Sunday, August 23, 2015

ACT-Wazalendo wavuna Wanachama 500 kutoka CHADEMA

Zaidi ya wanachama 500 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiwemo viongozi wa kata mbalimbali katika wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, wamekihama chama hicho na kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo.

Zaidi ya wanachama 500 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiwemo viongozi wa kata mbalimbali katika wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, wamekihama chama hicho na kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo.

Wanachama hao wamefikia maamuzi ya kukihama chama hicho huku wakiwalalamikia viongozi wao wa CHADEMA wilaya na taifa kumkata mgombea wao wa ubunge jimbo la Ludewa waliyemuhitaji Bwana Okol Haule na kumuweka mgombea wanayemuhitaji wao bwana Bathoromeo Mkinga.


Mamia ya wanachama hawa kutoka wilaya ya Ludewa, wamefanya maandamano ya amani kutoka mtaa wa Kilimahewa hadi katika ofisi za chama hicho zilizopo mjini Ludewa wakiwa na mabango ya aina mbalimbali yakilaani viongozi wa CHADEMA wilaya na taifa kumkata Okol Haule aliyeshinda katika kura za maoni kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo hilo.

Hata mara baada ya wanachama hawa kuwasili katika ofisi za CHADEMA wilaya, viongozi waliingia mitini na kufunga ofisi, lakini dhamira ya wafuasi hawa wa CHADEMA wakiwemo viongozi wa juu kutoka kata mbalimbali za wilaya ya Ludewa, haikuishia hapo na wote wakiwa hawana imani tena na CHADEMA wakaelekea ofisi za ACT Wazalendo mtaa wa Sokoni na kujiunga nacho.
Huku wakidhamiria kuisambaratisha kabisa CHADEMA wilayani humo, wanachama hao wakiungana na mgombea wao wanayemuhitaji bwana Okol Haule wakachoma moto nguo aina ya kombati alizokua akizitumia mgombea huyo, bendera na kadi za CHADEMA ambapo bwana Haule anasema ameshindwa kuvumilia ubakaji wa demokrasia uliofanywa na viongozi wa CHADEMA. chanzo EATV



Friday, August 21, 2015

Mh.Mbatia awaonya Viongozi wa UKAWA

Wakati Umoja wa Katiba ya wananchi UKAWA ukikumbwa na changamoto ya ugawanaji wa majimbo baada ya maeneo mengi nchini Tanzania kuibuka migogoro mara baada ya majimbo ya uchaguzi kugawanywa kwa vyama hivyo,hatimaye mwenyekiti wa chama cha NCCR MAGEUZI ambaye ni mwenyekiti mwenza wa umoja huo ameibuka na kutoa onyo kali kwa viongozi ambao wanakuwa wabinafsi wa kutokutaka kuachiana majimbo na kusema kuwa ubinafsi ni jambo ambalo halitaendekezwa ndani ya umoja huo.

Akizungumza na wanahabari leo jioni hii Dar es salaam amesema kuwa mara baada ya kukamilika kwa kazi ya kugawana majimbo kwa vyama vinne vinavyounda umoja huo kumeibuka sintofahamu ya baadhi ya watu kungangania majimbo ambayo tayari wamepewa watu wengine jambo ambalo amesema kuwa sio makubaliano ya umoja huo na hawatavumilia viongozi wa namna hiyo.

Amesema kuwa moja ya maazimio makubwa ya umoja huo ni kuepuka ubinafsi na kuhakikishya kuwa mambo wanayoyahubiri kwa wananchi wanayatekeleza kwa vitendo ikiwa ni pamoja na amani na umoja hivyo hawako tayari kuona chama au mtu yoyote anaanzisha vurugu ndani ya umoja huo.

Amesema Tayari leo jioni viongozi wakuu watakutana kuona ni jinsi gani wanaweza kushughulikia jambo hilo ili ndoto za watanzania za kuhakikisha kuwa wanauondoa mfumo dhalimu wa CCM uliopo kwa sasa zinatimia na nchi inakuwa na amani na utulivu mkubwa.

