi, mkoa wa tanga ni bora, mkoa wa Dar es salaam ni Bora, mkoa wa Arusha ni bora mikoa mingine si bora, Taifa fulani ni bora, nchi fulani ni bora.kwake yeye la, ubaguzi wa hata wa aina hiyo wa kimaeneo kwake yeye haupo. Hii ni moja na siri ya Utawala bora, Utawala bora ni Utawala ambao unalenga maeneo yote katika kupeleka huduma na kuwaangalia watu.

Jambo la pili:Kuwatumikia watu, bwana huyu atakapodhihiri atahakikisha anawatumikia wanadamu,Mtume Muhammad (s.a.w.w) anasema bora ya Jambo ni kuwatumikia watu, Utawala wake utawatumikia watu kwa kila mambo muhimu, huduma za kijamii, kama vile huduma ya elimu itakuwa kwa watu wote, haitobagua watu.

Utawala wake ni utawala hautokuwa na wajinga,ni Utawala wa kuhakikisha unafuta ujinga,ni Utawala ambao watu wake watakuwa na masomo yao ya mwanzo mpaka masomo ya juu, kupatikana Profesa, Injinia, watu wenye PHD katika jamii yake ni kitu cha kawaida nah ii ndio siri ya Utawala bora. Babu yake Imam Mahdi (a.s) ambae ni Mtume Muhammad (s.a.w.w) anasema anaetaka dunia lazima awe na elimu, na anaetaka akhera lazima awe na elimu.

Katika utawala wake Tiba itaboreshwa kwa hali ya juu, maji salama na safi ndio watakao kunywa wanadamu, maisha yatakuwa mazuri kwa watu, nah ii ndio siri ya Utawala bora.Mtawala bora ni Yule anaejali watu wake, ni Yule anaetaka huduma ziwafikie wanadamu wote na watu wake wote, hivyo ndivyo atakavyokuwa Imam Mahdi (a.s).

Jambo la tatu:Mivutano, bwana huyu atakapodhihiri atahakikisha kwamba anaondoa mivutano iliyopo kwa walimwengu wote na hiyo ndio sifa ya Utawala bora, Utawala bota ni ule utawala ambao unahakikisha hauna mivutano, ni utawala wenye maelewano.ataondoa mivutano ndani ya Jamii, ndani ya Taasisi, ndani ya nyumba za ibada,zitakuwa hazina mivutano, ataelekeza watu wapendane, watu washikamane na wamtumukie mungu mmoja, wasitumikie waungu wengi ambao ndio sababu ya mivutano tulionayo katika jamii yetu.

Jambo la nne:Ufisadi, bwana huyu atakapodhihiri atahakikisha anaondoa ufisadi, Ufisadi katika Nyanja zote na ufisadi wa waina yoyote,.Yeye atapambana na Ufisadi, atahakikisha Rushwa hailiwi katika jamii yake, na kataika utawala wake, na ndio maana tukauita utawala wa Imam Mahd (a.s) ni Utawala bora, Rushwa itakuwa ni Marufuku, Mikataba feti kwake itakuwa hakuna.

Wafanyakazi hewa katika Utawala wake kutakuwa hakuna, hakutokuwa na matengenezo ya ujanja ujanja kitu kimetengenezwa kwa kitu kidogo lakini mahesabu ni mengi, hapana, Ubabaishaji huo katika Utawala wake kutakuwa hakuna kwa sababu, watu wanamtambua Mungu, watu wanamuelewa Mungu, Utawala wake ni Utawala unaolinda mali za Umma, unaolinda mali za Watu.

Jambo la tano : Amani, na la mwisho atahakikisha amani inatawala kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji, tarafa , Kata, wilaya, Mkoa, Taifa na dunia yote itakuwa ni mahala pa utulivu na amani. Katika Utawala wa Imam Mahdi (a.s) Amani itakuwa inachukua nafasi ya kwanza,riwaya zinatuambia yakwamba katika Utawala wa Imam Mahdi (a.s) katika Utawala wake Bora utakuwa Mtu unatembea masaa 24 hakuna mtu atakaekunyanganya kidani chako cha dhahabu, mama hawezi kunyanganywa herein yake alievaa hata usiku wa manane.

Kwahiyo atahakikisha amani imeboreka kwa ngazi zote na kwa dunia, Amani kwa mtu mmoja mmoja, amani kwa upande wa Familia, amani kwa upande wa jamii, amani kwa mji mzima, amani kwa mabara yetu na amani kwa dunia nzima, itakuwa ni wakati ambao Amani imetanda , upendo umetawala, watu wanamtambua mungu mmoja, wanamuabudu mungu mmoja, hivi ndivyo utakavyokuwa utawala wa Imam Mahdi (a.s).

