Wednesday, December 23, 2015

Waislamu wawatea wenzao wa Nigeria mbele ya UN

Waislamu wa Marekani jana walikusanyika mbele ya ofisi za Nigeria katika Umoja wa Mataifa mjini New York wakitaka kuachiwa huru kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa na vyombo vya usalama.

Walioshiriki katika mjumuiko huo wametoa nara na kaulimbiu za kulaani mauaji yaliyofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu nchini humo. Sayyid Iliya mwanachama wa Congresi ya Waislamu wa Marekani ambaye amehutubia mjumuiko huo amesema kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky ni miongoni mwa viongozi wakubwa wa kidini barani Afrika na kwamba shughuli zake haziwahusu Waislamu wa madhehebu ya Shia pekee bali hata Waislamu wa Suni na jamii za Wakristo.

Mwanaharakati wa Kiislamu wa Marekani, Ali Naqavi ambaye pia amehutubia mjumuiko huo mjini New York amesema kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky na wenzake wanaoshikiliwa na jeshi la Nigeria wanapaswa kuachiwa huru bila ya masharti yoyote.

Mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia wameuawa shahidi katika mashambulizi yaliyofanywa siku kadhaa zilizopita dhidi ya kituo cha kidini cha Baqiyatullah katika mji wa Zaria nchini Nigeria. Kiongozi wa Waislamu hao, Sheikh Ibrahim Zakzaky pia ametiwa nguvuni na jeshi baada ya kujeruhiwa kwa risasi na kupelekwa kusikojulikana.

UN: Muungano wa Saudia unaua raia nchini Yemen

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kuwa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Yemen unashambulia maeneo mengi ya rais na yasiyo ya kijeshi.
Zeid Ra’ad Zeid Al-Hussein alisema jana katika kikao cha kwanza cha wazi cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen kwamba, anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa mashambulizi ya Saudi Arabia yanayolenga miundombinu kama hospitali, shule na maeneo yenye makazi mengi ya raia wa Yemen tangu nchi hiyo ianzishe mashambulizi ya anga miezi tisa iliyopita. Ameongeza kuwa watu wapatao 6000 ambao nusu yao ni raia wa kawaida, wameuawa katika mashambulizi ya Saudia huko Yemen. 

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza la Usalama kwamba miongoni mwa matokeo mabaya ya mashambulizi ya Saudia dhidi ya nchi iliyosambaratika ya Yemen ni kuwa maficho salama kwa makundi yenye misimamo mikali kama lile la Daesh. 

Mwezi Machi mwaka huu muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ulianzisha mashambulizi makali dhidi ya watu wa Yemen kwa kisingizio cha kumrejesha madarakani rais aliyejiuzulu na kutoroka nchi Abd Rabbuh Mansur Hadi-Chanzo irib

Saturday, December 12, 2015

Wanawake Saudia wanashiriki uchaguzi kwa mara ya kwanza

Uchaguzi wa mabaraza ya miji unafanyika leo nchini Saudi Arabia huku wanawake wa nchi hiyo wakishiriki katika uchaguzi kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Wanawake wa nchi hiyo leo wameelekea katika masanduku ya kupigia kura kuwachagua wawakilishi wao wa mabaraza ya miji kwa mara ya kwanza kabisa baada ya kupata haki ya kupiga kura na pia kusimama kugombea nafasi za mabaraza ya miji.
Katika uchaguzi wa leo ambao ni wa aina yake kwa wanawake wa Saudi Arabia, zaidi ya wagombea elfu tano wanaume na wagombea 980 wanawake wanachuana kuwania viti vya mabaraza ya miji.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, wanawake laki moja na thelathini elfu walijiandikisha kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi wa leo huku wanaume milioni moja na laki tatu na nusu wakiwa nao wamejiandikisha kama wapiga kura.
Mabaraza ya Miji ndio bodi pekee ya serikali ambayo wananchi wa Saudia wanaruhusiwa kuchagua wawakilishi wao huku nyadhifa nyingine muhimu serikalini zikiwa ni za kurithishana baina ya ukoo wa Aal Saud na wananchi hawana nafasi yoyote katika uteuzi huo.
Licha ya wanawake wa Saudia kuruhusiwa kuwa wagombea na wapiga kura, wachambuzi wa mambo wanasema kwamba, wana nafasi ndogo mno ya kushinda na kuwa wawakilishi wa mabaraza ya miji.
Wanawake wa Saudi Arabia wanaruhusiwa kupiga kura katika mabaraza ya miji ilihali hadi leo bado hawajaruhusiwa kuendesha gari.

Hawzat Imam Swadiq (a.s)-Dar es salaam, cha Adhimisha Kifo cha Mtume Muhammad (s.a.w.w)

Sheikh Said Athumani, Mwalim wa Hawzat Imam Swadiq (a.s) akitoa hutuba juu ya kumbukumbu ya kifo cha Mtume Muhammad, Masjid Ghadir, Kigogo-Post
Waislamu katika maeneo mbalimbali ya dunia leo tarehe 28 Safar wamekumbuka tukio chungu la kufariki dunia Mbora wa Viumbe na Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad Mwaminifu, amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake. Tarehe 28 Safar.mwaka huu ni sawa na 12/12/2015, Masjid Ghadir Kigogo-Post Dar es salaam
Majlisi na vikao vya kukumbuka siku aliyofariki dunia Mtume wa Mwisho Muhammad (s.a.w.w) vimefanyika katika nchi mbalimbali huku Waislamu wakikumbushana matukufu ya mtukufu huyo na mafundisho yake kwa walimwengu.