Wednesday, August 19, 2015

Mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu

Watu watatu wamekufa na wengine thelathini wamelazwa hospitalini kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Tanzania na hasa katika mji wa kibiashara wa Dar es salaam.

Wataalamu wa afya wamesema kwamba mlipuko huo unapatikana kwenye maeneo ambayo hayana usafi wa kutosha na vyoo vya kisasa hasa katika maeneo yenye msongamano wa makazi katika jiji hilo.
Maafisa wa afya tayari wameshachukua hatua ili kuzuia mlipuko huo usienee zaidi tangu mlipuko mkubwa wa kwanza ulioripotiwa kulikumba jiji hilo mwaka 2009.
Wodi tengefu kwa wagonjwa wa ugonjwa huo imeshaandaliwa katika hospitali za wilaya ya Kinondoni eneo ambalo limeathiriwa vibaya na ugonjwa huo.
 Umma wa watanzania wametakiwa kuwa waangalifu baada ya kifo cha mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka ishirini na saba,mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuonesha dalili zinazoshabihiana na magonjwa ya milipuko.
Dar es salaam ni mmoja kati ya miji yenye idadi kubwa ya watu, mji huo pekee una idadi ya watu zaidi ya milioni tano.
Watu waishio katika makazi holela wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa kipindupindu kutokana na kutokuwa na vyoo bora na vya kisasa .
CHANZO BBC Swahili

UTAFITI WA AFYA YA UZAZI NA MTOTO NA MALARIA KUANZA RASMI TAREHE 21 AGOSTI, 2015

 
Mgeni rasmi, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Dkt. Ahmed Makuwani kutoka Wizara ya Afya na Usitawi wa Jamii akiwahutubia Wasimamizi, Wahariri na Wadadisi wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015 wakati wa hafla fupi ya kufunga mafunzo ya utafiti huo iliyofanyika leo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Wito umetolewa kwa viongozi wote wa Serikali katika Ngazi zote na wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa Wasimamizi, Wahariri na Wadadisi wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria utakaoanza rasmi tarehe 21 Agosti, 2015.
 
 Wito huo uletolewa leo na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Ahmed Makuwani wakati wa hafla fupi ya kufunga mafunzo ya utafiti huo iliyofanyika wilayani Moshi, Kilimanjaro.
 
“Ninawaomba Wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Wadadisi, Wasimamizi na Wahaririwatakaoshiriki zoezi la kukusanya Takwimu za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria wa mwaka 2015 ili kupata taarifa muhimu na sahihi kwa ajili ya kupanga Mipango na Sera endelevu za Sekta ya Afya katika nchi yetu, amesema Makuwani”.
 
Dkt. Makuwani amesema kuwa taarifa zitakazokusanywa kwa wananchi kwa ajili ya  utafiti huo zitakuwa ni siri na zitatumika kwa shughuli za Kitakwimu tu na wala hazina uhusiano wowote na Uchaguzi mkuu wa Mwaka huu.
 
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akielezea umuhimu waUtafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015 wakati wa hafla fupi ya kufunga mafunzo ya utafiti huo iliyofanyika leo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema utafiti huu wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria wa mwaka 2015  unalenga kukusanya taarifa nyingi za sekta ya afya zinazotumika katika kutathmini malengo mbalimbali na pia kusaidia katika kupanga mikakati mipya.
 
Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa mara nyingine tena inafanya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria wa mwaka 2015 ambao kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2010. Utafiti huu utaanza rasmi tarehe 21 Agosti, 2015 kwa nchi nzima na utamalizika mwishoni mwa Mwezi Februari 2016.source.Fullshagwe