Hayo ni mambo matano Imam Mahdi (a.s) atakapodhihiri atapambana nayo na kuhakikisha yanatawala, na ndio maana tukasema Utawala wale ni Utawala bora, Kwahivyo katika siku hii tunayokumbuka mazazi ya Imam Mahdi (a.s) ni siku ya kukumbuka na kujifunza utawala bora,Utawala wa Imam Mahdi (a.s) ambapo utawala huo utakapokuwepo mahali popote, basi mahali hapo itakuwa ni pepo na mahali hapo.

Asanteni sana, namuomba Mwenyezi Mungu (swt) kwa Baraka ya Kuzaliwa Imam Mahdi (a.s), Mwenyezi Mungu atupe nguvu za kuweza kuienzi amani, maelewano mazuri, Tanzania iendelee kubakia kisiwa cha amani, mahala pa watu wanaopendana, mahala panapokimbiliwa na watu, kwasababu ya hali yake nzuri ya hewa lakini kwasababu ya watu wake wanavyowapenda watu,na kwasababu ya watu wake wanavyopenda amani, asanteni sana na Mungu awabariki.

Imetolewa na:
Maulana Sheikh Hemed Jalala
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania
Tare:Jumamosi, 20.04.2019 Sawa na 14 Shaban 1440.

Wednesday, April 3, 2019

Siku ya Israa na Miiraj ni siku ya kuwafunza Watanzania Elimu,Maadili Mema, Umoja wa Dini zote na kuenzi Amani-Sheikh Jalala


                                           
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akiongea na Waandishi wa Habari katika unasheherekea kwa shangwe na furaha kubwa tukio la Israa na Miiraj, tukio la Mtume Muhammad (s.a.w.w) kupelekwa usiku kutoka Makka mpaka Masjid al Aqswa ulioko Jurusalem nchini Palestina, na baada ya hapo msafara wa kutoka Masjid al Aqswa kwenda Mbungu za juu, jana Masjid Ghadir Kigogo Post Dar es salaam.
                            Bismillah Rahmani Rahimu
                         Ndugu zangu Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kweny nyote                                      

Siku ya Israa na Miiraj ni siku ya kuwafunza Watanzania Elimu,Maadili Mema, Umoja wa Dini zote na kuenzi Amani.

“SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona” 17. SURA AL ISRAAI,aya ya 1.

Siku hii ya leo tunasheherekea kwa shangwe na furaha kubwa matukio mawili makubwa, tukio la kwanza ni tukio la Israa na Miiraj, tukio la Mtume Muhammad (s.a.w.w) kupelekwa usiku kutoka Makka mpaka Masjid al Aqswa ulioko Jurusalem nchini Palestina, na baada ya hapo msafara wa kutoka Masjid al Aqswa kwenda Mbungu za juu.

Na tukio la pili ni tukio la Mtume Muhammad (s.a.w.w) kukabidhiwa Utume na kupelekwa kama Mtume kwa walimwengu wote, matukio haya mawili, kwanza kwa matukio haya mawili na kwa sherehe hizi mbili, napenda kutoa Salamu zangu za dhati kwa Viongozi wa Dini wote, na kwa Marajii wetu wote wakubwa akiwemo Ayatullah Sayyid Sistan.

Lakini vilevile natoa salamu katika siku hii ya leo ya Israa, Miiraj na Siku ya Biidha kwa Kiongozi wa Umma wa Kiislamu Duniani Imam Khamenei,Mwenyezi Mungu amuhafidhi na ambakishe, lakini vile vile natoa salamu zangu za dhati na hongra na pongezi zangu kwa Imam wa Zama hizi Imam wa 12 Imam al Mahd (a.j.t.s).Tukio la Israa, Miiraj na Biidhaa lina tafsi nyingi na lina ishara nyingi, lakini nitapenda kusema tukio hili linaweza kutupa ishara 5 Muhimu.

Ishara ya Kwanza: ni ishara ya Umuhimu wa Elimu, tukio la Mtume Muhammad (s.a.w.w) la kutoka Makka na kupelekwa Jerusalem nchini Palestina kwenye msikiti mtakatifu  wa al Aqswa ni tukio la kielimu, ni tukio la kisayansi, ni tukio la kiteknolojia. Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuondoka Masjid al Aqswa kwenda kwenye sayari za juu, ni ishara ya Elimu, ni ishara ya Sayansi,ni ishara ya Teknolojia.

Na mwenyezi Mungu amelizungumza katika Qur’an “Kama mnaweza kwenda katika sayari za juu, basi mnaweza kwenda lakini huko kunahitajia Elimu”. Tukio la Mtume Muhammad (s.a.w.w) kukabidhiwa Utume kwa neon “Soma” ni dalili ya elimu, kwa hivyo tukio la Israa na Miiraj moja ya funzo yake muhimu ni funzo ya elimu. Kwa kuwa Israa na Miiraj na kwa kuwa Bi’idha, kupelekwa ni funzo la elimu ni nafasi yetu na ni muda wetu kutilia umuhimu jambo la Elimu.