Mtume Muhammad (s.a.w.w) alifariki dunia tarehe 28 Safar mwaka 11 Hijria akiwa na umri wa miaka 63. Alipewa utume akiwa na umri wa miaka 40 na katika kipindi chote cha miaka 23 aliwalingania wanadamu haki, upendo, uadilifu na kumwamini Mwenyezi Mungu Mmoja.
Katika siku za mwisho za uhai wake Mtume (saw) aliwausia mengi Waislamu na kuwataka washikamane na kufuata vizito viwili ambavyo alisema ni Qur'ani na Watu wa Nyumba yake tukufu, akisisitiza kwamba hawatapotea iwapo watashikamana barabara na viwili hivyo.



Mamlaka ya Mapato nchini TRA yapanga utaratibu wa kutoa bure mashine za EFD’S kwa wafanya biashara.

Mamlaka ya mapato Tanzania TRA inaangalia utaratibu wa kutoa bure  mashine za kutolea risiti za EFD’s kwa wafanyabiashara ili kurahisisha ukusanyaji wa kodi.

Kaimu kamishna mkuu wa  TRA Dr.Philiph Mpango amesema hayo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ambapo amesema mwisho wa watumishi wa mamlaka hiyo kujaza fomu za mali wanazomiliki ni  December 15 huku akiomba wananchi kusaidia kufichua vitendo vya ufisadi kweneye mamlaka hiyo.
 
Kuhusu  waliotorosha makontena bila kulipia ushuru  amesema  wafanyabiashara 13 tuu ndio wamemaliza kulipa kwa hiari katika muda uliotolewa na rais  na wengine 15 wamelipa sehemu na bado wanadaiwa na watalazimika kulipa  kwa mabavu ambapo kiasi kilichopatikana ni shilingi bilioni 10.

Kituo cha Darulmuslimeen Morogoro,cha Adhimisha Kifo cha Mtume Muhammad (s.a.w.w)

 Waislamu katika maeneo mbalimbali ya dunia leo tarehe 28 Safar wamekumbuka tukio chungu la kufariki dunia Mbora wa Viumbe na Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad Mwaminifu, amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake. Tarehe 28 Safar.kwa mwaka ni sawa na 11/12/2015.

Mtume Muhammad (s.a.w.w) alifariki dunia tarehe 28 Safar mwaka 11 Hijria akiwa na umri wa miaka 63. Alipewa utume akiwa na umri wa miaka 40 na katika kipindi chote cha miaka 23 aliwalingania wanadamu haki, upendo, uadilifu na kumwamini Mwenyezi Mungu Mmoja.

Katika siku za mwisho za uhai wake Mtume (saw) aliwausia mengi Waislamu na kuwataka washikamane na kufuata vizito viwili ambavyo alisema ni Qur'ani na Watu wa Nyumba yake tukufu, akisisitiza kwamba hawatapotea iwapo watashikamana barabara na viwili hivyo.

Monday, November 30, 2015

RAIS MAGUFULI: BILIONI 4 ZA SHEREHE ZA UHURU ZITUMIKE KUPANUA BARABARA YA MWENGE-MOROCO YENYE UREFU WA KILOMITA 4.3


Sehemu ambako utaanzia upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es salaam yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami kufuatia agizo la Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli la kutumia fedha shilingi bilioni nne zilizopaswa kutumika kugharamia Shamrashamra za siku ya Uhuru Desemba 9, 2015 kutumika kufanya upanuzi wa barabara hiyo. PICHA NA IKULU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameamuru fedha zilizopaswa kutumika kugharamia shamra shamra za siku ya Uhuru ambazo zingefanyika tarehe 09 Desemba 2015, kutumika kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.
Tayari fedha hizo kiasi cha shilingi bilioni nne zimepelekwa kwa wakala wa barabara hapa nchini TANROADS kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo, linalopaswa kuanza mara moja.

Akizungumza na Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi PATRICK MFUGALE Ikulu Jijini Dar es Salaam, Dkt. Magufuli ametaka ujenzi wa barabara hiyo uanze haraka ili kukabiliana na adha ya msongamano wa magari katika barabara hiyo
Kujengwa kwa njia hizo kutaifanya barabara ya Morroco hadi Mwenge kuwa na njia tano.

Wakati huo huo, Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba Ikulu Jijini Dar es salaam.
Katika Mazungumzo hayo Prof. Lipumba amempongeza Dkt. Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia kwa kutoa hotuba nzuri ya uzinduzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyokonga nyoyo za Watanzania.
Kwa Upande wake Rais Magufuli amempongeza Prof. Lipumba kwa msimamo wake thabiti wa kupinga ufisadi na amemtakia heri katika shughuli zake.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Dar es Salaam.
30 Novemba,2015