Sunday, August 16, 2015

Nasrullah aikosoa Marekani kwa kuitumia Daesh


Katibu Mkuu wa chama cha Hizbullah cha Lebanon amesema kuwa Marekani inalitumia kundi la kigaidi la Daesh kuligawa eneo la Mashariki ya Kati. 
 Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa Washington na waitifaki wake wanatumia ugaidi hususan kundi la kigaidi la Daesh kama wenzo wa kutekeleza mpango wa kuligawa eneo la Mashariki ya Kati, kuanzia Iraq hadi Syria na hata Saudi Arabia kwa sababu mpango huo unafanyika kwa maslahi ya Marekani na utawala wa Kizayuni. 
Sayyid Hassan Nasrullah ameyasema hayo jana usiku katika hafla ya kuadhimisha mwaka wa tisa wa ushindi wa Muqawama wa Lebanon dhidi ya utawala wa Kizayuni katika vita vya mwezi Julai mwaka 2006. 
Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema kuwa upo udharura wa kupinga na kukabiliana na mpango wa kuligawa eneo hili. 
Amesema njama ya kuigawa upya Mashariki ya Kati itasababisha vita vya ndani na vya kikaumu vya muda mrefu, ambavyo matokeo yake yatakuwa uharibifu, maafa na kuongezeka idadi ya wakimbizi.Chanzo Irib

Mawahabi wataka misikiti saba ya Madina ibomolewe

Mjumbe wa baraza la maulamaa wa Saudi Arabia na mmoja wa mawahabi mwenye misimamo ya kufurutu ada ametaka misikiti saba maarufu ya Madina ibomolewe. 
Saleh al-Fawzan, mjumbe wa baraza la maulamaa wakuu wa Saudia na mjumbe wa kamati ya kudumu ya utoaji fatuwa amedai leo kuwa misikiti saba ya kihistoria ya mjini Madina ni bid’a na yote inapasa ibomolewe. 
 Historia ya misikiti hiyo saba inarejea kwenye zama za vita vya Khandaq na iko kwenye bonde la mlima Sala’a magharibi mwa Msikiti mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW mjini Madina. 
Misikiti hiyo saba hivi sasa imekuwa moja ya maeneo ya ziara kwa Waislamu kutoka nchi mbalimbali duniani; ambapo mara baada ya kuwasili Madina Waislamu hao huenda kuzuru misikiti hiyo.chanzo Irib.

Saturday, August 15, 2015

CUF vs POLISI-Soma walichosema CUF muda huu kuhusu agizo la polisi

Baada ya jeshi la Polisi nchini Tanzania kupiga marufuku maandamano ya wanasiasa wakati wa kampeni,chama cha wananchi cuf wameibuka na kusema kuwa kauli hiyo ni mzaha wa jeshi la polisi ambao unaweza kuleta madhara makubwa kwani hakuna sheria inayokataza maandamano ya wanasiasa na hawako tayari kutii sheria hiyo kwani ni uonevu wa watanzania.

Akizungumza na wanahabari mapema asubuhi leo naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho mama MAGDALENA SAKAYA amesema kuwa kuandamana ni haki ya mtanzania ya kikatiba,ambayo imeelezwa kama njia ya kujieleza,hivyo Polisi wanakiuka katiba na sheria za nchi zinazoruhusu kuandamana ambapo pia amesema wanakiuka sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2002 ibara ya 11 ambayo inatambua maandamano na mikusanyiko kama sehemu ya shughuli za kisiasa.

Sakaya anasema kuwa ni kitu ambacho hakiwezi na hakiwezekani wakati wa kampeni kwa vyama vya siasa kufanya kampeni kimya kimya pasipo maandamano ambapo amesema ni utamaduni ambao hata nchi zilizoendelea uliwashinda huku akisema huwezi kutenganisha kuandamana na kampeni kwani ni vitu vinavyokwenda sambamba.

Aidha amesema chama cha wananchi CUF kinaona hizi ni dalili za jeshi la polisi kutumiwa na chama cha mapinduzi CCM ili kuziba aibu wanayoipata kwa kukosa umati wa watu katika mikutano yao.
Mwisho CUF wamesema kuwa hawakubaliani na agizo hilo na kusema kama polisi wataendelea na msimamo huo wao ndio watakuwa wameanzisha vurugu ambazo hazina ulazima katika uchaguzi huo.