Sisi kama Watanzania, sisi kama Waislamu lazima kuhakikisha watoto wetu wanasoma, watoto wetu wanakwenda Shuleni, watoto wetu wanakwenda Vyuo, watoto wetu wanakwenda Madrasa, wanakwenda kujisomea kuhakikisha wanakuwa na elimu. Ilakuwa ni kuwadhulumu haki zao kufikia kwamba kutakuwa na watoto wa kitanzania ambao hawapelekwi Shuleni.

 Hawaendi kusoma au wako majumbani kwasababu yoyote itakayopatikana, imefikia muda kwa sisi kama waislamu na kama watanzania kuhakikisha watoto wetu wote wanakwenda masomoni pasina kuwabagua  wawe watoto wa kiume wawe watoto wa kike kwasababu wote wanahaki ya elimu.

Ishara ya pili: ni ishara ya Umuhimu wa Akida, katika ishara ya za tukio la Israa na Miiraj pamoja na Bi’idha ni akida, tendo la Mtume Muhammad (s.a.w.w) kutoka Makka msikitini na kufikizia Masjid al Aqwa hii ni ishara ya kwamba msikiti mtakatifu wa Masjid al Aqswa ulioko Juerusalem ni msikiti wa Waislamu, ni mali ya Waislamu na ni haki ya Waislamu, nan i Lazima (Wajibu) kwa waislamu kuutaka Msikiti wao, kuunadi Msikiti wao,kuhakikisha ya kwamba msikiti wao upo katika mahali pa amani, kuhakikisha msikiti wao huu unabakia kumbukumbu yao hii inabakia, Masjid Aqswa msikiti ambao Mtume Muhammad (s.a.w.w) ndie alievikizia baada ya kutoka msikiti wa Makka.

hii ni ishara kubwa ya kwamba msikiti huu hauna tofauti na msikiti wa Makka, na kwamba utukufu baada ya Msikiti wa Makka unafuatia msikiti wa al Aqswa. Kwa hivyo katika fursa hii tunachukua nafasi kuwaeleza maimam wa Misikiti, kuwaeleza Masheikh kwamba imefikia muda wa kuwaeleza waumuni wao ni upi msikiti mtakatifu, msikiti mtakatifu ni mali ya nani? Na ni sehemu ya nani katika ardhi ile ambao upo msikiti mtakatifu.

Ishara ya tatu: ni ishara ya maadili mema, Msafara wa Israa na Miiraj pamoja na Bi’idha ni msafara unaotupa funzo la Maadili, msafara unaotupa funzo la maadili mazuri, tendo la mtume Muhammad (s.a.w.w) tendo la kuingia peponi, tendo la mtume Muhammad (s.a.w.w) kuwaangalia moto na adhabu zilizopo ndani ya moto na kubainisha Mtume Muhammad (s.a.w.w) ya kwamba watu walioko mototni ni watu wa aina gani.

Na kwanini walikuwepo ndani ya moto? Na kwanini ipo pepo?, kwanini Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikutana na baadhi ya mambo njiani, alikutana na Maidhriti na akapewa maneno ya kuyasoma, alikutana na watu wabaya lakini akapewa kinga ya kujikinga na watu wabaya, alipewa vinywaji akachagua kinywaji kizuri, kwanini haya yote? Haya yote ni kufunza maadili mema, siku ya Israa na Miiraj iwe ni siku ya kuwafunza watanzania  ya kuwaelekeza watanzania maadili mema, maadili mazuri, imefikia muda kuachana na kila jambo ambalo ni maadili mabaya, si mila za watanzania, si mila za waafrika, si mambo yao, na haya maadili leo ni mengi ambayo ni changamoto kubwa inayoikabili taifa na inayowakabili watanzania kwa ujumla.

Ishara ya nne: ni ishara ya Umoja wa dini zote, tukio la Israa na Miiraj pamoja na Bi’idha tunajifunza funzo la Umoja wa dini zote, Mtume Muhammad (s.a.w.w) baada ya kufika Masjid al Aqswa aliweza kuswali na Mitume wote (a.s) nay eye akatangulia mbele akawaswalisha , Mitume wote waliotumwa na Mungu 124,000 walikusanyika pale, wakaswali pamoja na Mtume Muhammad (s.a.w.w), wakaswali swala moja, wakaomba maombi mamoja,wakakaa kikao kimoja, wakatanguliwa na mtu mmoja.

Hii ni ishara na ni mafunzo ya kwamba Mitume (a.s) wote waliotumwa na Mungu, wote ujumbe wao ni mmoja, mafunzo yao ni mamoja, maelekezo yao ni mamoja. Kwahivyo yeyote hapa Tanzania, yoyote hapa Afrika, yoyote hapa Duniani atakae kuja na dini yake akafunza kinyume na umoja, akafunza kinyume na mshikamano, akafunza kinyume na Upendo, huyo amekwenda kinyume mafunzo ya Mitume (a.s) wote, na maimam wote, Vitabu vyote, na watu waliokusanyika pale katika msikiti mtakatifu wa al Aqswa na wakamuomba Mwenyezi Mungu na wakaswali swala moja wakiongozwa ni Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Ishara ya tano: ni ishara ya Umuhumu wa kuenzi Amani na maelewano,Nukta ya tano nay a Mwisho kitendo cha msafara wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuondoka mahala panapoitwa Masjid Harraam yaani Msikiti mtakatifu, nini maana ya msikiti mtakatifu? Msikiti mtakatifu maana yeke ni msikiti ambao huruhusiwi kumwaga damu, hauruhusiwi vita, hauruhusiwi mapambano, msafara ukaanzia katika msikiti huo moja kwa moja ukaja msikiti wa pili  Masjid al Aqswa, hii ni ishara ya nini? Ni ishara ya kwamba kilichopo Masjid Haraam ndio kilichopo Masjid al Aqswa,kama ulivyokuwa Masjid al Haraam Hairuhusiwi Vita,  hauruhusiwi kumwaga damu, hairuhusiwi mapambano.

Hivyo hivyo Masjid Aqswa hairuhusiwi vita vyoyote, hairuhusiwi kumwaga damu, hairuhusiwi mapambano yoyote, kama ilivyokuwa Al kaaba ni mahala pa kuenziwa amani, hivyohivyo masjid al Aqswa ni mahala pa kuenziwa amani,kama ilivyokuwa msafara uliondoka uliondoka kwenye msikiti na ukafikizia kwenye msikiti, msikiti ni mahala pa amani, msikiti ni mahala pa upendo, msikiti ni mahala pa kutokumwaga damu.

Tuko dhidi ya yoyote ambae anamwaga damu katika msikiti iwe ni masjid Haraam iwe ni Masjid al Aqswa, tuko dhidi ya yoyote ambae anatumia nguvu zake kumwaga damu, iwe ni msikiti ulioko Makka au ni Msikiti ulioko Jerusalem, yoyote ambae anavunja amani ya sehemu hizi mbili huyo sisi tuko dhidi yake na hatuko nae na yuko dhidi ya  amani ya dunia,yupo dhidi ya Upendo wa Dunia. Kwa hivyo msafara wa Israa, Miiraj na Bi’idha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni msafara wa unaofunza amani, ni msafara wa kuenzi amani, ni msafara wa kusomesha upendo na maelewano.

Mwisho: Ujumbe wetu katika siku hii ya Israa na Miiraj pamoja na Bi’idha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), ujumbe wetu mkubwa tunaouelekeza kwa watanzania ni Ujumbe wa umuhimu wa Elimu, kimefika kipindi ya kwamba itakuwa ni kosa la jinai watoto kubakia majumbani pasina kupelekwa Shuleni, hususani katika kipindi hiki ambacho  Elimu imekuwa ni Elimu ya Bure, nafasi za Shuleni zimekuwa nafasi pana, ujumbe mkubwa ni kuhakikisha watoto wetu wanasoma, kama tunataka maendeleo ya familia zetu lazima watoto wetu wasome, kama tunataka maendeleo ya taifa letu lazima watoto wetu wasome, kama tunaitaka dunia basi watoto wetu wasome, kama tunataka akhera watoto wetu wasome.

Mwenyezi Mungu nakuomba kwasababu ya tukio la Israa na Miiraj pamoja na Bi’idha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) Taifa hili ulipe amani, taifa hili ulipe utulivu, yoyote mwenyekuitakia matatizo na migogoro Tanzania , Mwenyezi Mungu huyo asiweze kufanikiwa.

Mwenyezi Mungu endelea kubakiza Upendo na Mshikamano kwa watanzania wote, endelea kuifanya Tanzania ni kisiwa na amani ni mahala pa watu wanakaa vizuri,na Mshikamano watu wasioelewa Vita wala kugombana , Asanteni sana, Miiraj njema, Israa njema na Bi’idha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) njema. Ndugu zangu Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kweny nyote.

Imetolewa na 
Maulana Sheikh Hemed Jalala
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania
Tare: Jumanne 02.04.2019 sawa na 26 Rajab 1440
Masjid Ghadir, Kigogo Dar es salaam